Jumatatu, 19 Julai 2021

MASHAURI YA WATOTO YASIKILIZWE KWA WAKATI; JAJI MKUU

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezindua rasmi kitabu cha Mkusanyiko wa Mashauri ya Watoto (Compendium of Child Justice Cases) huku akitoa wito kwa Majaji, Mahakimu na wadau wa ‘Haki Mtoto’ nchini kuwezesha mashauri ya Watoto kusikilizwa na kumalizwa kwa wakati.

Akizindua rasmi kitabu hicho leo Julai 19, 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa maamuzi yanayotolewa na Mahakama nchini yamebeba na kusheheni maelekezo, mafundisho na busara zinazohitajika katika kulinda haki za mtoto na hivyo maamuzi yanayogusa haki na maslahi ya mtoto ni lazima yapatikane kwa urahisi na yakatumiwa kama rejea na wadau wote wa haki za mtoto.

“Sisi sote tukumbuke kuwa, ‘Haki Mtoto’, kwa maana ya haki, ulinzi na ustawi wa mtoto; haipatikani Mahakamani peke yake. Bali, inapatikana katika “Mfumo Jumuishi wa Haki Mtoto” ambao ni mwavuli mpana zaidi ya mahakama, polisi au ustawi wa jamii mmoja mmoja. Tukumbuke kuwa, katika Haki Mtoto, kila mmoja wetu atimize wajibu wake,” alisisitiza.

Akitaja faida kadhaa za kitabu hicho, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa kitabu hiki kinakumbusha kuwa, zipo sheria nyingi zaidi ya Sheria ya Mtoto ya 2009 [Law of the Child Act Na. 21 ya 2009], na kuwa Haki Mtoto haipatikani ndani ya Sheria moja tu bali kuna vifungu vya Katiba, Sheria mbalimbali, Kanuni, Taratibu, Mazoea na vigezo vingi ambazo kwa pamoja vinajenga mfumo wa kufahamu mapana na marefu ya Haki ya Mtoto.

“Naweza kusema kuwa mkusanyiko huu ni ‘One-Stop Centre’ kuhusu kesi za Haki mtoto na muhimu katika kazi za polisi, wapelelezi, mahakimu, majaji, maafisa ustawi wa jamii, magereza na hata kwa watunga sera wanaposhughulikia ‘HAKI MTOTO’, alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Prof. Juma alitoa wito kwa Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa kanda zote, Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa na Mahakama za Wilaya kuhakikisha kuwa katika maeneo yenu ya kazi kuna nakala za kitabu hiki ili kusaidia kufanya rejea pale inapobidi kufanya hivyo.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaohudumia Watoto (UNICEF), Bi. Sampathi Perera alieleza kuwa uzinduzi wa kitabu hicho ni fanikio litakalowawezesha Majaji na Mahakimu kuendelea kutoa maamuzi sahihi kuhusu mashauri ya Watoto.

Sambasamba na hilo, katika hafla hiyo, Mhe. Jaji Mkuu alizindua pia Ripoti ya Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto Tanzania, Mafunzo hayo yaliendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2020 chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF).

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa mafunzo yaliendeshwa kwa wadau wa haki za watoto Mia Saba na Arobaini na Sita (746) katika kanda zote za Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo kupitia mafunzo hayo.

Uzinduzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) 2018/2019-2022/2023 wa kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya sheria nchini.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Sheria nchini wanaohusika na haki za mtoto wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu wa ngazi mbalimbali, Wawakilishi wa Taasisi za Serikali, Wawakilishi kutoka Mashirika yasiyo ya Serikali na Wawakilishi wa UNICEF.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akionyesha Kitabu cha mkusanyiko wa kesi za watoto “Compendium for Juvenile cases” mara baada ya kukizindua rasmi.Wengine ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mhe. Jaji Mkuu ya Utafiti na Mafunzo-Mahakama, Mhe. Augustine Mwarija (kushoto) na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, uzinduzi huo umefanyika leo Julai 19, 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikata utepe  kuashiria uzinduzi wa Ripoti ya tathmini ya mafunzo kwa Wadau wa Haki za watoto “Impact Assessment on trainings of Juvenile Justice Frontline workers” wanaoshuhudia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija (kushoto) na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Gerald Ndika.

Wakionyesha vitabu vya ripoti hiyo mara baada ya kuzindua.

Mhe. Jaji Mkuu akimkabidhi Mwakilishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Kitabu cha Mkusanyiko wa Kesi za Watoto na Ripoti ya Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto mara baada ya uzinduzi.

Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji Wafawidhi, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Viongozi wa Mahakama na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha mkusanyiko wa kesi za watoto na Ripoti ya Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto uliofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Bi. Sampathi Perera akielezea jinsi Tanzania ilivyopiga hatua kubwa katika kushughulikia masuala ya watoto, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uzinduzi wa kitabu hicho muhimu.


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa ufafanuzi wa namna ya uandaaji wa Kitabu cha mkusanyiko wa kesi za watoto na Ripoti ya Tathmini ya Mafunzo kwa Wadau wa Haki za Watoto ulivyotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau.

(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni