Ijumaa, 9 Julai 2021

KUWENI WABUNIFU ILI KUENDANA NA SOKO LA AJIRA; JAJI MKUU

Na Magreth Kinabo na Mary Gwera- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  amewataka mawakili kuwa na tabia ya kujisomea vitu mbalimbali ili kuweza kubaini fursa za  ajira za kisheria zilizopo nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Akizungumza katika sherehe ya 64 ya kuwapokea na  kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea wapya iliyofanyika leo Julai 09, 2021 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema karne ya 21 ni ya ushindani, hivyo ni lazima wajifunze ili kuweza kuendana na mazingira hayo.

“Karne ya 21 inahitaji watu wenye ujuzi, umahiri na sifa za ziada, bila kutegemea zaidi vyeti, hivyo, ni jukumu lenu ni  kujifunza Tanzania ikoje na kuisoma Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025’’ alisema Prof. Juma.

Aliwataka Mawakili hao wapya kutumia vyema elimu, maarifa na ujuzi waliopata kutoka katika mitaala yenye maudhui ya karne ya 20 kujisomea, kujiongezea na kupata ujuzi zaidi unaohitajika katika Karne ya 21.

 

“Katika usaili, niligundua kuwa mlikuwa na uelewa mkubwa katika maeneo ya kisheria mliyosomea vyuoni. Lakini mlikuwa na uelewa mdogo wa mwelekeo wa Tanzania na nafasi yenu katika huo mwelekeo wa Tanzania,” alieleza.

 

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu aliwakumbusha Mawakili hao kuwa na ujuzi wa mawasiliano, kwa kuzijua vyema lugha za mawasiliano ikiwa ni pamoja na lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa kuwa ndio lugha ya kimataifa.

 

Alisema kuwa Sheria ya Mawakili Sura ya 341 Toleo la 2019 na Sheria iliyoanzisha Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (Tanganyika Law Society Act, Cap 307), zilitungwa Mwaka 1954 na zote mbili zilianza kufanya kazi tarehe  Januari 1, 1955 (miaka 66 iliyopita). Sheria hizi zimebeba matarajio na maudhui, na mahitaji ya karne ya 20.

Ni jukumu lenu wanasheria na Mawakili kuhakikisha kuwa katika utekelezaji, Sheria hizi zilingane na matarajio ya Karne ya 21 na pia ushindani wa Dunia ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda,” alisisitiza.

Aidha, Mhe. Jaji Prof. Juma alitaja baadhi ya changamoto ambazo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) zinakabiliana nazo ambazo ni pamoja na  Kanzidata ya wanachama wa TLS kuwa kubwa ambayo inaonyesha kuwa  wanachama wengi hawalipi ada za uanachama; Mahakama kuwalipa kiasi kidogo cha fedha Mawakili wanaokamilisha majukumu ya utetezi wa washtakiwa wa mashauri pindi kesi zinapokamilika na kadhalika. 

Hata hivyo, Mahakama kwa kushirikiana na Chama hicho wameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo kwa manufaa ya umma.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na Mhe. Jaji Kiongozi, baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Rais wa TLS, baadhi  ya viongozi wengine wa Serikali, baadhi ya Watumishi wa Mahakama pamoja na wageni waalikwa.

Jumla ya Mawakili wapya wa Kujitegemea 308 wamekubaliwa na kuongeza idadi ya Mawakili hao kufikia 10,436. Miongoni mwa Mawakili waliokubaliwa katika sherehe hiyo ni pamoja Mhe. Jaji Augustine Mwarija na Mahakimu nane (8).

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mawakili wapya  (hawapo pichani) mara baada ya kuwapokea na kuwakubali katika sherehe ya 64 iliyofanyika Julai 09, 2021 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Mawakili wapya 308 waliopokelewa na kukubaliwa leo wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu alipokuwa akitoa hotuba yake.
Mhe. Jaji Mkuu akiwakubali Mawakili wapya kwa mujibu wa sheria.
Usikivu makini.
Meza ya upande wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya DPP pamoja Rais wa TLS, Prof. Edward Hoseah wakipokea heshima kutoka kwa Mawakili wapya wa Kujitegemea pindi walipokuwa wakitoa heshima kwa Viongozi hao.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akitoa neno wakati wa sherehe hiyo.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt ambaye pia alikuwa Mshereheshaji wa sherehe hiyo ya kuwapokea Mawakili wapya akitoa mwongozo.
Wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya kutunukiwa vyeti vya kufuzu kuwa Mawakili.
Sehemu ya ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria katika sherehe hizo.









 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni