Jumanne, 8 Julai 2025

KUMECHANGAMKA SABASABA

  • Viongozi wamiminika kwenye Banda la Mahakama

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali leo tarehe 8 Julai, 2025 wametembelea Banda la Mahakama ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa, Saba Saba, kujionea zoezi la utoaji elimu kwa wananchi katika masuala mbalimbali ya kisheria.

Banda la Mahakama lipo katika Maonesho hayo kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Temeke Jijini Dar es Salaam likiwa limesheheni watalaam waliobobea kwenye sekta ya sheria, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA, uboreshaji wa miundombinu ya majengo na maeneo mengine mbalimbali muhimu.

Viongozi hao ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini na Majaji wanne wa Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.

Wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Masoko na Mitaji, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumushi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.

Viongozi hao wamejionea jinsi watalaam wa Mahakama na Wadau walivyojipanga kushiriki kwenye zoezi la utoaji elimu kwenye masuala mbalimbali ya kisheria na kwa wakati tofauti wameelezea kufurahishwa na maandalizi ambayo yamefanyika.

Jana tarehe 7 Julai, 2025, Viongozi wengine, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winfrida Korosso, Mhe. Dkt. Mary Levira na Mhe. Gerson Mdemu walitembelea Banda la Mahakama na kushuhudia jinsi wananchi kutoka viunga mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam wakinufaika na zoezi la utoaji elimu ya sheria.

Alikuwepo pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Eliakim Maswi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt.

Banda la Mahakama ya Tanzania linajumusha watalaam kutoka Kurugenzi ya Menejimenti ya Mashauri, Kurugenzi ya Ujenzi na Usimamizi wa Majengo, Kurugenzi ya Mipango, Kurugenzi ya TEHAMA, Huduma kwa Mteja na Kurugenzi ya Huduma za Mahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili.

Wapo pia watalaam kutoka Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mahakama ya Rufani na Masjala Kuu ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Watoto.

Kadhalika, Banda la Mahakama limesheheni watalaam kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka, Idara ya Huduma za Maktaba, Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi.

Kuna Wadau wanaoshirikiana na Mahakama katika zoezi la utoaji elimu, wakiwemo Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania-TAWJA, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto-IJA na Wakili Mkuu wa Serikali.

Wadau wengine ni Chama cha Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu-LHRC na Chama cha Mawakili Tanganyika-TLS.































(Picha na INNOCENT KANSHA- Mahakama 77)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni