Ijumaa, 20 Februari 2026

MAHAKAMA KUU GEITA YAFANYA BONANZA LA MICHEZO KUFUNGUA MWAKA 2026

Na DOTTO NKAJA – Mahakama, Geita

Timu ya Mpira wa Miguu ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita, hivi karibuni ilimenyana vikali na Timu ya Polisi Mkoa wa Geita katika mchezo uliovutia hisia za mashabiki wengi, licha ya kupoteza kwa mabao 4-2.

Mchezo huo wa kirafiki ulifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Waja uliopo eneo la Magogo, mkoani Geita. Kuanzia dakika za mwanzo, timu ya Mahakama ilionyesha kiwango cha juu cha mchezo kwa kushambulia kwa kasi na nidhamu kubwa.

Kipindi cha kwanza kilitawaliwa na Mahakama ambapo walifanikiwa kufunga magoli mawili safi yaliyoamsha shangwe kwa mashabiki wao. Ushirikiano mzuri kati ya safu ya kiungo na ushambuliaji uliwapa nafasi nyingi za kufunga, huku safu ya ulinzi ikidhibiti vyema mashambulizi ya wapinzani.

Hata hivyo, kipindi cha pili kilileta ushindani mpya baada ya Polisi Mkoa wa Geita kurejea uwanjani wakiwa na ari na mikakati mipya. Walifanikiwa kusawazisha kwa kufunga magoli mawili ya haraka na kurejesha matumaini yao. Baada ya kusawazisha, waliendelea kushambulia kwa nguvu na kuongeza magoli mengine mawili, na kufanya jumla ya magoli yao kufikia manne.

Mchezo huo ulimalizika kwa Polisi Mkoa wa Geita kuibuka na ushindi wa magoli 4–2 dhidi ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita. Licha ya matokeo hayo, Mahakama Kuu Kanda ya Geita wanastahili pongezi kwa kiwango bora walichoonesha hasa katika kipindi cha kwanza, wakidhihirisha ushindani na umoja mkubwa.

Baada ya mashindano hayo, watumishi na wadau wote walikutana kwa ajili ya kufungua mwaka. Waliohudhuria ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina na Jaji wa Mahakama Kuu Geita, Mhe. Giffin Mwakapeje.

Wengine ni Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Waendesha Mashtaka wa Mkoa wa Geita pamoja na Polisi Mkoa wa Geita, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna akitoa maelekezo kwa wachezaji katika Timu ya Mahakama Kanda ya Geita.

Wachezaji kutoka Polisi Geita wakijiandaa kuanza mashindano na Timu ya Mahakama Geita.

Timu ya Mahakama Kanda ya Geita ikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mchuano na Timu ya Polisi Geita.

Innocent Mwandoje wa Timu ya Mahakama akichuana na mchezaji kutoka Polisi Mkoa Geita.

Kiungo mshambuliaji wa Timu ya Mahakama Abel Lucas Bunzali akiwa kasi kuelekea lango la Police Geita. 

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fredrick Lukuna akiwakilibisha wageni.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina, akiwahimiza wadau wa Mahakama kuongeza umoja na mshikamano ili kuongeza kasi ya kutoa haki mapema ipasavyo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni