Jumapili, 7 Desemba 2025

WANAFUNZI KOZI YA POLISI JESHI WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO IJC MOROGORO

Na ASHA JUMA-Mahakama Morogoro

Katika kuimarisha uelewa wa taratibu za utoaji haki nchini, wanafunzi 96 wa kozi ya Polisi Jeshi Daraja la Kwanza kutoka Shule ya Mafunzo ya Huduma Pangawe, wamefanya ziara ya mafunzo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro.

Ziara hiyo ya siku tatu ilikwa ni sehemu ya utekelezaji wa somo lao la Sheria ya Ushahidi, ikilenga kuwapatia wanafunzi hao maarifa ya moja kwa moja kuhusu mchakato wa kimahakama, haki za watuhumiwa na washtakiwa kabla na baada ya kukamatwa, pamoja na mbinu sahihi za utoaji ushahidi mahakamani.

Wanafunzi hao wakiwa na Wakufunzi wao, wakiongozwa na Kapteni Yona Mtaita, walifundishwa juu ya taratibu za Mahakama za jinai na madai, hatua mbalimbali za uendeshaji wa kesi, haki ya rufaa na namna Mahakama ya Rufani inavyofanya kazi.

Vilevile, walifundishwa kuhusu kinga na utetezi wa kisheria, haki ya kusikilizwa, haki ya kuwa na wakili na nafasi ya wakili katika kutetea mteja kupitia vielelezo na mashahidi.

Mada nyingine muhimu zilizotolewa ni uwasilishwaji wa nyaraka na vielelezo vya ushahidi mahakamani ikiwemo aina za vielelezo vya ushahidi, maoni ya kitaalamu kutoka kwa madaktari, wataalamu wa vidole na sayansi, pamoja na jinsi Mahakama inavyochambua uhalali, uzito na uhusiano wa vielelezo hivyo na kesi husika, mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA] inavyo fanya kazi pamoja na Adhabu mbadala

Zaidi ya hayo, wanafunzi walifahamishwa dhumuni na faida za Vituo Jumuishi vya utoaji haki (IJC), ambavyo huwezesha huduma zote za kisheria kupatikana sehemu moja kwa ufanisi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa haki jinai.

Miongoni mwa wakufunzi waliotoa elimu hizo ni pamoja na  baadhi ya  Mahakimu Wakazi wa Mkoa wa Morogoro, Ofisi ya TEHAMA, Chama Cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) na Ofisi ya Uangalizi.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, moja ya mwanafunzi Koplo Rodgers Lucas John alieleza kuwa wamefurahia mafunzo hayo ya vitendo na kueleza kuwa yamewasaidia kuongeza uelewa wa kina kuhusu mfumo wa haki na namna vyombo vya sheria vinavyofanya kazi kwa kushirikiana.

Aidha, wamejifunza pia namna ambavyo Mahakama mbalimbali zinavyofanya kazi kimuundo kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufani.

“Tumefurahi kujifunza namna Mahakama ya Rufani ya Tanzania inavyofanya kazi, pia tumefurahi sana kupata nafasi ya kushuhudia uendeshwaji wa mashauri ya madai kwenye moja wapo ya vikao vya Mahakama ya Rufani hapa Morogoro,” alisema Koplo Rodgers

Ziara hiyo imekuwa chachu kwa wanafunzi hao kuelekea kuwa maofisa wa usalama wenye maarifa na weledi wa hali ya juu katika kulinda haki za binadamu na kuhakikisha sheria inatekelezwa kwa haki.


Picha ya pamoja ya wanafunzi  wa kozi ya Polisi Jeshi Daraja la Kwanza kutoka Shule ya Mafunzo ya Huduma Pangawe, pamoja na wenyeji wao wakiwa wamewasili.

Picha ya wanafunzi  wa kozi ya Polisi Jeshi Daraja la Kwanza kutoka Shule ya Mafunzo ya Huduma Pangawe wakipatiwa mafunzo katika ukumbi wa Mahakama.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni