- Yarejesha kwenye mzunguko wa fedha bilioni 11 za Kitanzania kila mwezi
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Divisheni ya Biashara, imefanikiwa kurejesha kwenye mzunguko wa fedha wastani
wa kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 11 kila mwezi kwa mwaka wa 2025.
Hayo yamebainishwa na Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, kwenye
hotuba iliyowasilishwa kwa niaba yake na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Iman Aboud, kwenye uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya
Biashara uliofanyika leo tarehe 12 Desemba, 2025 jijini Dar es Salaam.
‘Hizi fedha zinatokana na
mashauri ambayo uamuzi wake umekamilika hadi utekelezaji. Ninaposema Mahakama
ya Biashara ipo kwa ajili ya kuwezesha miamala ya kibiashara, itekelezwe kwa
ufanisi ninamaanisha hiyo. Taarifa za Mahakama hii zinathibitisha eneo la
ukuaji wa uchumi na ufanisi wa biashara nchini,’ Mhe. Dkt. Siyani ameeleza
kwenye hotuba yake.
Jaji Kiongozi ameeleza
kuwa urejeshaji wa kiasi kikibwa cha fedha hizo kwenye mzunguko wa fedha ni tafsiri
kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imechangia katika utekelezaji wa Dira ya
Taifa ya mwaka 2025-2050 inayolenga kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kuongeza
imani ya wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kwa
Mahakama ya Tanzania.
Ameeleza kuwa anafahamu pia kuwa kuanzia
katikati ya mwezi Octoba hadi Novemba, 2025, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara
ilikuwa na vikao maalum vya usikilizaji mashauri, ambapo jumla ya mashauri ya
kibishara yaliyoamuliwa ni 96 yenye
thamani ya Shilingi za Kitanzania 65,964,979,029/04, Dola za Kimarekani
10,195,592,01 na Euro 172,892.
‘Taarifa nilizozipokea kutoka kwa Jaji Mfawidhi ni kwamba mashauri
haya yalisikilizwa kama yalivyopangwa kwa
zaidi ya asilimia 90,’ sehemu ya hotuba ya Jaji Kiongozi inaeleza.
Ameeleza kuwa Mahakama
Kuu Divisheni ya Biashara imeamua kutoa mwongozo huo kwa kutambua kuwa mashauri
ya kibiashara yanapaswa kusikilizwa na kuamriwa mapema ipasavyo na kuzingatia
weledi unaoakisi kwa usahihi ujuzi kwenye eneo husika la mgogoro na kwa kutambua
kuwa si wengi walio na maarifa sahihi kwenye ushughulikiaji wa mashauri ya kibiashara.
Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi,
licha ya mwongozo huo kushughulika na mashauri ya kibiashara, ni imani yake kuwa
utanufaisha Wadau wengi, hata kwenye mashauri mengine ya madai kwa kuwa mashauri
ya kibiashara ni mashauri ya madai pia.
‘Kwa sababu hiyo, taratibu
za uendeshaji wa mashauri ya kibiashara zinashabihiana na taratibu za uendeshaji
wa mashauri mengine ya madai, ingawa kuna tofauti za hapa na pale,’ Mhe. Dkt.
Siyani amesema.
Kwa upande mwingine, Jaji
Kiongozi amesema kuwa Mwongozo huo utakuwa rejea nzuri kwa vijana waliopo
kwenye Shule ya Sheria kwa Vitendo na Vyuo Vikuu kwa mambo mbalimbali wanayojifunza.
Kadhalika, Wahadhiri na Watafiti mbalimbali wa ndani na nje ya nchi pia watanufaika
na maarifa yaliyomo ndani ya Mwongozo huo.
Akizungumzia chimbuko la
Mwongozo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian
Mkeha, ameeleza kuwa pamoja na uboreshaji ambao umefanyika kwenye maeneo
mbalimbali, nyenzo na vitendea kazi vilivyopo kwa sasa katika eneo la haki
madai haviwezeshi Maofisa Mahakama, Mawakili na Wadau wenye mashauri mahakamani
hapo kufanya mambo kwa wepesi.
Amesema kuwa hali hiyo
inatokana na upekee wa migogoro ya kibiashara ambao utatuzi wake wakati
mwingine unaweza kuhitaji maarifa ya ziada yasiyopatikana kwenye vitendea kazi
vilivyopo. Mhe. Mkeha ametaja sababu nyingine ni mabadiliko ya namna njia za ufanyaji
biashara zinavyobadilika kwa kasi kutokana na kukua kwa teknolojia ulimwenguni.
Hivyo, Mhe. Mkeha
ameishukuru Benki Kuu ya Tanzania, hususan Gavana wa Benki Kuu Emmanuel Tutuba
kwa kufanikisha kwa kiasi kikubwa uandishi, uhariri na uzalishaji wan akala 100
za Mwongozo huo.
Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii,
uaminifu na kasi itakayowezesha kurudi kwa fedha zinazoshikiliwa, kwa sababu ya
uwepo wa mashauri katika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, kwenye mzunguko wa
uchumi.
‘Tutafanya hivyo kwa
kuharakisha ukazaji wa tuzo tunazozitoa, eneo ambalo Benki imeliwekea pia mkazo
katika fedha ambazo imezitoa kwa Divisheni ya Biashara katika mwaka huu wa
fedha wa 2025/2026. Kwa kufanya hivyo, Mahakama itakuwa imechangia ukuaji wa uchumi
na kuwa kivutio cha uwekezaji nchini,’ amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto [IJA] na Jaji wa Mahakama ya Rufani
Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, akiwasilisha neno lake wakati wa uzinduzi
huo, amepongeza ushirikiano kati ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara na Benki
Kuu, ambao umefanikisha kupatikana kwa Mwongozo huo.
Ameeleza kuwa wao kama
Chuo, ambao kazi yao ni kufundisha na kuwajengea weledi na uwezo Majaji na
Majaji katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, watautumia Mwongozo huo
kama nyenzo ya kufundishia na ameahidi kuenedeleza ushirikiano uliopo kati ya
IJA na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwenye eneo la mafunzo.
Uzinduzi wa Mwongozo huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama, Wahadhiri wa Vyuo, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea, Wadau na watumishi wa Divisheni ya Biashara.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji na Viongozi Waandamizi wa Mahakama Kuu Divisnehi ya Biashara. Picha chini ni wajumbe wa kamati iliyofanikisha utayarishaji wa Mwongozo huo.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama kutoka Makao Makuu Dodoma. Picha chini Wadau waliohudhuria hafla hiyo.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama Kuu. Picha chini ni Mawakili na Wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara [juu na chini] waliohudhuria uzinduzi huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni