Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma
Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dodoma imezindua hema maalum litakalokuwa linatumika kutoa huduma za haki kwenye mashauri ya familia, ikiwemo ndoa, mirathi na talaka katika ngazi ya Mahakama ya Mwanzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Dkt Juliana Masabo ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa hema hili-Hema
Haki-uliohudhuriwa na mamia ya Wananchi wa Dodoma na viunga vyake.
Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 1 Julai, 2025 katika eneo la
Mahakama ya Mwanzo ya zamani ya Dodoma mjini
iliyopo relini, Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Mhe. Dkt. Masabo alisema,
“ni jambo lisilopingika kuwa, migogoro ya kifamilia
imeongezeka kwa kasi, na imekuwa chanzo kikubwa cha maumivu ya kijamii.
‘..Kumekuwa na utitiri wa migogoro inayotokana na mizozo ya ndoa, talaka
zisizo na mwongozo wa kisheria, malezi ya watoto, hasa pale wazazi wanapokuwa
wametengana, usimamizi na ugawaji wa mali za marehemu (mirathi), pamoja na
mambo mengine mengi yanayokosa utatuzi na hivyo kuleta migogoro ya kifamilia na
kijamii,’alisema.
Alieleza kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha mateso kwa watu wengi na hivyo
kuhitaji mfumo rahisi, wa haraka, na wa haki na Haki Hema ni mojawapo ya majibu
ya changamoto hizo.
Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa takwimu za mashauri katika Mahakama za Mwanzo zinaonesha kuwa kwa kipindi
cha mwaka 2023 hadi Juni 2025, Mahakama tatu za Mwanzo zilizopo mjini Dodoma, yaani: Mahakama ya Mwanzo Dodoma Mjini (iliyopo katika Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki- maarufu IJC), Mahakama ya Mwanzo Makole na Mahakama ya Mwanzo Chamwino Mjini,
zilipokea na kusajili jumla ya mashauri 12,267.
Kati ya hayo, Mashauri 4,627 (sawa na asilimia 37.7) ni ya ndoa, talaka na
mirathi. Kwa Mahakama ya Mwanzo Makole pekee, mashauri ya familia (ndoa, talaka
na mirathi) yaliyopokelewa katika kipindi hicho ni 1,492,
sawa na asilimia 38.9 ya mashauri 3,838 yaliyopokelewa
na kusajiliwa katika mahakama hii.
Akitoa salam za pongezi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma Mjini, Mhe. Alhaji Jabir Shekimweri aliipongeza Mahakama kwa hatua nzuri
iliyoichukua ya kusogeza huduma hiyo ya Mahakama karibu na Wananchi.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Majaji kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Wadau mbalimbali wa haki, watumishi wa Mahakama, Viongozi wa Dini, wawakilishi wa serikali na wananchi wa Dodoma ambao walipokea hatua hiyo kwa furaha na matumaini makubwa katika kuboresha haki nchini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akizungumza wakati wa halfla ya uzinduzi wa Huduma ya Mahakama katika Haki Hema.
Mkuu wa Wilaya wa Dodoma, Mhe Jabiri Shekimweri akitoa salamu wakati wa hafla hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo-wa pili kutoka kulia-akikata utepe wakati wa halfla ya uzinduzi wa Huduma ya Mahakama katika Haki Hema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Dkt. Juliana Masabo akisaini kitabu ch wageni mara baada ya uzinduzi huo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi.
Baadhi ya Viongozi wa Mahakama waliohudhuria uzinduzi huo.
Mwananchi akisema neno la shukrani kwa niaba ya Wananchi
wenzake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Dkt. Juliana Masabo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wananchi wa
Dodoma kutoka sehemu mbalimbali wakati
wa hafla hiyo ya uzinduzi.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni