Jumatano, 17 Aprili 2024

BARAZA LA WAFANYAKAZI LINAWAJIBU WA KUJENGA MAHUSIANO BORA KAZINI; JAJI NONGWA

Na Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya 

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa ameongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika tarehe 15 Aprili, 2024 katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu Mbeya.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Mhe. Nongwa aliwataka wajumbe kushiriki kikamilifu katika kuwasilisha hoja zao kwani Baraza la wafanyakazi ndilo jukwaa la kisheria la majadiliano ya pamoja kati ya viongozi na watumishi katika utumishi wa umma.

Mhe. Nongwa alisema kupitia Baraza la wafanyakazi ndiyo njia rasmi ya kujadili namna bora ya kujenga mahusiano kazini hususani katika eneo la wajibu na maslahi ya watumishi kwa pamoja ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kuwashirikisha wafanyakazi katika dhana ya uongozi wa pamoja.

“Nichukue nafasi hii kupitia kikao cha Baraza hili kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kufanya mafunzo ya watumishi kwa kada za wasaidizi wa kumbukumbu na waandishi waendesha ofisi nchi nzima, hatua hiyo inaleta tija na ufanisi katika utendaji wa kazi kwa watumishi wetu,” alisema Jaji Nongwa. 

“Sisi kama Mahakama tunaongozwa na Mpango Mkakati tuendelee kutoa elimu kuhusu maboresho yote yaliyokwishafanyika na yanayoendelea kufanyika. Hii imesaidia kuongeza ufanisi mkubwa wa kazi kwa watumishi wetu, na tumeendelea kushuhudia wateja wetu wakipatiwa huduma nzuri na kwa wakati bila manung’uniko yoyote,” alisema Mhe. Nongwa.

Naye, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu ambaye pia ni mjumbe katika Baraza hilo aliwasisitiza wajumbe kwamba hoja zote zilizojadiliwa zinawakumbusha watumishi umuhimu wa kuongeza bidii katika kujifunza na kujiendeleleza ili kuongeza ufanisi wa kazi na kujiwekea misingi imara ya kujenga utumishi ulio bora.

“Hoja zote zilizojengwa hapa zinakwenda kuimarisha misingi bora ya utendaji kazi na kuongeza tija kwa chombo chetu cha utoaji haki na Taifa kwa ujumla. Hivyo nawasisitiza kuwajibika, kushirikiana na kuimarisha weledi katika kazi zetu,” alisistiza Mhe. Temu.

Baraza hilo lilihudhuriwa na wajumbe kutoka Mkoa wa Mbeya na Songwe na kufanya jumla ya wajumbe 56 walioshiriki katika baraza hilo.

Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa (katikati) akieleza jambo wakati alipokuwa akiongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya tarehe 15 Aprili, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya

Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama Kuu Mbeya ambaye ni katibu katika baraza hilo Bw. Charles Mapunda akielezea jambo wakati wa Baraza hilo.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa (kulia) na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda Mbeya Mhe. Aziza Temu wakifuatilia hoja za kikao hicho.

Sehemu ya Washiriki wa Baraza wakifuatilia hoja mbalimbali kwa makini.

Sehemu ya Washiriki wa Baraza wakifuatilia hoja mbalimbali kwa makini.

Washiriki wa Baraza hilo la wafanyakazi wakiimba wimbo wa Mshikamano (solidarity forever)

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kyela Mhe. Andrew Njau ambaye ni mjumbe wa Baraza hilo akichangia hoja wakati wa kikao hicho.


Washiriki wa Baraza hilo la wafanyakazi wakiimba wimbo wa Mshikamano (solidarity forever)

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni