Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Divisheni Biashara, leo tarehe 12 Desemba, 2025 imezindua Mwongozo wa
Uendeshaji wa Mashauri ya Biashara utakaowawezesha Maofisa Mahakama, Mawakili
na Wadau mbalimbali kushughulikia mashauri ya kibiashara kwa ufanisi, weledi na
mapema ipasavyo.
Uzinduzi wa Mwongozo huo
umefanywa na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud, kwa niaba ya
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani,
ambaye alialikwa kuwa Mgeni Rasmi.
Hafla hiyo imehudhuriwa
na Viongozi mbalimbali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu,
Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Naibu Wasajili na
Watendaji wa Mahakama, Wahadhiri wa Vyuo, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea,
Wadau na watumishi wa Divisheni ya Biashara.
Alikuwepo pia mwakilishi
wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Mosy Lukuvi, ambaye ameeleza kuwa Banki
Kuu ni Mdau muhimu wa Mahakama kutokana na nafasi yake katika usimamizi wa
uchumi na sekta ya benki na Taasisi za fedha.
Amesema kuwa wanatambua kwamba
sekta hizo mbili ndizo zinazochangia uwepo wa mashauri mengi katika Mahakama
Kuu Divisheni ya Biashara, hivyo Benki Kuu ni nguzo muhimu ya kuhakikisha
ufanisi wa uendeshaji wa mashauri ya biashara unaongezeka.
Kwa mujibu wa Bw. Lukuvi,
hatua hiyo ya Benki Kuu inasaidia kuleta ustawi wa biashara nchini na kukuza
uchumi na pia kuweza kuvutia uwekezaji kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya
nchi.
‘Nchi yoyote ambayo haina
Mahakama yenye ufanisi haiwezi kuwa kimbilio au kivutio cha biashara. Kwa hiyo,
tunaamini jitihada zote zinazofanyika, hususan uzinduzi wa Mwongozo huu zinalenga
kuzingatia masharti ya kikatiba wakati wa usikilizaji wa mashauri,’ amesema.
Wadau mbalimbali pia
walipata nafasi ya kuuzungumzia Mwongozo huo, wakiwemo Mawakili wa Serikali na
Kujitegemea, ambao katika nyakati tofauti, wameipongeza Mahakama kwa hatua hiyo
nzuri kwani unawasaidia namna ya kufikia haki kwenye mashauri ya kibiashara.
‘Mwongozo huu unatusaidia
kujua ukienda Mahakama ya Biashara unatazamia nini na nini kinatolewa kule.
Huwezi kukimbia kutafuta haki kama hujui taratibu. Kwa hiyo, hiki ni kitu
kizuri sana na tukimbizane ili kuhakikisha kwamba tunakitumia ipasavyo,’ Wakili
Msomi Alex Mgonmgolwa, ambaye ni miongoni mwa Wadau hao, amesema.
Akizungumzia maudhui,
Mhadhiri anayefundisha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Idd
Mandi, ameipongeza Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa kuamua kuandaa
Mwongozo wa namna hiyo.
Amesema kuwa Mwongozo huo siyo tu utawasaidia Majaji na Mawakili wanaoshughulika na mashauri ya kibiashara katika Mahakama hiyo, bali pia Wanafunzi, hasa kwenye Shule ya Sheria kwa Vitendo, ili kuwa na uelewa mpana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni