Jumapili, 21 Mei 2017

MAHAKAMA YA WATOTO NI SULUHISHO LA KESI ZA WATOTO.

          Muonekano wa Jengo la Mahakama ya Watoto lililopo jiji Mbeya.
                                          
Na Magreth Kinabo
Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu habari za vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto.
Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa  matamko ambayo yanaitaka jamii kufahamu haki za mtoto ikiwa  ni hatua ya  kuwaepusha watoto wasiathiriwe na tabia hatarishi.
Miongoni mwa viongozi hao ni Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.  Ummy Mwalimu Naibu wake. Dkt. Hamis Kingwallah na viongozi wengine mbalimbali.
Serikali  kwa kushirikiana na viongozi  wa asasi za kiraia  na dini mbalimbali  wameungana ili kuhakikisha  watoto hao wanakua katika maadili mema na kuweza kutimiza ndoto zao.
Mbali na hilo, kuhakikisha kwamba watu wanaowarubuni  watoto  wanachukuliwa hatua za kisheria.
Ili kukababiliana na athari hizo kwa watoto kulingana na mazingira ya jiografia ya nchi, Mahakama  ya Tanzania  kupitia Mpango Mkakati  wa Miaka Mitano wa 2015/2016 hadi 2019/2020, imejenga  Mahakama  nyingine  ya  watoto  katika Jiji la Mbeya hatua ambayo itarahisisha utoaji wa haki kwa wakati.
Kupitia  mpango huo nchini,  hivi  sasa kuna mahakama mbili za watoto ambazo moja iko katika jiji la Dares Salaam na nyingine  jiji la Mbeya.
Uanzishwaji wa Mahakama hizi mbili  unatokana na dhamira  ya Mahakama ya Tanzania, kuhakikisha  inaboresha  huduma  za utoaji  haki    na kusongeza  huduma  karibu  na  wananchi.
Mahakama ya Watoto imeanzishwa kisheria kwa lengo la kushughulikia kesi maalum zinazohusu watoto.
Umri unatambuliwa na Mahakama hiyokuwa ni mtoto ni mtu aliye na umri wa chini ya 18 kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyosema sura ya kwanza, kifungu cha 5 (1) na Sheria ya Mtoto  namba 21 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake, marekebisho  ya mwaka 2006.
Jukumu la Mahakama ni kushughulikia makosa mbalimbali ambayo yanaweza kufanywa na watoto wakiwa katika maeneo ya shuleni, mitaani na sehemu nyinginezo.
Mambo mengine ambayo yanayashughulikiwa na Mahakama hii ni pamoja na taratibu za kuasili watoto na mambo ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na mchakato mzima wa kufanya hivyo, ikiwemo kupokea mashauri ya madai.
Usikilizaji wa mashauri katika Mahakama hii, hufanyika faragha ili kulinda maslahi ya mtoto.
Hivyo,  jamii inapaswa  kuzifahamu  haki  za  mtoto kama vile  haki ya kuishi, kupata huduma bora za afya, mahali pa kuishi, kupata elimu, haki ya kutambuliwa, haki ya kurithi mali, haki ya kutonyanyaswa, ikiwemo kutofanyiwa  vitendo  vya ukatili wa kijinsia.
Kwa  mujibu  wa  taarifa  ya  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya  Jamii, Jinsia,  Wazee  na Watoto Sihaba Nkinga, alipokuwa akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia ukeketaji iliyofanyika Desemba  5, mwaka 2016, Sihaba Nkinga, alisema hali bado ni mbaya.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba taarifa zinaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu wa kike na mtoto mmoja wa kati ya saba wa kiume walifanyiwa ukatili wa kingono.
Kupitia maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, Bi Zainabu Issa ametaka jamii ipige vita vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ili kuwawezesha kufikia ndoto zao ikiwa ni hatua ya kuwawezesha ustawi wa maisha yao na  hatimaye kulijenga taifa la kesho.
“Ninasema kesi dhidi ya ukatili wa watoto sasa zisizidi miezi sita au mwaka, kesi zisikae, muda mrefu Mahakamani. Ninasema sasa mtu akipatikana na hatia ya kumpa ujauzito mwanafunzi au kubaka afungwe miaka 30 jela,” alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Pangani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Appi akizungumza wakati wa maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam, alipiga marufuku vitendo vya baadhi ya walimu kuwafungia geti wanafunzi wanapochelewa kufika shuleni hatua inayowapelekea kushindwa kuingia shuleni na badala yake wanaweza kuwasababishia watoto kujiunga na makundi yenye tabia hatarishi.
Ili kuweza  kuwaepusha  watoto kutoathiriwa  na tabia hatarishi, Mkuu huyo  Appi alipendekeza walimu watumie adhabu mbadala kwa wanafunzi  wanapofanya makosa  wakiwa  shuleni.
Alisema  adhabu mbadala  zinaweza kutolewa na walimu,  wakati wa  kipindi  cha  mapunziko.
Naye Hakimu Mkuu wa  Mahakama  ya  Mwanzo   Mjini Mbeya, Mhe. Onesmo  Zunda akizungumzia  kuhusu uzoefu wa usikilizaji  kesi za watoto  zinazohusiana na  madai na kusema  kuwa amekuwa kesi za ndoa na talaka nyingi  zinatoka  maeneo ya vijijini  kuliko mjini.
“Kuna changamoto katika  kusikiliza kesi  hizi. Miongoni mwa changamoto tunazokabiliana  nazo ni mgawanyo wa mali hasa pale inapotokea  mtu   amefariki dunia  au wazazi kutengana mmojawapo akiwa  ana fedha au mali au kaoa mke mwingine.  Mara nyingi mgawanyo  wa mali huwa unaleta  malalamiko katika  baadhi ya familia,” alisema Mhe. Zunda.
Alifafanua changamoto hiyo katika kesi  hizo amesema inatokea wakati Baba anapotaka kubaki na watoto halafu mama hataki, mara nyingi   mama huwa anataka kubakia na watoto, lakini  baba hataki  kutokana na tabia ya mama.
“Hali hii inamfanya Hakimu kutumia  sheria pale  ndoa  inapotaka kuvunjika, kinachongaliwa zaidi  ni maslahi ya mtoto hata kama  mtoto ana umri wa  zaidi ya miaka 7,” anasititiza Mhe.  Zunda.
Akitolea mfano wa  kesi mojawapo, ambapo alisema kwamba aliwahi kutoa maamuzi  mtoto  abaki  kwa  baba kwa sababu  mama  alikuwa  na tabia  ya  ulevi kwa mujibu wa shuhuda za watoto ili kulinda maslahi na tabia za watoto uamuzi huo.
Ingawa kulingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni jukumu la baba kuwapa watoto matunzo japo  jukumu la kuwalea watoto ni  la wazazi wote. Hata hivyo, mwanamke anatakiwa achangie katika kuhudumia watoto. Iwapo wazazi wametengana amri ya matunzo hutolewa na Mahakama ili baba asiyeishi na mtoto.
 
Matunzo  hayo  huwa  ni pamoja  na kutoa  nguo, chakula, kugharamia masomo shuleni na matunzo yataendelea hadi kufikia umri wa miaka 18.
“Licha ya changamoto tunazozipitia tunajitahidi kuzitatua kwa kutumia  sheria, hakuna rufaa zinazofunguliwa,”alisema Mhe. Zunda.
Mhe. Zunda  alizitaja takwimu   za kesi za ndoa na talaka walizozipokea kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 23, mwaka huu, kuwa  ni 26 na hivyo kati ya hizo  11 bado zinaendelea kushughulikiwa na nyingine zinaendelea kufanyiwa  kazi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa, Mhe. Happiness Chuwa, alisema ili kukabiliana na tatizo la kesi zinazo husiana na watoto ni vema jamii ijenge tabia ya kuwatambulisha watoto na kuandika wosia ili kuondoa migongano inapotokea matatizo ya kifamilia.
Kwa mujibu wa Hakimu  Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto ya  Kisutu  jijini Dar es Salaam, Devotha Kissoka,  akizungumza wakati wa Wiki ya Sheria iliyofanyika mwaka huu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, alisema mtoto akikosa anaweza kupelekwa katika  makao ya watoto.
Ikiwa kuna tatizo, ambalo limeleta mabishano kuhusu mtoto baba yake au wazazi wake ni akina nani? Mahakama hiyo inatoa amri Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya vipimo vya utambuzi (DNA).
Takwimu zinaonesha kuwa kesi za madai katika Mahakama  hiyo kwa kipindi cha  mwaka 2016 ni 154 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2015 ambapo kuliwa kesi 19. Kwa mujibu wa takwimu hizo kesi hizo zimeongezeka kwa asilimia 78.
Hakimu huyo alifafanua kwamba sababu ya kuongezeka kwa kesi hizo ni hali ya uchumi, mmomonyoko wa maadili na kupelekea kuongezeka kwa watoto walio nje ya ndoa.
Aidha, Mahakama hiyo, pia inawajibu wa kusikiliza kesi za jinai  zikiwemo wizi wa kutumia silaha,  kujeruhi  na kuua.
Mhe.  Kissoka aliongeza kuwa ieleweke kwa mujibu wa Sheria, mtoto aliyechini ya umri wa miaka kumi hawezi kutenda kosa la jinai.
Desemba 5, mwaka 2016 Tanzania iliazimisha Maadhimsho ya Kupiga Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto, ikiwemo kufanyishwa kazi ngumu, kubaka na kuolewa wakiwa na umri mdogo, au kutopewa fursa ya kupata elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Mtoto ana haki ya kupata dhamana katika  mashitaka yote isipokuwa yale, ambayo sheria imetamka  hayana  dhamana.
Mhe. Kisoka  alizitaja  adhabu ambazo hutolewa kwa mtoto, kuwa ni kuachiwa kwa masharti kwa kipindi fulani, kisizidi miaka mitatu, adhabu ya kulipa faini, adhabu  ya kuripoti  kwa Afisa Ustawi  wa  Jamii, adhabu ya kupelekwa katika shule maalum.
Pamoja na adhabu hizo mahakama ina uwezo wa kutoa amri mbalimbali kama vile kulipa faini, kuachiwa bila masharti yoyote.
Kutokana na maoni ya watu mbalimbali mfumo mmoja wa kisheria  na nguvu za pamoja zitasaidia kupunguza au kutokomeza vitendo vya kikatili na unyanyasaji  dhidi ya watoto.

Maoni 1 :

  1. Je ni miaka mingapi mtoto anaweza akalelewa na baba ama kuishi na baba yake

    JibuFuta