Ijumaa, 12 Desemba 2025

MWONGOZO WA UENDESHAJI MASHAURI YA BIASHARA WAZINDULIWA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni Biashara, leo tarehe 12 Desemba, 2025 imezindua Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Biashara utakaowawezesha Maofisa Mahakama, Mawakili na Wadau mbalimbali kushughulikia mashauri ya kibiashara kwa ufanisi, weledi na mapema ipasavyo.

Uzinduzi wa Mwongozo huo umefanywa na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud, kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ambaye alialikwa kuwa Mgeni Rasmi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama, Wahadhiri wa Vyuo, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea, Wadau na watumishi wa Divisheni ya Biashara.

Alikuwepo pia mwakilishi wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Mosy Lukuvi, ambaye ameeleza kuwa Banki Kuu ni Mdau muhimu wa Mahakama kutokana na nafasi yake katika usimamizi wa uchumi na sekta ya benki na Taasisi za fedha.

Amesema kuwa wanatambua kwamba sekta hizo mbili ndizo zinazochangia uwepo wa mashauri mengi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, hivyo Benki Kuu ni nguzo muhimu ya kuhakikisha ufanisi wa uendeshaji wa mashauri ya biashara unaongezeka.

Kwa mujibu wa Bw. Lukuvi, hatua hiyo ya Benki Kuu inasaidia kuleta ustawi wa biashara nchini na kukuza uchumi na pia kuweza kuvutia uwekezaji kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

‘Nchi yoyote ambayo haina Mahakama yenye ufanisi haiwezi kuwa kimbilio au kivutio cha biashara. Kwa hiyo, tunaamini jitihada zote zinazofanyika, hususan uzinduzi wa Mwongozo huu zinalenga kuzingatia masharti ya kikatiba wakati wa usikilizaji wa mashauri,’ amesema.

Wadau mbalimbali pia walipata nafasi ya kuuzungumzia Mwongozo huo, wakiwemo Mawakili wa Serikali na Kujitegemea, ambao katika nyakati tofauti, wameipongeza Mahakama kwa hatua hiyo nzuri kwani unawasaidia namna ya kufikia haki kwenye mashauri ya kibiashara.

‘Mwongozo huu unatusaidia kujua ukienda Mahakama ya Biashara unatazamia nini na nini kinatolewa kule. Huwezi kukimbia kutafuta haki kama hujui taratibu. Kwa hiyo, hiki ni kitu kizuri sana na tukimbizane ili kuhakikisha kwamba tunakitumia ipasavyo,’ Wakili Msomi Alex Mgonmgolwa, ambaye ni miongoni mwa Wadau hao, amesema.

Akizungumzia maudhui, Mhadhiri anayefundisha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Idd Mandi, ameipongeza Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa kuamua kuandaa Mwongozo wa namna hiyo.

Amesema kuwa Mwongozo huo siyo tu utawasaidia Majaji na Mawakili wanaoshughulika na mashauri ya kibiashara katika Mahakama hiyo, bali pia Wanafunzi, hasa kwenye Shule ya Sheria kwa Vitendo, ili kuwa na uelewa mpana.


Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud [kushoto] akionesha Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Biashara baada ya uzinduzi. Picha chini ni Viongozi wa Meza Kuu wakionesha Mwongpozo huo.


Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Iman Aboud akizungunza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo huo.

Mhadhiri anayefundisha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Idd Mambi akieleza kwa ufupi maudhui ya Mwongozo huo. Picha chini ni Mwakilishi wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Mosy Lukuvi, akizungumza kwenye hafla hiyo.


Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu [juu na chini] ikiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mwongozo huo.


Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Wadau wakiwa kwenye uzinduzi huo [juu na picha mbili chini].



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni