Alhamisi, 18 Aprili 2024

OFISI YA MSAJILI MKUU NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YA KIKATIBA

 

 Magreth    Kinabo -Mahakama

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Wilbert Chuma, amewataka viongozi na watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuendelea kutoa  ushirikiano kwa Msajili Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya ili aweze kutekeleza majukumu yake ya shughuli za kimahakama kwa mujibu wa Katiba.

 

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 18 Aprili,2024 kwenye hafla ya makabidhiano  iliyofanyika  katika ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania iliyopo katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ambapo Mhe. Jaji Chuma, amekabidhi kiti hicho na vitendea kazi kwa Msajili huyo mpya baada yeye kuteuliwa kuwa Jaji.

 

Awali kabla kukabidhi kiti hicho, Mhe. Jaji Chuma alisema kimsingi, Msajili Mkuu ni nguzo muhimu katika kutekeleza matakwa ya Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara hiyo inabainisha kwamba,mamlaka ya utoaji haki katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, itakuwa mikononi mwa Mahakama. 

 

“Katika kutekeleza jukumu hili la kikatiba, Mahakama inamtegemea sana na inatarajia Msajili Mkuu kusimamia ipasavyo shughuli za kimahakama.Hivyo,  ninawaomba muendelee kutoa ushirikiano kama mlivyokuwa mnaniapatia,” alisema Mhe Jaji Chuma.

 

Mhe. Jaji Chuma alisema kama alivyoeleza hapo awali, Msajili Mkuu ndiye kiungo kati ya Mahakama na wadau kuhusu masuala yote ya sheria na wale wanaohusika na mnyororo wa utoaji haki. Hivyo wakati akiwa Msajili Mkuu, katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake, Mahakama kwa kushirikiana na wadau wa haki jinai na madai ilipata mafanikio makubwa ambayo yamewanufaisha wananchi.

 

Aliyataja mafanikio hayo ni uboreshaji wa miundombinu, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma za kimahakama, uondoshaji wa mlundikano wa mashauri ya muda mrefu ambayo ilikuwa kero kubwa kwa wananchi, umalizaji wa mashauri ndani ya kipindi kifupi, utoaji wa elimu kwa wananchi n.k. 

 

“Kwahiyo, Mhe. Eva Kiaki Nkya, hatuna budi kuendelea kushirikiana na wadau katika kutatua changamoto za wananchi. Nitoe rai kwa wadau kuendelea kuwekeza katika mifumo ya TEHAMA inayosaidia kutoa na kupokea hudma kwa urahisi,”alisisitiza.

 

Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha,Mhe. Sylvester Kainda, ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji alikuwa Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, alisema Mahakama kwa sasa uwezo wake wa kusajili na kuamua mashauri una kwenda kasi huku akitolea mfano kwa kipindi cha mwaka 2021 ilisajili takribani mashauri 250,000 na kwa sasa ni takribani mashauri 300,000, hivyo yayoamuliwa ni kwa kiasi hicho hicho kwa mwaka,hivyo uwezo wa uondoshaji wa mashauri ni takribani asilimia 100.

 

Mhe. Jaji Kainda alitolea mfano wa Mahakama ya Rufani Tanzania kuwa uwezo wa kumaliza ni takribani asilimia 100, ambapo alisema kwa mwaka ilisajili mashauri takribani 1800 na kuamua mashauri takribani 1300, mwaka 2022 ilisajili 2000 na 2023 ilisajili mashauri 3000 na yaliamuliwa kwa kiwango hicho hicho.

 

Alisema mwaka 2023 Mahakama ya Tanzania iilikuwa na mlundikano wa mashauri 2500, kati ya hayo mahakama za chini zilikuwa na asilimia tano, ambapo Mahakama ya Rufani Tanzania ilikuwa na mlundikano 1100 sawa na asilimia 44.

 

Tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili Mkuu ilisimamiwa vema na Wasajili Wakuu wafuatao, Mhe. Ignus P. Kitusi kati ya mwaka 2012 hadi 2015, (kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania) Mhe. Katarina T. Revokati kati ya mwaka 2015 hadi 2019 (kwa sasa ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tanga) na Mhe. Wilbert M. Chuma kati ya mwaka 2020 hadi 2023 (kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza). Sasa ni Mhe. Eva Kiaki Nkya aliteuliwa na kuapishwa tarehe 4 Aprili, 2024. 

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Wilbert Chuma akimkabidhi vitendea kazi vya Ofisi ya Msajili Mkuu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Mhe. Eva Nkya.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) akimkabidhi kitabu cha taarifa ya makabidhiano cha Ofisi ya ya Msajili Mkuu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Mhe. Eva Nkya.(Katikati) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Prof. Elisante Ole Gabriel.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Wilbert Chuma(katikati) akitoa hotuba yake ya makabidhiano, (kushoto) ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na (kulia) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Prof. Elisante Ole Gabriel.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya(katikati) akizungumza jambo mara baada ya kukabidhiwa ofisi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Wilbert Chuma(kushoto) na (kulia) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Wilbert Chuma(kushoto) na (kulia) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe.Wilbert Chuma(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Sylvester Kainda akitoa neno katika makabidhiano hayo.



Baadhi ya viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo.


(Picha na Innocent Kansha) 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni