· Ni katika Mkutano wa Wadau kuhusu ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani
· Asisitiza
pia uwajibikaji wa wadau wa mnyororo wa haki
· Ashauri
mikutano hiyo kufanyika angalau mara nne kwa mwaka
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju amewahimiza Wadau wa Mahakama nchini juu ya
umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na mahusiano ili kutekeleza
jukumu la utoaji haki mapema ipasavyo na kwa ustawi wa wananchi.
Akizungumza leo tarehe 24
Septemba, 2025 wakati akifungua Mkutano wenye ajenda kuu ya
Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu- Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju amesema ushirikiano na
mshikamano ni wa lazima na ni takwa la kikatiba, kisheria na hata Dira ya Taifa
ya Maendeleo, 2050.
“Nawashukuru Viongozi kwa
kutenga muda wenu kuja kushiriki katika mkutano huu muhimu, niseme tu kwamba
ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu yetu Mahakamani
umejengwa kwenye Katiba na kwenye sheria mbalimbali zinazoanzisha Taasisi zetu hizi,
kwa hiyo ni ushirikiano wa kulazimika na wala sio wa hiari, na wote sisi nia
yetu ni ustawi wa wananchi,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema kuwa,
kila mdau wa mnyonyoro wa haki ni muhimu, kunapokuwa na ushirikiano na uhusiano
wa namna hiyo kwa wadau, kuna umuhimu mkubwa ambao ni pamoja na kuyaimarisha,
kutambua mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zinazokabili ushirikiano na
mahusiano hayo na kuziwekea mikakati ya kuzitatua.
“Kwahiyo mambo haya
yanatuhusu sisi wote, sisi wote tumewekwa na wananchi kwa ajili ya kuwatumikia
ili kufikia ustawi wao, tumepewa majukumu ya uwajibikaji, tunapotekeleza
majukumu yetu na sisi sasa tunazungumza kwenye huu mnyororo wa haki ambao
unaishia Mahakamani, Ibara ya 25 ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano inasema wajibu wa kushiriki kazini,” ‘Kazi pekee ndio huzaa utajiri wa
mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu na
kila mtu anao wajibu (a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika
kazi halali na ya uzalishaji mali na (b) kutimiza nidhamu ya kazi na
kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya
pamoja na yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju ameeleza
kwamba, Taasisi zote ikiwemo Mahakama zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria,
hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu kuimarisha ushirikiano na
mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki Mahakamani.
Aidha, Jaji Mkuu
ameongeza kwa kushauri kuwa, vikao hivyo viwe endelevu na vifanyike angalau
mara nne kwa mwaka (kila robo mwaka) ili kupata fursa ya kujadiliana masuala
mbalimbali yanayohusu Mahakama na wadau wake na hatimaye kupata suluhisho ya
changamoto mbalimbali kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuzitatua ili kusonga
mbele.
Kadhalika, Mhe. Masaju
amesema kwamba mkutano huo umekuja wakati muafaka, ambapo kuna Dira ya Taifa ya
Maendeleo ya mwaka 2050 ambapo msingi mkuu wa Dira hiyo ni Utawala, Amani,
Usalama na Utulivu na moja ya kipaumbele cha kwanza ni Utawala Bora na Haki,
kipaumbele cha pili ni Serikali za Mitaa Imara na zenye ufanisi na cha tatu ni
Utumishi wa Umma unaowajibika na kipaumbele cha nne ni Amani, Usalama na
Utulivu. Amesema wadau wote ni wahusika katika kusimamia na kutekeleza masuala
hayo.
Aidha, Jaji Mkuu
amesisitiza juu ya kipengele cha tatu cha Dira hiyo kinachohusu 'utumishi wa umma unaowajibika' kwa kutoa rai kwa wadau hao
kuwa, kila mmoja anawajibika kutekeleza malengo ya kudumisha utawala bora
kwenye utekelezaji wa upatikanaji wa haki Mahakamani na amani, usalama na
utulivu.
"Ikiwa Serikali inapata mamlaka yake kutoka kwa wananchi na lengo lake kuu ni ustawi wa wananchi na inawajibika kwa wananchi, sisi ambao ni watumishi wa umma tuna wajibu mkubwa sana kuwajibika katika kutekeleza majukumu yetu," ameeleza Mhe. Masaju.
Aidha Mhe. Masaju
amerejea ukurasa wa 63 wa Dira hiyo ambao unahimiza ushirikiano katika sekta
mbalimbali, inasema ‘ili kuhakikisha Dira 2050 inatekelezwa kwa ufanisi,
Serikali imeweka mfumo imara wa usimamizi unaozingatia malengo yake mahsusi,
mfumo huu umekusudia kuhimiza uwajibikaji, ukihitaji uongozi mahiri na ulio
makini katika ufuatiliaji, aidha mfumo unahimiza matumizi ya mbinu zinazotoa
matokeo yanayopimika......’
‘.....msingi wa mkakati
huu ni mabadiliko makubwa ya kifikra yakilenga vitendo badala ya maneno na
matokeo badala ya ahadi, uongozi, taasisi pamoja na watendaji na wadau wote
wanapaswa kuwajibika ili kutimiza malengo ya Dira kwa ufanisi, Taasisi imara na
mifumo Madhubuti inayolenga kuondoa uzembe, inayohimiza uwajibikaji na
kuchochea ufanisi itakuwa nguzo kuu ya utekelezaji wa Dira 2050...Dira imeweka
mfumo madhubuti wa utawala unaohakikisha utekelezaji unafanyika kwa nidhamu,
sera zinasomana, taasisi zinakuwa imara na sekta na wadau wote wanashirikiana.’
Amesema kwamba, mkutano huo utakuwa pia kichocheo kwa taasisi nyingine kuandaa mikutano kama huo na kuwashirikisha wadau muhimu kwenye Sekta ya Sheria inayohusu utoaji haki.
Aidha, Jaji Mkuu
amesisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano ili mashauri yaweze kukamilika mapema
ipasavyo huku akigusia mashauri ya jinai, mashauri ya kodi, mashauri ya
biashara, mashauri ya migogoro ya kibenki na mengine.
Kadhalika, Mhe. Masaju amewaomba Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kufuatilia utekelezaji na kutoa mrejesho kuhusu utekelezaji wa Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai ambacho kinasema kwamba mashauri hayatafunguliwa Mahakamani isipokuwa kama upelelezi umekamilika isipokuwa kwa mashauri yanayosikilizwa na Mahakama Kuu na yaliyotajwa na kifungu hicho yanayoitwa 'Serious Offences' (Makosa Makubwa ya Jinai) ambayo yametajwa kwa mujibu wa 'Criminal Procedure Act' (Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai).
"Nawaomba Jeshi la Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mtusaidie kufuatilia utekelezaji wa kifungu cha i (34) je inatekelezwa? tuleteeni taarifa hili ni kosa ambalo mtu anapaswa akamatwe wakati upelelezi umekamilika na kupelekwa Mahakamani, lakini pia tusaidieni kufuatilia na kutupatia taarifa za yale mashauri ambayo yanasikilizwa na Mahakama za Mahakimu isipokuwa Mahakama za Mwanzo ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka na sisi mahakamani tumeshajiwekea utaratibu kwamba yamalizike ndani ya miezi sita, je yapo ambayo hayajamalizika ambayo yapo kwenye hatua ya 'trial'? au yapo kwenye upelelezi, tuleteeni taarifa hizo ndio ushirikishwaji huu ambao tunazungumza sisi Wadau wa Haki Mahakamani tukifanya hivyo tutapiga hatua," amesisitiza Jaji Mkuu.
“Nilipokutana na Taasisi za utatu tarehe 19 Agosti, 2025 jijini Dodoma, nilipokuwa nashiriki kwenye ule mkutano mengine niliyowashirikisha nitarejea kidogo hapa, nilisema nakusudia kutengeza Kanuni zitakazowezesha wale watu wanaoshtakiwa kwa makosa ya jinai kwenye Mahakama za Mahakimu ispokuwa Mahakama za Mwanzo na wao hao washtakiwa na Mahakama hizo wao nao wawe na ushahidi wa upande wa kesi za mashtaka ili wajue kesi zao, tumetengeneza sisi hapa rasimu ya hizo kanuni tumeziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, tumeziwasilisha kwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ili wazipitie, watuletee maoni yao kabla hatujazitangaza kwenye Gazeti la Serikali, ilikuwa ifikapo tarehe 19 Septemba, 2025 lakini tumechelewa kwakuwa tunasubiri maoni ya wadau," alisisitiza Jaji Mkuu.
Ameongeza kuwa, msingi wa mabadiliko ya kanuni hizo umejengwa kwenye Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 'usawa mbele ya sheria' ibara ndogo ya sita ya Ibara ya 13 (b) inasema kila anayeshitakiwa Mahakamani kwa kosa la jinai atachukuliwa kwamba hana hatia hadi itakapothibitishwa hivyo na Mahakama.
"Sasa hivi mtu anashtakiwa anaenda Mahakamani hajui kitu kitakachomtokea huko mbeleni, Mahakama inakuwa haina ushahidi, mshtakiwa naye hajui kwahiyo Mahakama inakuwa katika mazingira magumu sana ya kuweza kufanya maamuzi yanayostahili ni tofauti na ilivyo sasa Mahakama Kuu unakuta Mahakama ina ushahidi wote, mshtakiwa naye ana ushahidi wote, huu kwa ni mfumo shirikishi kwahiyo Mahakama inakuwa katika mazingira mazuri ya kufanya maamuzi sahihi," amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju ameeleza kuwa, kupatikana kwa kanuni hizo kutawezesha kuimarisha umakini katika upelelezi kwa kuwa upelelezi ukiwa mzuri na maamuzi yatafanyika vizuri, kupunguza ubambikizaji wa mashauri, itasaidia kuharakisha usikilizwaji wa kesi kwa haraka na hatimaye kutoa maamuzi mapema, italeta pia umakini katika utoaji haki, itadhibiti vitendo vya rushwa, itaendana na Katiba ambayo inataka usawa mbele ya sheria na vilevile itasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani.
Mhe. Masaju amewaomba
ushirikiano wadau hao, kuwa huru kutoa maoni yao katika mkutano huo na kuweka
mikakati thabiti itakayoboresha utendaji kazi ya utoaji haki na hatimaye
Mahakama ya Tanzania iwe moja kati ya mihimili yenye hadhi duniani.
Naye Kaimu Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba amesema kufanyika kwa mkutano
huo ni sehemu ya utekelezaji wa Nguzo namba tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama
ya Tanzania 2020/2021-2024/2025 ya Kuimarisha Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji
wa Wadau.
“Kupitia nguzo ya Tatu ya
Mpango Mkakati wa Mahakama, tumesisitizwa juu ya kuimarisha ushirikiano na
wadau wa sekta ya haki kama mhimili muhimu unaoimarisha misingi ya utawala
bora. Katika utekelezaji wa nguzo hii, hivi karibuni tumeshuhudia juhudi zako za
dhati Mheshimiwa Jaji Mkuu juu ya kuimarisha dhana nzima ya ushirikishwaji wa
wadau. Ushiriki wako katika matukio mbalimbali, ikiwemo ziara uliyofanya Gereza
Kuu Isanga tarehe 10 Julai, 2025, ufunguzi wa mjadala wa kitaifa juu ya
maboresho ya sheria na sera tarehe 19 Agosti, 2025, ufunguzi wa kikao kazi
baina ya ofisi ya DPP, DCI, PCCB na DCEA tarehe 20 Agosti, 2025, ufunguzi wa
mkutano wa tisa wa kamati ya utatu tarehe 25 Agosti, 2025, na mengineyo mengi,
unathibitisha juhudi hizo,” amesema Mhe. Kagomba.
Kaimu Jaji Kiongozi huyo amesema, kupitia ushirikiano wa dhati baina ya Mahakama na wadau, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na wadau wote waliokusanyika katika mkutano huo, utajenga taswira moja ya utumishi wa haki na kuongeza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa utoaji wa haki.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Wadau wa Mahakama leo tarehe 24 Septemba, 2025 wakati akifungua Mkutano wenye ajenda kuu ya Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Sehemu ya
Viongozi wa Mahakama walioshiriki katika Mkutano wa Wadau wa
Mahakama kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya
Utoaji Haki mahakamani uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji
Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Wadau mbalimbali walioshiriki katika mkutano huo wakifuatilia kinachojiri katika mkutano huo.
Jaji wa Mahakama
ya Rufani Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija
akizungumza jambo wakati wa Mkutano huo.
Meza kuu
ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati)
wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mkutano kati ya Mahakama na Wadau
kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika
Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani uliofanyika leo tarehe
24 Septemba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu- Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani
Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija na kulia ni Kaimu
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha za pamoja na Mkutano kati ya Mahakama na Wadau waliohudhuria Mkutano uliobeba ajenda ya Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki mahakamani uliofanyika leo tarehe 24 Septemba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija na kulia ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Abdi Kagomba.
(Picha na MARY
GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni