Alhamisi, 18 Aprili 2024

MAJAJI WATEMBELEA MWISHO WA RELI KIGOMA, MAKUMBUSHO YA DKT. LIVINGSTONE

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar ambao wapo Kigoma kuhudhuria Kikao Kazi kujadili sheria za kazi leo tarehe 18 Aprili, 2024 wametembelea maeneo kadhaa ya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Kumbukumbu ya Dkt. David Livingstone iliyopo katika mji wa Ujiji.

Maeneo mengi waliyotembelea Majaji hao ni Bandari ya Kigoma na eneo inapoishia reli ya kati, maarufu kama Mwisho wa Reli.

Msafara wa Majaji hao ulioongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ulianza majira ya saa 10.00 jioni kwa kutembelea Bandari ya Kigoma na kupokelewa na Nahodha wa Meri ya Liemba, Benjamin Mnyinyi.

Majaji wengine ni waliokuwepo kwenye msafara huo ni Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, Mhe. Thadeo Mwenempazi, Mhe. Biswalo Mganga, Mhe. Messe Chaba, Mhe. James Karayemaha, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika na Mhe. Aziza Idd Suwedi kutoka Mahakama Kuu Zanzibar.

Viongozi wengine wa Mahakama waliokuwepo ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Divisheni, Bi. Mary Shirima, Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Bw. Jumanne Muna, Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Geita, Mhe. Fredrick Rutashobya.

Wakiwa bandarini hapo, Majaji hao walipata maelezo mafupi namna inavyofanya kazi na jinsi Meli ya Liemba ilivyosimama kufanya kazi mwaka 2018 ili kupisha matengenezo makubwa.

"Sasa hivi Meli hii pamoja na nyingine zinazofanya kazi katika Ziwa Tanganyika ambazo zinahitaji matengenezo zimeshaanza kutengenezwa baada ya kupata fedha kutoka serikalini," Nahodha Mnyinyi alisema.

Baada ya kupata maelezo hayo mafupi, Majaji hao walipitishwa katika baadhi ya maeneo ya Bandari na kujionea upakiaji na upakuaji wa mizigo unaofanywa na mashine mbalimbali na mabehewa kadhaa yanayoleta mizigo katika eneo hilo kupitia reli.

Baadaye, Majaji hao walielekea kwenye Kituo cha Reli Kigoma na kujionea eneo maarufu la Mwisho wa Reli’ kabla ya kwenda kwenye Makumbusho ya Dkt. Livingstone katika Mji wa Ujiji ukiopo umbali wa takribani kilomita 15 kutoka Kigoma mjini.

Baada ya kufika katika makumbusho hayo, Majaji hao walipokelewa na Mtembeza Watalii, Mzee Kassim Mbingo, maarufu kama German Iron, ambaye aliwatembeza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo sehemu maarufu iliyojengwa mnara kwa ajili ya kumbukumbu ya Dkt. Livingstone.

Mzee Mbingo alieleza kuwa mnara huo ambao umejengwa mwaka 1927 kwa kutumia mawe kutoka Yerico Yerusalemu upo katika eneo ambalo kulikuwepo na mwembe maarufu ambao Dkt. Livingstone alikuwa akiutumia kupumzika kwa ajili ya kutafakari mambo mbalimbali, ikiwemo biarasha haramu ya utumwa.

“Sehemu hii ndiyo ambayo Dkt. Livingstone alikuwa akikaa kutafakari mambo mbalimbali. Eneo hili pia ndiyo alilokutana na Henry Stanley Novemba 10, 1871 kwa mara ya kwanza hapa Ujiji kufuatia hofu ya Waingereza kuwa alikuwa amekufa,” alisema. 

Mzee Mbingo aliwaeleza Majaji kuwa mwembe huo uliishi mpaka miaka ya 1920. Lakini katika kipindi hicho mti huo ulikuwa umeanza kuonesha dalili za kudhoofika. 

Alieleza kuwa kutokana na umaarufu wa mti huo wa mwembe, Serikali ya kikoloni ya Mwingereza haikutaka upotee, ndipo ilipoamua kukata matawi manne ya mwembe na kuyapandikiza. 

“Hapa kuna miti miwili ya maembe iliyopandikizwa. Baada ya mti huu wa mwembe kufa kuliamuriwa kujengwe mnara ili uwakilishe mti huu wenye historia ya kipekee. Mnara huu ulijengwa mwaka 1927 chini ya Serikali ya Mwingereza,” Mzee wa Chuma cha Ujerumani alisema.

Alisema kuwa Stanley na Livingstone walikaa kwa pamoja kwa muda wa miezi mnne katika eneo la Ujiji na Kwihara Tabora. Stanley alimshawishi Livingstone arudi kwao Uingereza lakini Dkt. Livingstone alikataa.

Mzee wa ‘Chuma cha Ujerumani’ pia aliwapitisha Majaji hao katika maeneo mengine ya Makumbusho hayo ili kujionea na kujifunza historia mbalimbali za Mkoa wa Kigoma na Ziwa Tanganyika.

Dkt. Livingstone alizaliwa mwaka 1814 na anafahamika sana kutokana na jitihada zake za kupambana na biashara ya watumwa na safari za kati ya Afrika ya Kusini na Tanganyika hadi Kongo. Alifariki tarehe 1 Mei, 1873 huko Chitambo, Zambia. 

Watumishi wake wanne Susi, Chuma, Mumwaswere na Uchopere waliufanyia upasuaji mwili wake na kumtolea utumbo, maini na moyo na kuviweka katika sanduku la chuma na kulifukia chini ya mti wa Mvule. 

Pia waliupaka mwili wa Livingstone chumvi na viungo vingine ili usiharibike. Walianza safari yao kutoka Chitambo, Zambia mpaka Bagamoyo ambapo mwili wake ulipokelewa na Wamissionari. 

Wamissionari waliusafirisha kwenda Uingereza kupitia Zanzibar. Tarehe 15 Aprili, 1874 mwili wa Dkt. Livingstone ulizikwa katika makaburi ya Westminster Abbey.

Majaji pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na Nahodha wa Meli ya Liemba (mwenye fulana na rangi ya bluu), Benjamin Mnyinyi. Picha chini Nahodha Mnyinyi akiwaeleza Majaji hao jambo.





Majaji (juu na picha mbili chini) wakiwa katika maeneo ya bandari




Hii ndiyo reli inayotumika kusafirisha mizigo kwenye Bandari ya Kigoma.


Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni, Bi. Mary Shirima anasema hapa ndiyo mwisho wa reli. Picha chini inaonesha mwisho wa reli Kigoma.



Majaji na Viongozi wengine wa Mahakama (juu na chini) wakiwa katika mwamba unaoonesha mwisho wa reli katika kituo cha Kigoma.




Majaji na Viongozi wengine wa Mahakama (juu na chini) wakiwa katika kituo cha reli Kigoma.



Majaji na Viongozi wengine wa Mahakama wakiwasili katika Hifadhi ya Kumbukumbu ya Dkt. David Livingstone.


Mtembeza Watalii, Mzee Kassim Mbingo, maarufu kama German Iron akiwaonesha Majaji na Viongozi wengine wa Mahakama mnara uliojengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya Dkt. David Livingstone.



Mtembeza Watalii, Mzee Kassim Mbingo, maarufu kama German Iron akiwa katika picha ya pamoja na Majaji hao kwenye mnara huo. Picha chini inaonesha mnara wenye maandishi yanaoonesha lini Dkt. Livingstone alikutana na Stanley walikutana.





Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akiwaonesha Majaji wenzake mnara huo.


Majaji wakipata maelezo ya kumbukumbu mbalimbali za Dkt. Livingstone kutoka kwa mzee wa Chuma cha Ujerumani ndani ya hifadhi hiyo.



Mwamba huyu hapa


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na Jaji Dkt. Eliamani Laltaika wakiagana na German Iron.




Majaji na Viongozi wengine wa Mahakama wakiwa mbele ya jengo la hifadhi hiyo baada ya kujionea kumbukumbu mbalimbali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni