Jumamosi, 15 Septemba 2018

JAJI MFAWIDHI MWANZA ATEMBELEA MAHAKAMA YA WILAYA MISUNGWI


Na Jovian Katundu, Mahakama ya Wilaya Misungwi

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika amewapongeza watumishi wa Mahakama ya Wilaya Misungwi kwa kusalia na mashauri yasiozidi miezi 3 katika Mahakama za Mwanzo na upanuzi mdogo uliofanyika katika jengo linatumika kwa shughuli za mahakama ya wilaya.

Mhe. Jaji Rumanyika alitoa pongezi hizo alipofanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama hiyo mapema Septemba 14, ikiwa ni mara yake ya kwanza baada ya kuhamia katika Kanda hiyo.

Akisoma risala mbele ya Jaji Mfawidhi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Misungwi Mhe Erick Marley, alieleza kuwa Mahakama yake imejiwekea malengo ya kuhakikisha mashauri ambayo Mahakama yake ina mamlaka nayo yasizidi miezi 6 tangu kufunguliwa kwake.

Akiongea na Watumishi wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Rumanyika amewataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na  ubunifu katika kuwahudumia wateja wanaofika Mahakamani kupata huduma.

Sambamba na hayo, amewasisitiza Watumishi wote wa Mahakama Kanda ya Mwanza kuongozwa na kauli mbiu ya Kanda ambayo ni "Mpe raha mteja, Mahakama ing'are" kauli mbiu ambayo inampa kipaumbele mteja ikiwa ni pamoja na kumuelimisha.

Katika ziara hiyo Mhe Jaji Mfawidhi ameambata na Naibu Msajili Mfawidhi Kanda ya Mwanza, Mhe.Mary Moyo na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Bw. Ibrahimu Mohamed.
      Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Sam Rumanyika akikaribishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Misngwa, Mhe. Erick Marley pindi Mhe. Jaji alipowasili katika Mahakama ya Wilaya Misungwi.
   Mhe. Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza akisalimiana na Watumishi wa Mahakama hiyo mara baada ya kuwasili.


     Akisalimiana na baadhi ya Wananchi waliokuwa wakipata huduma katika Mahakama hiyo.
   Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza akisaini kitabu cha Wageni katika ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Misungwi.

     Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi wakimsikiliza Mhe. Jaji Rumanyika (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.


Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Sam Rumanyika akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Misungwi. Aliyeketi wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Mary Moyo, aliyeketi wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Misungwi Mhe Erick R. Marley na wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi, Mahakama Kuu Mwanza,Bw. Ibrahimu Mohamed.
 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni