- Yaadhimisha Jubilei ya miaka 20 tangu kuanzishwa
- Ndiyo Kanda ya kwanza kuweka historia hiyo ya Mahakama Tanzania
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Iringa
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Iringa, leo tarehe 15 Desemba, 2025 imeweka historia ya kipekee baada
ya kuadhimisha jubilei ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005.
Tukio hilo linaifanya
Mahakama Kuu Iringa kuwa ya kwanza kati ya Kanda 20 za Mahakama Kuu Tanzania
kuadhimisha jubilei tangu zianzishwe. Hatua hiyo imepongezwa na Viongozi wengi
waliohudhuria maadhimisho hayo, akiwemo Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud.
Kanda nyingine za
Mahakama Kuu zilizopo kwa sasa ni Dar-es-Salaam, Morogoro, Temeke,Tanga, Moshi,
Arusha, Manyara, Mwanza, Bukoba, Geita, Shinyanga, Dodoma, Tabora, Sumbawanga,
Kigoma, Mbeya, Songea, Mtwara na Musoma.
Maadhimisho hayo
yaliyofanyika kwenye viunga vya Mahakama hiyo, maarufu kama 'Uwanja wa Haki'
yamehudhuriwa na Mhe. Aboud na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda
mbalimbali.
Viongozi wengine wa
Mahakama waliohudhuria maadhimisho hayo ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
kwa niaba ya Msajili Mkuu na Mtendaji wa Mahakama Kuu, kwa niaba ya Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Majaji wastaafu, Naibu Wasajili, Watendaji wa
Mahakama, Mahakimu na watumushi wengine wengi wa Mahakama Kanda ya Iringa.
Kwa upande wa Serikali
alikuwepo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakuu wa
Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa na Mawakili wa Serikali. Wengine
waliohudhuria maadhimisho hayo ni Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Dini na
wananchi kwa ujumla.
Viongozi mbalimbali
walipata nafasi ya kutoa salamu kwenye maadhimisho hayo. Katika salamu zake, Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewapongeza watumishi wa Mahakama kwa
kuadhimisha miaka 20 tangua kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.
Amesema kuwa maadhimisho
hayo yanawakumbusha umuhimu na wajibu wa kuzisimamia, kuzipigania na kuhakikisha
haki za wananchi zinatolewa wakati wote.
“Sisi wote tunafahamu,
umoja, mshikamano, amani na maendeleo yetu ni matunda ya haki. Kwa msingi huo,
tunaendelea kuwajibika kama wananchi, viongozi na watumishi ndani ya Mkoa wa
Iringa kuhakikisha Taasisi hii muhimu iliyopewa mamlaka ya kikatiba kutafsi na
kutoa haki kwa wananchi tunailinda, tunaitetea na kuiwezesha kufanya wajibu huu
wa msingi ili haki iweze kutamalaki katika jamii yetu,” amesema.
Mkuu wa Mkoa ametumia
fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuipa ushirikiano Mahakama pale kesi zinazopoanza
ili wanapohitajika mahakamani kutoa ushahidi wajitokeze ili kurahisisha
mchakato wa haki .
Naye Rais wa Chama cha
Mawakili Tanganyika, Mkoa wa Iringa, Wakili Msomi Moses Ambindwile, amesema kuwa Mahakama Kuu
Kanda ya Iringa imeandika na inaendelea kuandika historia ya kipekee katika
utoaji haki na ujenzi wa uongozi wa Mahakama ya Tanzania.
Wakili Msomi Ambindwile
amebainisha pia kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imekuwa mithiri ya Chuo Kikuu
cha Uongozi nchini kwa kutoa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye,
Mhe. Rehema Kerefu, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.
Kwa mujibu wa Wakili
Msomi, wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dunstan Ndunguru, Mhe.
David Ngunyale, Mhe. Ruth Massam, Mhe. Isaya Arufani, Mhe. Augustine Rwizile,
Mhe. Gladys Barthy, Mhe. Cyprian Mkeha, Mhe. Martha Mpaze na Mhe. Victoria
Nongwa.
“Lakini pia imewahi kutoa
Jaji Viongozi wawili, Mhe. Fakih Jundu na Mhe. Dkt. Feleshi na Wanasheria Wakuu
wa Serikali wawili, Mhe. Fredrick Welema na Mhe. Dkt. Feleshi, ambao wamewahi
kufanya kazi hapa Kanda ya Iringa,” amesema.
Ameeleza kuwa wao kama
TLS wataendelea kusimama bega kwa bega na Mahakama kwa maslahi ya wananchi na
Taifa kwa ujumla.
Wakati wa maadhimisho
hayo kulifanyika uzinduzi wa Jarida la Mahakama Kanda ya Iringa linaloitwa,
"Uwanja wa Haki " ambao ulifanywa na Mhe. Aboud. Jarida hilo
limesheheni makala mbalimbali zinazoelezea historia ya Mahakama Kanda ya
Iringa, shughuli za usikilizaji wa mashauri na utendaji kwa ujumla na andiko la
kusisimua la chimbuko la Mahakama ya Mwanzo Kalenga iliyopo kwenye Makumbusho
ya Taifa ya Kalenga ya Chifu Mkwawa.
Burudani za ngoma, bendi na kwaya ya Mahakama Kanda ya Iringa zimepamba maadhimisho hayo. Kikundi cha Ngoma Kibate kinachocheza na Nyoka aina ya Chatu kimekonga nyoyo za wananchi waliokuwa wamefurika kwenye viunga hivyo vya Mahakama. Kulifanyika pia igizo la mfano wa namna Mahakama inavyofanya kazi wakati wa kuendesha mashauri.
Kabla ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuanzishwa mwaka 2005, shughuli za kimahakama katika Mkoa wa Iringa na Njombe zilikuwa zinafanyika katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Meza Kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud ikifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa maadhimisho ya jubilei ya miaka 20 tangu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuanzishwa mwaka 2005. Picha chini ikiimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni