- Awapokea, awakubali Mawakili wapya zaidi ya 400
Na FAUSTINE KAPAMA na
ARAPHA RUSHEKE- Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche
Masaju leo tarehe 3 Julai, 2025 amewapokea na kuwakubali waombaji 449, wakiwemo
wanaume 252 na wanawake 197, kuwa Mawakili wapya wa Kujitegeme.
Hili ni tukio kubwa la
kwanza kwa Mhe. Masaju kulifanya tangu alipoapishwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 15 Juni,
2025, kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Sherehe hiyo imefanyika
katika Ukumbi wa Jiji uliopo Mtumba katika Ofisi za Serikali na kuhudhuriwa na
Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Viongozi wengine wa
Mahakama.
Walikuwepo pia Viongozi
wengine, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwakilishi wa Mkurugenzi wa
Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali, Viongozi wa Baraza la Elimu ya Sheria na
Wananchi kwa ujumla.
Miongoni mwa Mawakili hao
wapya, 81 ni wale waliopata msamaha wa kutohudhuria Shule ya Sheria kwa Vitendo
baada ya kuhudumu katika masuala ya kisheria kwa muda mrefu.
Yupo pia mmoja aliyefaulu
mtihani wakuwa Wakili na wengine 367 waliofaulu katika Shule ya Sheria kwa
Vitendo.
“Kwa mamlaka niliyopewa
na Sheria ya Mawakili Sura 341, Kifungu cha 16 (4) natamka kwamba wale wote ambao
majina yao yamesomwa hapa wamekubaliwa kuwa Mawakili na wameingizwa rasmi
kwenye daftari la Mawakili kuanzia leo tarehe 3 Julai, 2025," amesikika
Jaji Mkuu akitangaza mara baada ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili hao wapya.
Tukio hilo la kuwapokea
na kuwakubali Mawakili hao wapya 449 lililofanywa na Jaji Mkuu linafĂ nya idadi
ya Mawakili nchini kuongezeka na kufikia 13,446.
Baada ya kukubaliwa, Jaji
Mkuu wa Tanzania aliwatunuku vyeti vya uwakili na kusema, “Kwa mamlaka niliyopewa
na Sheria ya Mawakili Sura 341, Kifungu cha 16 (4), nawatunuku vyeti vya
uwakili nyinyi wote Mawakili mliopokelewa na kukubaliwa kuwa Mawakili.”
Kisha Mawakili hao walikula kiapo cha uadilifu mbele ya Msaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa. Msajili wa Mahakama Kuu amewakumbusha Mawakili ambao bado ni watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya kuanza kutetea wateja hadi hapo watakapofika ukomo katika utumishi wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni