Na FAUSTINE KAPAMA na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. George Mcheche Masaju amewahimiza Mawakili wapya kuzingatia maadili,
uadilifu na weledi na kuishi viapo vyao wanapotekeleza majukumu yao katika
muktadha mzima wa utoaji haki kwa Wananchi.
Mhe. Masaju, ambaye ni Jaji
Mkuu wa tisa wa Tanzania na Jaji Mkuu wa saba Mtanzania, ametoa wito huo leo
tarehe 3 Julai, 2025 baada ya kuwapokea na kuwakubali waombaji 449 kuwa Mawakili
wa Kujitegemea.
Hili ni tukio lake la
kwanza tangu alipoapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu tarehe 15 Juni, 2025, kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Katika hotuba yake kwenye
sherehe hiyo ya uapisho iliyofanyika katika ukumbi wa Jiji Mtumba Jijini Dodoma,
Jaji Mkuu Masaju amewakumbusha Mawakili kuwa taaluma ya sheria ni wito wa
kuhudumia wananchi kwa haki na sio njia ya kujinufaisha binafsi.
“Mnaingia kwenye taaluma
nyeti inayogusa maisha ya watu. Haki ya mwananchi inaweza kupatikana au kupotea
kupitia maneno yenu. Kuweni waadilifu, wenye maadili, na waaminifu kwa wito
wenu,” amesema Mhe. Masaju kwa msisitizo.
Ameongeza kuwa Mawakili
wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanyonge, kulinda Katiba
na kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya kimahakama yanayoendelea nchini.
Hafla hiyo imehudhuriwa
na Viongozi wa Mahakama, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu
ya Tanzania. Alikuwepo pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa
Serikali.
Wengine ni Mwakilishi wa Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini, mwakilishi wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), familia za Mawakili wapya na Wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.
Uapisho huo unaashiria mwanzo mpya kwa Mawakili hao katika kujenga jamii yenye haki, usawa na utawala bora wa sheria.
Viongozi Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa sherehe hiyo. Kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni