Jumatatu, 17 Septemba 2018

ZINGATIENI SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA KAZI KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI


  Na Emmanuel  Oguda, Mahakama Kuu, Shinyanga

Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga wamekumbushwa kutimiza wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia wananchi.

Akitoa maelekezo ya utekelezaji majukumu kwa viongozi hao, mwishoni mwa wiki katika kikao cha Menejimenti Kanda ya Shinyanga kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu.Kikao hicho,kilichojumuisha viongozi wa Mahakama Mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe.Jaji Richard Malima Kibela, amesisitiza juu ya kuzingatia taratibu, miongozo na kanuni mbalimbali zilizotolewa ili kuhakikisha lengo la utoaji haki kwa wakati kwa wananchi linafikiwa kama ilivyo kwenye Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka mitano.

Viongozi hao ambao ni Wahe. Naibu Wasajili, Mahakimu wakazi Wafawidhi, Watendaji wa Mahakama, Wakaguzi wa Ndani, Afisa TEHAMA na Afisa Masjala Mahakama Kuu wamesisitizwa kusimama katika nafasi zao kusimamia masuala ya utendaji kazi zikiwamo taarifa mbalimbali za Mahakama, JSDS 2, Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Fedha, Miundombinu ya Mahakama ili kuleta ufanisi na uwajibikaji kwa kila mmoja kwa nafasi yake.

Aidha, Mhe Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga alisisitiza upendo na kuthaminiana baina ya viongozi hao na watumishi wengine kwa kuwa upendo ndio nguzo kuu ya utendaji bora na ushirikiano huleta mafanikio makubwa katika kufikia lengo la utoaji haki kwa wakati.

Akisisitiza juu ya utendaji bora na utekelezaji wa majukumu,Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Sekela Mwaiseje alisema kuwa kwa sasa Mahakama hiyo inatekeleza majukumu yake vizuri, mbali na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza lakini kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikitatuliwa.

Aliongeza kwamba wananchi wanaelimishwa kupitia kipindi cha elimu kwa wananchi ambacho hutolewa asubuhi kabla ya kuanza Mahakama.

Mhe.Jaji Mfawidhi alisisitiza wananchi waendelee kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali ya Mahakama, huku akiwataka watumishi wote kuzingatia taratibu na miongozo katika utendaji kazi wa kila siku.                                                              

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga,Mhe. JaJi Richard Kibela akizungumzia kuhusu utendaji kazi kwa viongozi wa Mahakama wa kanda hiyo.
Naibu Msajili  Mfawidhi  Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga,Mhe. Sekela Mwaiseje akifafanua jambo.

Wahe. Mahakimu Wafawidhi wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe.  Kibela.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni