Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo magazetini. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo magazetini. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 23 Januari 2022

ONDOENI KESI ZISIZO NA USHAHIDI MAHAKAMANI


Na Magreth Kinabo- Mahakama

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Lubigija Ng’wilabuzu, ameiomba Mahakama ya Tanzania kuondoa kesi zisizokuwa na ushahidi mahakamani, isipokuwa zile zenye mazingira ya kiusalama, mfano kuua au kubaka ili kuweza kupunguza mlundikano wa mahabusu  magerezani.

Bw. Ng'wilabuzu, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, ametoa ombi hilo leo tarehe 23 Januari, 2022 baada ya kushiriki katika matembezi ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ulioandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.Matembezi hayo yalianzia Mahakama Kuu ya Tanzania mpaka mahakama hiyo.

Ameviomba vyombo husika kushirikiana na Mahakama kuziondoa kesi hizo kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya mahabusu katika magereza.

‘‘Uondoshaji wa mashauri haya yasiyokuwa na ushahidi mahakamani utasaidia kupunguza idadi ya mahabusu magerezani, pia utasaidia Serikali kupunguza gharama za kuwahudumia. Hatua hii itawapa fursa Majaji au Mahakimu kupata fursa ya kusikiliza mashauri mengine,’’ alisema Ngw’ilabuzu.

Aliongeza kuwa njia nyingine ya kupunguza mlundikano huo ni vyema mtuhumiwa kupelekwa mahakamani wakati ushahidi ukiwa umeshakamilika.

Kaimu Mkuu wa Mkoa huyo alisema siku za nyuma walikuwa wanapokea malalamiko mengi kuhusu mashauri kukaa muda mrefu mahakamani au kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama, lakini hivi sasa malalamiko hayo hayapo.

Hata hivyo, alisema kuwa changamoto iliyopo ni mashauri ya ardhi, hivyo alishauri wanasheria wa Serikali, Mawakili na Mabaraza ya Ardhi kushirikiana ili kuweza kutatua suala hilo. Pia alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama ili kuboresha miundombinu chakavu.

Aliwaomba wananchi kufika katika viwanja hivyo, ambapo maadhimisho hayo yameaanza leo tarehe 23 Januari, 2022 na yatamalizika tarehe 29 Januari, 2022, ili kupata elimu ya mambo mbalimbali kuhusu masuala ya kisheria. Kauli mbiu ya maashimisho hayo ni ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao’.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma alisema Kanda hiyo imeweza kusajili zaidi ya mashauri 1,871 kati ya mashauri 2,225 yalisajiliwa kwa njia ya mtandao ambayo ni sawa na asilimia 84. Aidha alisema kwa kipindi cha mwezi Desemba pekee jumla ya mashauri 798 yalisikilizwa kwa njia ya ‘Video Conference’ katika ngazi zote za Mahakama.

Alifafanua kuwa Kanda hiyo iliongoza kwa kusikiliza mashauri mengi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mwezi Desemba, ambapo ilisikiliza mashauri 6,352.

‘‘Kanda ya Dar es Salaam katika ngazi zote za Mahakama iliingia na jumla ya mashauri 13, 448 yaliyokuwa yamebakia kipindi cha mwaka 2020, huku jumla ya mashauri 39,031 yalifunguliwa na mashauri 40,146 yalisikilizwa na kubakiwa na mashauri 12, 333. Kati ya mashauri yaliyobakia hadi kufikia mwaka 2021 ni asilimia 15,’’ alisema Jaji Mruma.  

Jaji Mruma alisema ufanisi huo wa kazi umetokana na malengo ya kusikiliza mashauri ndani ya muda uliopangwa


  Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Lubigija Ng'wilabuzu  akizungumza              jambo, wakati akifungua Maadhimisho ya Wiki ya Sheria  kwa  Mahakama Kuu ya            Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam leo kwenye viwanja kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. 
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma akizungumza   , wakati akitoa hotuba yake kwenye mazungumzo ya  Maadhimisho ya Wiki ya Sheria  kwa  Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam leo kwenye viwanja kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wadau wa Mahakama wakiwa katika matembezi hayo.

Bendi ya polisi ikitumbuiza matembezi hayo.
Watumishi hao na wadau wakifanya mazoezi.

Jumatano, 11 Mei 2016

MAHAKAMA NA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

             MAHAKAMA NA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

Kwa mujibu wa Kifungu 107 (A) Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa Mahakama. Na kazi kubwa ya Mahakama kama mhimili ni kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge.Kwa wananchi walio wengi kazi ya vyombo vya habari ni kama Mahakama kwa maana ya ukweli kuwa habari hutumika kwa ukweli na uhakika kwa wananchi.

 Tarehe 2 na 3 Mei 2016 itakumbukwa na Wanahabari wengi nchini kwa kuadhimisha siku ya muhimu ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani. Madhimisho hayo yaliyofanyika katika Hoteli maarufu ya Malaika Beach Resort jijini Mwanza, yaliambatana na maadhimisho ya miaka 25 ya Azimio la Windhoek lilioridhia kuanzishwa kwa Tasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika yaani (MISA). Wanahabari waliadhimisha pia miaka 250 ya sheria ya kwanza ya kupata taarifa ikijumuisha nchi ya Sweden na Finland. Kadhalika kongomano hilo la siku mbili lilitathimini mafaniko ya mwaka wa kwanza wa miaka 15 ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Millenia (Sustainable Development Goals (SDGs) ya Umoja wa Mataifa.

Katika kongomano hilo la Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani mgeni rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Mohamed Chande Othman, ambaye katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Mwanza Mhe.Robert Makaramba alielezea umuhimu wa Mahakama kuheshimu Uhuru wa vyombo vya habari katika mustabali wa kuleta demokrasia ya kweli nchini.  Aidha Mhe. Jaji Mkuu aliendelea kwa kuwauliza wanahabari ni kwa kiasi gani vyombo vya habari huripoti habari za maendeleo,haki za binadamu, masuala ya utawala bora?. Na vipi Wahariri wetu hupima ubora wa habari zinazoandikwa katika magazeti yetu na je kiandikwacho kinaweza kuleta mabadiliko kwa mtu atakayesoma,kusikiliza,ama kuona habari hiyo? 


   Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Robert Makaramba (aliyesimama) akisoma hotuba kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Mohamed Chande Othman wakati ufunguzi wa Komngomano la Sikiu ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani katika Hotel ya Malaika Beach Resort Jijini Mwanza.

Maswali haya yaliibua mjadala kuhusu haki ya kupata habari na uhuru wa vyombo vya habari kwa ujumla. Mhe.Jaji mkuu alileeza kuwa, Mahakama kama mdau wa habari inashauri  wanahabari kupambana na changamoto zilizopo katika kuwasilisha habari za aina tofuti. ‘’ Kuna changamoto kubwa katika kauandika habari zinazohusu haki za binadamu. Kwa siku za karibuni suala la haki za binadamu limekuwa likipigwa chapuo na wadau wa eneo hilo kwa kiasi kikubwa ‘’ alisema Jaji Mkuu. 

Serikali na viongozi mbalimbali wamekuwa wakirejea misingi ya kimataifa ya haki za binadamu kwenye matamko ya sera na hotuba mbalimbali. Mahakama inatambua kuwa, uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu, kukuza utawala bora pamoja na kukuza demokrasia. Alitoa mfano wa uhuru wa wa vyombo vya habari kati ya India na China, ambazo zote zilipata uhuru kwa wakati mmoja ila china ilifanya vizuri katika maendeleo ya kijamii  na uchumi lakini katika eneo moja India iliipiku China. India huru iliweza kuipiku China kwa kushinda majanga mbalimbali kama njaa .Hiii iliwezekana kwa sababu ya mfumo wa vyama vingi na uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo huru vya habari huonya jamii juu ya majanga mbalimbali yanayoweza kutokea, na maonyo hayo hufanya jamii kujikinga mapema. Kwa maana hiyo, uhaba wa upatikanji wa habari ni aina nyingine ya umasikini na inaaminika kuwa, kwa kiasi kikubwa bila taarifa sahihi huwezi kufanya maamuzi.

      Mahakama ya Tanzania kwa kutambua changamoto na umuhimu wa utoaji na upatikanaji wa habari kote kwa watumishi wa Mahakama na waandishi wa habari,  ilifanya mambo kadhaa yakiwemo, kwa  kushirikiana na Baraza la Habari la Tanzania (MCT) yalianzishwa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari yakilenga namna bora ya kuripoti habari za Mahakama. Waandishi mbalimbali 42 walinufaika na mafunzo hayo na matunda yake yameanza kuonekana kwa kufuatilia habari mbalimbali za Mahakama kwenye vyombo vya habari. 

Aidha,ili kuhakikisha kuwa waandishi wetu wa habari wanapata taarifa za Mahakama ya Tanzania kwa wakati na urahisi,kwa kushirikiana na Tasisi ya Vyombo vya Habari kusini mwa Afrika (MISA) yamenzishwa mafunzo maalum yahusuyo upatikanaji wa taarifa na huduma bora kwa wateja kwa huduma ya kada mbalimbali za Mahakama. Hadi sasa zaidi ya watumishi 150 wamenufaika na mafunzo hayo. Kwa hiyo, ni kweli kuwa juhudi hizi zinazofanywa na Mahakama inaendana kwa kiasi kikubwa na dhima ya mwaka huu ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari nchini.

Dr. Reginald Mengi, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania MOAT (aliyesimama), akisoma risala fupi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya  Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa 2016.

Hata hivyo, ni kweli usiofichika kuwa vyombo vya habari vinapaswa kupewa pongezi kubwa  kwa kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mwaka jana kwa kuripoti habari cha uchaguzi kuanzia wakati wa uchukuaji fomu,kuteua wagombea na suala zima la kampeni. Vyombo vya habari vilichangia kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi ule wa kihistoria.
      
 Kuhusu uhuru wa habari na kujieleza, Mahakama inaamini haki ya msingi ya uhuru kujieleza, ukihusisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa kama katiba inavyosema. Lakini kwa upande mwingine, Mahakama haiamini katika kusema chochote bila kujali unakisemea wapi,kwa nani na kwa manufaa gani. Hivyo Mahakama inamini kuwa haki yoyote lazima iambatane na wajibu na pia inaamini kuwa uwepo wa sheria nzuri ya vyombo vya habari ni chachu kubwa ya maendeleo. Hata hivyo, sheria hizo nzuri haziwezi kupatikina bila kushirikisha wadau husika. Mahakama inaaminini kuwa wote wanaohusika katika kutunga sheria mbalimbali watashirikiana kufanya kazi hiyo sio kwa maslahi ya mtu fulani bali kwa maslahi ya nchi.

Tunaamini kuwa jukumu la msingi la vyombo vya habari ni kusimamia uwajibikaji na utawala bora na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi. Aidha, ni wazi kuwa utekelezaji wa jukumu hili kwa vyombo vya habari hauwezekani kama hakuna sheria huru na endelevu ya vyombo vya habari. Hivyo Mahakama ina nia ya dhati kabisa kushirikiana na vyombo vya habari ikiwa kila mtu mhusika atatekeleza wajibu wake ili kuleta Tanzania yenye mafanikio.

Wanahabari na Wadau wa Habari wakiwa katika katika Maadhimisho ya Siku ya  Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2016 yaliyofanyika Kitaifa katika Hotel ya Malaika Beach Resort Jijini Mwanza.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari wakati wa kuripoti masuala ya uchaguzi kwa
 kiasi kikubwa hata katika demokrasia iliyokomaa popote pale, bado kuna tabia ya vyombo vya habari kuonesha mapenzi binafsi na vyama au mgombea fulani na vyombo vya habari huendeleza malumbano baina ya chama fulani na wafuasi wao na kusahau mambo ya msingi ya maendeleo wananchi. Ni tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kuendeleza kejeli ,kashfa na matusi na kuona ni kawaida katika jamii.’’Mambo haya yameonekana hapa kwetu kwenye uchaguzi wa mwaka jana’’ alisisitiza Jaji Mkuu. 

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Mnauye  (wa tatu toka kulia walioketi) katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa ,Wanahabari na Wadau wa Habari wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya  Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2016,yaliyofanyika mkoani Mwanza.
 

Ijumaa, 22 Aprili 2016



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 MAHAKAMA  

TANGAZO
            YAH: WASHINDI WA SHINDANO LA KUSANIFU BENDERA NA NEMBO YA MAHAKAMA

1.    Kwa mujibu wa Katiba  kifungu 107 (A) Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama. Sheria ya Bendera na Nembo ya Taifa, sura ya 10 kifungu cha 6 (1) inaruhusu taasisi yoyote ya Serikali ama Umma kuwa na Bendera yake ambayo ndani yake itakuwa na Bendera ya Taifa, Nembo ama alama yoyote ilivyooneshwa katika kifungu 6 (1) cha sheria ya bendera na Nembo ya Taifa.

2.     Mahakama ya Tanzania, ilitoa tangazo tarehe 29 Aprili 2015 katika magazeti ya Daily News,Mwananchi pamoja na The Gurdian kuhusu shindano la kusanifu Nembo na Bendera ya Mahakama. Jumla ya washiriki 224 walituma michoro yao. Baaada ya kupitia kwa kina na kamati maalumu ya wataalamu, wafauatao wanataarifiwa kuwa wameteuliwa kuwa washindi wa shindano hilo kama ifutavyo:

i)                   Clarance J.Mhoja
ii)                 Emanuel Makene/Patric Mwakitosi
iii)               Charles Kitanda
iv)               Moses Luhanga
v)                 Huruma S.Mpombo
vi)               Lightness Sirikwa
vii)             Zena Kidabu
viii)           Mwidadi M.Msangi
ix)               Jeremiya Mayeye
x)                 Hamisi Salum Fundi

3.     Washindi tajwa hapo juu wanaomba kuwasiliana na Ofisi ya Mtendaji Mkuu  Mahakama, iliyopo barabara ya kivukoni nyumba namba 26 ili kupata taratibu kutunukiwa zawadi zao. Barua za maelekezo zimetumwa kupitia anuani zenu.
4.     Mahakama ya Tanzania inawashukuru wote waliotuma michoro yao na tunathamini michango yenu yote.

Imetolewa na:

         MTENDAJI MKUU,
                     MAHAKAMA YA TANZANIA,
                      26 BARABARA YA KIVUKONI,
                                                S.L.P 9004,
                                               11409 DAR ES SALAAM.