Alhamisi, 3 Julai 2025

JAJI MFAWIDHI KANDA IRINGA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI MKOANI NJOMBE

  • Atembelea Mradi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe 

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru ameanza ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Mkoa wa Njombe kwa kufanya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya za Njombe na Wanging’ombe.

Mbali na Mahakama hizo, Mhe. Ndunguru alifanya pia ziara ya ukaguzi katika Mahakama za Mwanzo Wilaya kuanzia tarehe 01 Julai, 2025.

Akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe.Ndunguru alipokea taarifa ya jumla ya Mkoa mzima juu ya uendeshaji wa mashauri pamoja na miundombinu ya   Mahakama ya Mkoa Njombe pamoja na  Mahakama zake za Mwanzo za Wilaya zilizopo katika Mkoa huo.

Akiwasilisha taarifa ya Mahakama katika Mkoa huo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama alidokeza kuhusu hali ya usikilizwaji wa mashauri kwa Mkoa mzima pamoja  na   utekelezaji wa Nguzo namba moja (1) katika Mpango Mkakati wa Mahakama utawala bora uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali.

Mhe. Chamshama alibainisha mafanikio mbalimbali  yaliyopatikana katika Mahakama hiyo kuwa, ni pamoja na   kufanya marekebisho ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Makambako Mjini ambalo lilikuwa halipo kwenye hali nzuri licha ya ufinyu wa bajeti.

Aidha, baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe.Ndunguru alijibu hoja mbalimbli zilizojitokeza kwenye taarifa hiyo huku akisisitiza kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kupandisha vielelezo na hati za mashtaka   kwenye mfumo wa usimamizi wa mashauri Mahakamani (e-CMS) hasa kwa mashauri yaliyokatiwa rufaa kwenda Mahakama ya juu.

Sanjari na hilo Mhe. Ndunguru alizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe ambapo alitoa  pongezi juu ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo.

Baada ya hapo Mhe,Ndunguru alienda kukagua jengo la Mahakama ya mwanzo Mdandu ambalo lipo chini ya Mahakama ya Wilaya Wangingombe ambalo kulikuwa na jengo la zamani la kihistoria lillilojengwa na wakoloni kwa shunghuli za kiMahakama

Mhe. Ndunguru alitembelea pia jengo la kale la Mahakama ya Mwanzo Mdandu lililojengwa na wakoloni na kujionea majalada ya zamani waliokuwa wanatumia machifu kuhamua mashauri pamoja na kuona makabati yaliyokuwa yanatunza majalada hayo.

Kadhalika Mhe.Ndunguru alifanya ukaguzi Mahakama ya Mwanzo Njombe Mjini ambapo alizungumza na watumishi na kusomewa taarifa fupi ya  Mahakama hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe.Bernazitha Maziku alisisitiza juu ya kusajiLi mashauri yote yanayoingia mahakamani ili kuweka sawa kumbukumbu pamoja na  kuhuhisha mashauri hayo kwa kila Hakimu na kuwa rafiki na mifumo inayosimamia haki kwa wananchi  kwani bila kufanya hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya haki.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo pamoja na alioambatana nao walifanya ukaguzi katika Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe ambayo  inaendelea kujengwa na sasa umefikia asilimia 90 ili ukamilike. Hata hivyo, Mhe. Ndunguru amemtaka Mkandarasi wa Mradi huo kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda aliomba kuongezewa.

Katika ziara hiyo Jaji Mfawidhi huyo ameambatana na  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi.Melea Mkogwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Njombe, Mhe. Liadi Chamshama pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (aliyeketi mbele) akisikiliza taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa kwake na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Njombe, Mhe. Liadi Chamshama (aliyeketi wa kwanza kulia kwa Jaji Mfawidhi). Wengine ni Viongozi walioambatana na Jaji Mfawidhi katika ziara hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (kushoto) akifuatilia taarifa ya Mashauri ya  Mahakama ya Wilaya Wangingombe iliyokuwa ikisomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. James Muhoni (aliyesimama). Walioketi wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, anayefuata ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya  Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru  akipanda mti wa mparachichi nje ya jengo la Mahakama ya Wilaya Wangingombe. Waliosimama kutoka kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi.Melea Mkongwa, anayefuata ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya  Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku anayefuata ni Afisa Utumishi wa Mahakama yaHakimu Mkazi Njombe, Bi. Happy Merere, anayefuata ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe na wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe, Mhe.James Muhoni kwa pamoja wakishuhudia zoezi la upandaji mti.

Viongozi kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Iringa akiwemo  Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Dunstan Ndunguru (wa pili kushoto) wakizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe walipotembelea Mahakama hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama  ya Hakimu Mkazi wilaya Wanging’ombe. Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, wa kwanza kulia  ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Njombe, Mhe.Liadi Chamshama na wa pili kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bi.Happy Merere.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru akisoma moja ya jalada la zamani ndani ya jengo la zamani la Mahakama ya mwanzo mdandu ambalo ni la kihistoria lililojengwa na Wakoloni lililotumiwa na Machifu kuendeshea Mashauri mahakamani.

Makabati ya kihistoria ya kikoloni ambayo yalikuwa yanatumika kutunzia majalada ya mashauri yaliyokuwa yanaendeshwa na machifu enzi hizo. Makabati hayo yapo Mahakama ya zamani Mdandu.

Muonekano wa nje wa Jengo la kihistoria lililojengwa na wakoloni ambalo machifu walitumia kuamua mashauri kwenye jengo hilo la zamani la Mahakama ya Mwanzo Mdandu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ,kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru akikagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Jengo  la Mahakama ya Mwanzo lupembe ambalo lipo kwenye hatua za mwisho za kukamilika kwake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ,kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru akiwa katika picha pamoja na Viongozi wa Mahakama ya Mkoa Njombe.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni