Ijumaa, 18 Juni 2021

NENDENI MKAONESHE MOYO WA KUPENDA KUTOA HAKI – JAJI MROSSO

Na Innocent Kansha, Mahakama - Lushoto

Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. John Mrosso amefunga rasmi mafunzo elekezi ya Majaji 24 wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanziba na kuwaomba wakatende haki ili wananchi waone kweli kuwa haki inatendeka na si vinginevyo.

Akizungumza na Majaji hao wakati wa hafla ya kufunga mafunzo elekezi hayo yaliyoanza Mei 31, 2021 na kuhitimishwa Juni 18, 2021. Jaji Msataafu Mhe. Mrosso alisema moyo wa kupenda kutoa haki na kutetea maslahi ya wananchi kwa njia ya kutafsiri sheria ndilo liwe lengo la kwanza katika kazi zenu.

“Kupitia kwenu natamani kuona maboresho makubwa ya Chombo hiki kiwe kimbilio la watu wenye kiu ya kupata haki na hili litawezekana kama mtakuwa mnakumbuka viapo vyenu mara kwa mara”, alisema Jaji Mrosso.

Jaji Mrosso alisema, Jaji kazi yako kubwa ni kutenda haki hata kama mbingu itashuka ili kuondoa dhana na kasumba iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya watu kuwa mahakamani kuna sheria na pengine hakuna haki. Nendeni mkajaribu sana kuilinda na kuitetea sifa nzuri ya Mahakama na kurudisha imani kwa wadau.

Akiongelea suala ya Maadili kwa Majaji, Jaji Mrosso alisema wakati wa kutimiza majukumu yako epuke kuonyesha mrengo au itikadi, epukeni kuonyesha hisia za chama chochote cha siasa na hamtakiwi kufanya siasa mkiwa mahakamani.

“Maadili hayakuzuii Jaji kushiriki mijadala ya nje ya tasnia yako, ondokaneni na dhana ya kujikweza tafuteni namna bora ya kushirikiana na wadau wengine kwa namna isiyo athili viapo vyenu”, alisisitiza Jaji Mrosso.

Jaji Mrosso aliendelea kuwakumbusha Majaji wapya kuwa watakapo kuwa wanaamua mshauri na kutatua migogoro sheria imewapa mamlaka ya utashi (Descretion powers) wakati wa kutoa adhabu, busara hii itumike kwa uangalifu mkubwa bila kupoteza imani kwa wadau.

Jaji Mrosso aliwataka Majaji hao wapya wakawatumikie wananchi wakati wote bila uoga, chuki, huba, wala upendeleo na kumtanguliza Mungu katika majukumu yao ya kila siku ya kutafsiri sheria na kutenda haki.

Bila shaka kwa kupitia programu hiyo ya masomo 30 na wawezeshaji 25 Mahakama ina imani kuwa mmepikwa na mkaiva na kwamba mpo tayari kwenda kufanya kazi yenu ya ujaji kwani vigezo vya kuteuliwa kuwa Jaji ni tofauti na vigezo vya kupandishwa cheo, alieleza Jaji Mrosso.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo aliushukuru uongozi wa Mahakama kwa kuanzisha sera ya mafunzo iliyowezesha kuratibu na kuandaa mafunzo elekezi hayo kwa Majaji wapya.

Aidha, Jaji Kihwelo aliwapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuonyesha utulivu na usikivu wa hali ya juu pia michango yao wakati wa kujifunza ilidhihilisha umahili mkubwa walionao Majaji hao.

“Hakuna kazi ngumu kama Mchekeshaji, unachekesha watu alafu watu hao wasicheke hii ni sawa na uwezeshaji watu wanapokaa kimya utafikiria mambo mengi lakini kwa Majaji hawa hali ilikuwa tofauti kabisa”, alisema Jaji Kihwelo.

Naye Jaji Msataafu wa Mahakama ya Rufani aliyekuwa Mkurugezi wa Mafunzo hayo elekezi Mhe. Salum Massatti alisema Majaji wapya wamepitia masomo 30 kati ya hayo 13 yalilenga kuwajengea uwezo wa kazi za ujaji na masomo 17 yalikuwa ni mafunzo ya ziada kama vile afya, maadili, itifaki, usalama wa Taifa na wa Majaji na mengine mengi.

Jaji Massatti aliongeza kuwa kazi ya ujaji itawataka Majaji kuendelea kujisomea muda wote, na aliwaomba Majaji hao wakalisaidie Taifa kwa maslahi mapana kwa ustawi wa wananchi.


Jaji Msataafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. John Mrosso akiwa anazungumza na Majaji wapya (hawapo pichani)  wakati wa hafla ya kufunga mafunzo elekezi hayo yaliyoanza Mei 31, 2021 na kuhitimishwa Juni 18, 2021 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto nakuwakumbusha kuwa na moyo wa kupenda kutenda haki.

Jaji Msataafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na ambaye alikuwa Mkurugenzi wa mafunzo elekezi ya Majaji wapya Mhe. Salum Massatti akielezea namna mafunzo hayo yalivyowajengea uwezo washiriki (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo elekezi. 

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha sera ya mafunzo iliyowezesha kuratibu na kuandaa mafunzo elekezi hayo kwa Majaji wapya.

Baadhi ya Majaji wapya wakifuatilia mazungumzo ya kuwajengea uwezo kutoka kwa mgeni rasmi  Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. John Mrosso (hayupo pichani) wakati alipokuwa akifunga rasmi mafunzo elekezi

Baadhi ya Majaji wapya wakifuatilia mazungumzo ya kuwajengea uwezo kutoka kwa mgeni rasmi  Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. John Mrosso (hayupo pichani) wakati alipokuwa akifunga rasmi mafunzo elekezi

Baadhi ya Majaji wapya wakifuatilia mazungumzo ya kuwajengea uwezo kutoka kwa mgeni rasmi  Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. John Mrosso (hayupo pichani) wakati alipokuwa akifunga rasmi mafunzo elekezi

Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi (Majaji wapya) mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.

Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi (Majaji wapya) mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.


Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji wanawake Tanzania (TAWJA) na pia wakiwa washiriki wa mafunzo elekezi (Majaji wapya) mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.

Picha na Innocent Kansha na Ibrahim Mdachi


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni