Na Innocent Kansha- Mahakama
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya amemshukuru mtangulizi wake Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Mhe. Wilbert Chuma kwa nasaa nzuri alizompatia
ambazo zitamsaidia kumjenga akiwa anatekeleza jukumu la kuhudumia nafasi ya
Msajili Mkuu na kuomba apewe ushirikiano kutoka kwa viongozi na watumishi wote
wa Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza
katika hafla ya kukabidhiwa Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe
18 Aprili, 2024 jijini Dar es salaam, Mhe Nkya amesema umuhimu na majukumu ya
ofisi ya Msajili Mkuu ni kuratibu na kuongoza shughuli zote za uendeshaji wa mashauri
kwani ndiyo jukumu mama la Taasisi.
“Niahidi
nitatekeleza majukumu yangu ya Msajili Mkuu kulingana na kiapo changu nilichoapa
mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo
tarehe 4 Aprili, 2024, lakini vilevile kwa kutumia uwezo alionijalia Mwenyezi
Mungu kadri nitavyoweza nitajitahidi kutumia maarifa yangu na weledi wangu na kushirikiana
na viongozi wengine wa Mahakama kuhakikisha Ofisi ya Msajili Mkuu inatekeleza
majukumu yake ipasavyokwa,” amesema Mhe. Nkya
Mhe.
Nkya alimshukuru mtangulizi wake Jaji Chuma kwa jitihada kubwa alizozifanya
kwani katika kipindi chake cha kuhudumu kama Msajili Mkuu mambo mengi sana
yamefanyika na pia kuna mambo mengi sana ambayo yataendelea kufanyika ambayo ni
takribani mambo 43 yaliyowasilishwa kwenye ripoti ya makabidhiano.
“Wakati
Jaji Chuma anatoa hotuba yake nilichukua tu mambo nane kumbe alitaja haraka
haraka lakini mzigo niliokuwa nao mbele yangu kwa kweli ni mzigo mkubwa kwa
hiyo nitaomba ushirikiano katika kutimiza majukumu ya Ofisi ya Msajili Mkuu,”
ameongeza Mhe. Nkya.
Mhe.
Nkya ameishukuru Tume ya Mahakama ya Tanzania inayoongozwa na Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kupendekeza jina lake kwa Mhe. Rais ili
ateuliwe kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Naye,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya
Mahakama amemshukuru Jaji Chuma kwa kutenga muda na kupangua ratiba zake kwa
ajili ya kuja kushiriki hafla hiyo muhimu ya makabidhiano ya Ofisi ya Msajili
Mkuu wa Mahakama.
“Napenda
kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa ushirikiano wa hali ya juu kwani wakati
naapishwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama tarehe 21 Agosti 2021 ulinipokea na
kunisaidia kujua shughuli za Mahakama kwa haraka zaidi,”ameongeza Prof. Ole
Gabriel.
Mtendaji
Mkuu amesema Jaji Chuma alitoa ushirikiano wa kipekee katika eneo la kuimarisha
mahusiano kati ya watumishi wa kimahakama na wele wasio wa kimahakama ‘Judicial
Officers & Non-Judicial Officers’, hilo lilikuwa jambo kubwa lililomsaidia
Mtendaji Mkuu kutekeleza majukumu yake kwa urahisi zaidi.
“Tayari
tumeshateta na Msajili Mkuu mpya ili tuendeleze morali hiyo kwani ni jambo ambalo
ni la msingi sana katika utendaji wa Taasisi ya Mahakama inayotoa huduma ya
haki kwa wananchi,” ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Aidha,
Prof. Ole Gabriel amemuhakikishia Msajili Mkuu Mpya kuendelea kumpa ushirikiano
wa kutosha kama ambavyo alikuwa akifanya kwa mtangulizi wake, Ofisi ya Mtendaji
Mkuu ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama itakupa ushirikiano
wa kutosha kutenda kazi zako za kila siku kwani sisi sote tunajenga nyumba moja
na hatuna haja ya kugombania fito.
“Nichukue nafasi hii kipekee nimshukuru Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha Mhe. Sylvester Kainda aliyekaimu shughuli za ofisi ya Msajili Mkuu kwa kipindi chote hicho alinipa ushirikiano wa hali ya juu na kutenda kazi za Mahakama kama ilivyokusudiwa,” amesema Mtendaji Mkuu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Wilbert Chuma (katikati aliyekaa katikati) akizungumza na watanzania kupitia vyombo vya habari wakati wa hafla ya kukabidhi Ofisi ya Msajili Mkuu jijini Dar es salaama.
(Picha na Innocent Kansha- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni