Jumatatu, 15 Desemba 2025

WITO MUHIMU WA AMIDI MAHAKAMA KUU TANZANIA KWA VIONGOZI WA MAHAKAMA, SERIKALI

  • Ashiriki maadhimisho jubilee miaka 20 Kanda ya Iringa, ahimiza uwajibikaji
  • Asema kuanzishwa Mahakama Kuu Iringa kumesogeza huduma za haki kwa umma

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa

Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ametoa wito kwa Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa kujituma, kuzingatia misingi ya maadili na kutumia teknolojia kwa ufanisi.

Mhe. Aboud ametoa wito huo leo tarehe 15 Desemba, 2025 kwenye maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali na wananchi lukuki wa Mkoa wa Iringa.

Kadhalika, Kaimu Jaji Kiongozi amewasihi Wadau wote katika mnyororo wa utoaji haki na wananchi kwa ujumla, kushirikiana na Mahakama kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuendelea kuwa sehemu ya uboreshai wa utoaji haki kwa kutoa mrejesho wa wazi.

Kwa upande wa Serikali, Mhe. Aboud amewasihi Viongozi katika ngazi mbalimbali kuhamasisha wananchi kutumia vyombo vya haki badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Akizunguzia maadhimisho hayo, Amidi wa Mahakama Kuu ameeleza kuwa hatua hiyo ni kumbukumbu muhimu katika historia ya utoaji haki nchini, ni safari iliyojaa juhudi, changamoto na mafanikio ambayo kwa pamoja wameyaona na kuyaishi.

‘Mafanikio na changamoto tulizokutana nazo iwe ni fursa kwetu ya kubuni na kuweka mikakati thabiti katika kutekeleza wajibu wetu wa kikatiba wa utoaji haki kwa umma wa Watanzania…

“Ni wazi kuwa, safari ya utoaji wa huduma za haki kwa umma bado inaendelea, pamoja na mazingatio ya Katiba, Sheria na Kanuni katika utekelezaji wetu wa majukumu ya kila siku, tuendelee kuishi katika viapo vyetu vya kazi pamoja na salamu yetu ya Mahakama ambayo inasisitiza katika uadilifu, weledi na uwajibikaji,’ Mhe. Aboud amesema.

Amewapongeza na kuwashukuru watumishi wa ngazi zote wa Mahakama waliopitia Kanda hiyo tangu kuanzishwa kwake kwa jitihada na mchango wao katika kuijenga taswira nzuri ya Mahakama ya Tanzania.

Kaimu Jaji Kiongozi ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ilikuwa ni moja ya hatua muhimu katika kusogeza huduma za haki kwa umma wa Watanzania.

Ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Kanda hiyo, kulikuwepo na Mahakama Kuu Kanda ya Songea iliyoanzishwa mwaka 1992 na kuanzia mwaka hadi 1999, Kanda ya Songea ilijumuisha na kutoa huduma kupitia Mahakama zote za Mkoa wa Iringa.

‘Ilipofika mwaka 2000, Mahakama zote za Mkoa wa Iringa zilienguliwa kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Songea na kuwekwa chini ya Kanda ya Mbeya kwa tangazo la Serikali Na. 162/2000,’ amesema.

Mhe. Aboud amebainisha kuwa juhudi za dhati zilifanyika kufuatia changamoto walizokuwa wanapitia wananchi kutoka Mkoa wa Iringa waliokuwa wakitafuta haki zao mahakamani, ikiwemo kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya Mahakama sambamba na matumizi ya muda na gharama.

Ameeleza kuwa Serikali ilitoa majengo yaliyokuwa yakitumika kama kiwanda cha kuchakata Almasi (TUNCUT) Iringa, ambayo yalikarabatiwa na kuwa majengo ya kutolea huduma za Mahakama kwa ngazi tofauti, kwa maana ya Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya.

Majengo hayo yalizinduliwa tarehe 22 Novemba, 2005 na Rais wa Awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa. Shughuli za Mahakama Kuu Kanda ya Iringa zilianza rasmi mnamo mwaka 2006 baada ya Jaji Mfawidhi kutoka Kanda ya Dodoma kuhamishiwa Iringa pamoja na watumishi kutoka maeneo mbalimbali ya Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru ameeleza kuwa Kanda hiyo ilianzishwa mwaka 2005, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Mahakama ya Tanzania wa kusogeza huduma karibu na wananchi ili kupunguza umbali na gharama za kufuata haki katika Mikoa ya Iringa na Njombe.

Amesema kuwa wakati inaanzishwa, kulikuwepo na Jaji mmoja na idadi ndogo ya watumishi wasiozidi 30 katika ngazi mbalimbali, jengo kuu lilikuwa dogo, lenye uwezo mdogo wa kuhudumia idadi kubwa ya wananchi, mashauri yaliyofunguliwa kwa mwaka yalikuwa wastani wa mashauri 250 hadi 300 na hapakuwa na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA] katika uendeshaji wa mashauri.

“Katika kipindi cha miaka 20 tumepiga hatua kubwa na zinazooneka kwa uwazi katika maeneo makuu mawili; miundombinu na huduma kwa wananchi na usikilizaji wa mashauri na maboresho ya mifumo ya utoaji haki,” Mhe. Ndunguru amesema.

Kuhusu miundombinu, Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa katika miaka 20 wamejenga msingi imara wa miundombinu ya kimahakama na kufanya uboreshaji ili kusogeza huduma karibu na wananchi, pamoja na kufanya mazingira ya kazi kuwa rafiki kwa Wadau wa Mahakama.

Kupitia uboreshaji huo, jumla ya majengo 20 yamejengwa kwa kutumia fedha za ndani na ufadhili wa Benki ya Dunia na kwa kushirikiana na Wadau wa Mahakama Kanda ya Iringa, ikiwemo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Njombe ambacho ujenzi wake upo mbioni kukamilika.

Kuhusu TEHAMA, Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa katika miaka 20, wameingia katika zama za matumizi ya TEHAMA kwani wamewezesha watumishi kumiliki mfumo wa usimamizi wa mashauri (JoT-eCMS) katika uendeshaji wa mashauri, mfumo wa usikilizaji mashauri kwa njia ya mtandao, ambao unasaidia mdau kusikiliza shauri hata akiwa ndani ya nchi ama nje ya nchi, mfumo tumizi wa Mahakama za Mwanzo na mifumo mingine mingi.

Aidha, Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa kutokana na kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, kasi ya umalizaji wa mashauri imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na hii ni kwa sababu huduma zinapatikakana karibu, watuishi wa Mahakama wanatoa huduma wakiwa hapa hapa Iringa kwa kutumia nguvu kazi iliyopo.

“Hii imethibitishwa na viwango tofauti tofauti vya mashauri yaliyokuwa yakifunguliwa na kumalizika tangu 2006 hadi Octoba, 2025. Kwa mfano kwa mwaka, 2006 mashauri yaliyofunguliwa Mahakama Kuu yalikuwa 37, yaliyoaamriwa yalikuwa saba. Kwa mwaka, 2005 Januari hadi octoba, 2025 yalifunguliwa 551 na yaliyoamriwa yalikuwa ni 454. Kwa mwaka, 2006 hadi 0ktoba, 2025 mashauri yalitofunguliwa Mahakama Kuu Kanda yalikuwa 4,953 na kati ya hayo mashauri 4,289 yamemalizika,” amesema.

Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud [juu na chini] akizungumza kwenye maadhimisho ya jubilei ya miaka 20 tangu kuanzisha kwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku, akitambulisha wageni mbalimbali kwenye maadhimisho hayo.


Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, akiratibu matukio mbalimbali wakati wa maadhimisho hayo.


Meza Kuu inayoongzwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Mstaafu, waliohudhuria maadhimisho hayo. Picha chini ni Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama Kuu na Naibu Wasajili.


Meza Kuu inayoongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini na Mila wa Mkoa wa Iringa. Picha chini ni Watendaji na Wakuu wa Vitengo kutoka Mahakama mbalimbali na Makao Makuu.


Meza Kuu inayoongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili na Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Iringa.

Meza Kuu inayoongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Iringa [juu na chini].


Meza Kuu inayoongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama [juu na chini].

Meza Kuu inayoongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na Mawakili wa Serikali [juu] na Mawakili wa Kujitegemea [chini].


Meza Kuu inayoongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama [juu na chini].



 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni