Jumanne, 21 Februari 2017

KESI YA MBOWE YAANZA KUSIKILIZWA LEO MAHAKAMA KUU.


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Freeman  Mbowe(kushoto) akiwa Mahakama  Kuu  kwa ajili ya  kupeleka  ombi  la zuio la muda  la kukamatwa na polisi. Katika kesi hiyo jopo la Majaji  wanaoisikiliza wametoa  uamuzi  wa kutokamatwa kwa Mwenyekiti huyo kwa muda,  Aidha; Mahakama Kuu hiyo imemtaka Mwenyekiti huyo kurejea Mahakamani hapo Februari  23, mwaka huu.
Baadhi ya waandishi wakisubiri taarifa za ombi la zuio la kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman  Mbowe.
Wakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Peter Kibatala akitoa maelezi kuhusu ombi hilo, kwa waandishi wa habari. 

Jumatatu, 20 Februari 2017

MAJENGO 70 YA MAHAKAMA KUJENGWA NA KUKARABATIWANa Lydia Churi-Mahakama
Mahakama ya Tanzania inatarajia kukamilisha miradi ya ukarabati na ujenzi wa majengo 70 ya Mahakama katika kipindi cha miaka miwili ili kusogeza karibu huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Ili kusogeza huduma hiyo kwa wananchi, majengo ya Mahakama kuu katika mikoa tisa yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili, Mahakama za Mikoa sita zitajengwa ndani ya miezi 6-12 wakati Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 zinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2017.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika hivi karibuni, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma alisema Mahakama kwa kushirikiana na Wakala wa Majengo (TBA), Chuo Kikuu cha Ardhi, Baraza la Ujenzi la Taifa, Benki ya Dunia na wadau wengine wanaendeleza na kukamilisha miradi ya ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa tisa nchini. 

Aliitaja mikoa ambayo majengo ya Mahakama Kuu yatafanyiwa ukarabati na mengine kujengwa ndani ya kipindi cha miezi 24 kuwa ni Mbeya, Kigoma, Mara, Tanga na Dar es salaam. Mikoa mingine ni Arusha, Morogoro, Mwanza na Dodoma.

Alisema nia ya Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa ili kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi.

“Tunapaswa kuwa na Mahakama Kuu 26 kwenye kila ngazi ya Mkoa, kwa sasa tunazo Mahakama Kuu kwenye kanda 14 tu”, alisema Kaimu Jaji Mkuu.
Aidha, mikoa 12 isiyokuwa na Mahakama Kuu ni pamoja na Songwe, Katavi, Njombe, Lindi, Kigoma na Mara. Mikoa mingine ni Singida, Morogoro, Pwani, Simiyu, Geita na Manyara.  

Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa wakati huo huo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kukamilisha ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa sita ya Manyara, Geita, Simiyu, Njombe, Katavi na Lindi katika kipindi cha kati ya miezi 6 na mwaka mmoja.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma (kulia) akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kumalizika kwa Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mahakama vilivyoko Mtaa wa Chimara jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa Mahakama za Wilaya na zile za Mwanzo, Kaimu Jaji Mkuu alisema wanakusudia kujenga Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 ambazo zitakamilika ifikapo Desemba 2017.

Alisema hatua hii ya ujenzi wa Mahakama hizi si tu kwamba itasogeza karibu huduma za Mahakama kwa wananchi bali pia italeta mabadiliko makubwa ya miundombinu ya mahakama na kuweka historia ya upatikana wa miundombinu kwa wingi na kwa kifundi kifupi.    

Jumanne, 14 Februari 2017

JAJI FATUMA MASENGI ASTAAFU


Mheshimiwa Jaji Fatuma Masengi aliyestaafu rasmi jana. Mhe. Masengi alikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Mhe. Fatuma Masengi (wa nne kushoto) na Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama Kanda ya Arusha na Moshi mara baada ya Sherehe ya Kumuaga iliyofanyika jana Mahakama Kuu kanda ya Arusha.