Ijumaa, 19 Aprili 2024

WANANCHI KIGOMA WAKUMBUSHWA FAIDA ZA KUFUNGA MIRATHI MAHAKAMANI

Na Aidan Robert, Mahakama Kuu-Kigoma

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa Kigoma juu ya kufunga mirathi mara baada ya kupewa amri ya Mahakama ya kukusanya mali za marehemu na kuzigawa kwa warithi halali.

Akizungumza na wananchi waliofika kupata huduma mbalimbali katika Mahakama hiyo jana tarehe 18 Aprili, 2024 wakati akitoa elimu ya mashauri ya Mirathi, Mhe. Kagina ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Utoaji Elimu wa Kanda hiyo, alisema ni muhimu kuzingatia ufungaji wa mirathi mara tu baada ya   kukusanya mali za marehemu na kuzigawa kwa warithi halali wa marehemu.

“Elimu hii ituongezee uelewa juu kesi za Mirathi zinapofunguliwa mahakamani n ani muhimu mfuatilie vipindi vya elimu ya Sheria kila siku ya Jumatano kabla ya kuanza mashauri na kupitia Redio Joy Kigoma kila mwanzo na mwisho wa mwezi,” alisema Mhe. Kagina.

Akizungumzia kuhusu uhalali wa Watoto kumiliki mali za wazazi, Mhe. Kagina alieleza kuwa Watoto hupata uhalali wa kumiliki mali za wazazi wao mara tu baada ya kifo cha wazazi wao, kwani wazazi wakiwa hai mali zao haziwezi kumilikiwa na watoto wao kama zao. Hivyo, amewataka wananchi hao kuandika wosia ambao hutumika kisheria kuamua mali za marehemu kugawiwa na kumilikiwa na warithi alioona kuwa wanafaa kisheria, ambapo amesema kuwa, hatua hiyo huipa wepesi Mahakama na kwa upande wa familia kutokuwa na migogoro kwa kuwa marehemu mwenyewe ameacha amegawa mali zake kadri apendavyo. 

Bw. Ramadhani Barenya, Mkazi wa Mwandiga mkoani Kigoma, alisema pamoja na mirathi kuwa changamoto katika jamii, anaipongeza Mahakama kwa utaratibu wa kutoa elimu kwakuwa jamii kubwa haifahamu utaratibu wa Mirathi na kutokujua kunaleta migogoro mingi ya familia na isiyoisha hasa kwenye familia ambayo imekosa uelewa wa utaratibu wa kufunga Mirathi mahakamani.

 “Ni muhimu Mahakama iendelee kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwani ni muhimu katika mustakabali wa familia nyingi hapa kwetu Kigoma,” alisema Bw. Barenya.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kagina amewakumbusha wananchi kuhusu uandaaji wa wosia huku akiwatoa wasiwasi wa kuwa wosia ni unajichulia kifo bali ni hatua muhimu inayoondoa migogoro.

Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma hutoa elimu ya Sheria mara moja kwa wiki katika eneo maalum la wananchi kusubiria kuanza kwa mashauri mahakamani lengo likiwa ni kuwapa uelewa kuhusu taratibu mbalimbali za Kimahakama.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina akifafanua jambo wakati akitoa elimu ya kesi za Mirathi kwa wananchi waliofika kupata huduma katika Mahakama hiyo jana tarehe 18 Aprili, 2024.

Bw. Abdul Ngendanyi akisikiliza kwa makini majibu ya swali kuhusu ‘ukomo wa kukata rufaa kwa kesi ya Mirathi kwa mtu ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mahakama’ wakati Mhe. Kagina alipokuwa akijibu

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakaama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina akitoa ufafanuzi wa hoja aliyoulizwa na mwananchi ambaye amesimama na hakupenda jina lake litajwe mara baada ya kupewa nafasi ya kuuliza.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mhakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina akiwa pamoja na wananchi waliofika Mahakama hapo kupata huduma na kunufaika na elimu hiyo.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni