- Wabunge waipongeza Mahakama kwa maboresho ikiwemo matumizi ya TTS
- Wapongeza Uanzishwaji wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki ‘IJCs’
Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana tarehe 29 Aprili, 2024
lilipitisha jumla ya fedha za Kitanzania Bilioni 441.3 ikiwa ni bajeti ya Mwaka
wa Fedha 2024/2025 ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo Miradi ya
Maendeleo ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zilizopo chini yake.
Akizungumza wakati akiwasilisha Hotuba ya Mipango na Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025 katika Mkutano wa 15
wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe.
Dkt. Pindi Chana (MB) alisema Wizara hiyo imeendelea kusimamia na kuratibu
utekelezaji wa mipango inayolenga kufanikisha jukumu la kuimarisha mifumo ya
utoaji haki kwa kuweka mazingira yanayohakikisha usawa kwa wote na kwa wakati.
Mhe. Dkt. Chana alisema Serikali kupitia Wizara imejikita kushughulikia
masuala manne muhimu ili haki ipatikane kwa wote na kwa wakati ambayo ni pamoja
na kufanya mapitio ya mfumo wa Haki Jinai na kuandaa mpango wa marekebisho ya
Sheria ambazo zinatoa mianya ya ama kuchelewesha upatikanaji wa haki au
ukandamizaji katika upatikanaji wa haki.
“Katika kuendelea kusimamia upatikanaji wa haki kwa wananchi, Mahakama
imeendelea na mpango wa kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani, katika
kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Mahakama imeshughulikia jumla ya
mashauri 196,592,” alisema Mhe. Dkt. Chana.
Alieleza kuwa, kati ya mashauri hayo, mashauri 133,82 yamesikilizwa na
kuhitimishwa na mashauri 62,769 yaliyobaki yanaendelea kusikilizwa.
Aliongeza kwamba, katika mashauri yanayoendelea kusikilizwa, mashauri ya umri
mrefu ni 2,087 pekee sawa na asilimia tatu (3) ya mashauri
yote yaliyobaki Mahakamani.
Akizungumzia kuhusu, utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya
Mahakama katika ngazi mbalimbali, hadi kufikia Aprili, 2024, Miradi ya Ujenzi
iliyokamilishwa ni Mahakama za Wilaya ya Ulanga, Kwimba na Liwale; Ukarabati wa
jengo la Mahakama ya Wilaya ya
Maswa.
Ujenzi wa Majengo ya Mahakama za Mwanzo Usevya Mlele, Nyakibimbili Bukoba,
Mahenge (Kilolo), Newala Mjini, Madale Dar es Salaam, Kinesi Rorya na Luilo
Ludewa.
"Majengo ya Mahakama yanayoendelea ama kujengwa au kukarabatiwa ni kama
Ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita vya Katavi, Songea Ruvuma,
Songwe, Njombe, Simiyu na Geita," alieleza Balozi Mhe. Dkt. Chana.
Waziri huyo alisema ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo tatu ambazo ni
Ilangala (Ukerewe), Mbalizi (Mbeya) na Machame (Kilimanjaro).
Miradi mingine ni ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya sita (6) ambazo ni
Kibiti Pwani, Nachingwea Lindi, Simanjiro Manyara, Hanan’g Manyara, Mbulu
Manyara na Tunduru Ruvuma pamoja na Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya
Korogwe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 61, ujenzi wa Jengo la
Mahakama ya Wilaya Ubungo ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 98 na
ukarabati wa jengo la zamani la Mahakama Kuu Dodoma ambapo ukarabati wake
umefikia asilimia 49.
Kadhalika, Waziri huyo alizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo la Makao
Makuu ya Mahakama ya Tanzania ambapo hadi sasa umefikia asilimia 97.3 huku
akiongeza kuwa, ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kabanga-Ngara unaendelea na kwa
sasa upo asilimia 97, ujenzi wa nyumba 48 za Majaji eneo la Iyumbu Dodoma ambao
umefikia asilimia 98 na kuendelea kwa ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu jijini
Dodoma ambapo ujenzi umefikia asilimia 53.
Kwa upande mwingine, Waziri Mhe Dkt. Chana alisema katika mwaka wa fedha
2023/2024, Serikali imesajili jumla ya watoa huduma 46 walioomba kuthibitishwa
kama Watoa Huduma za Utatuzi wa Migogoro kwa njia mbadala, ambapo Waendesha
Maridhiano ni watatu (3), Watoa Huduma za Majadiliano watatu (3), Wapatanishi
13 na Wasuluhishi 27.
”Hadi kufikia Aprili, 2024 wapo Watatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala
576, kati ya hao, Waendesha Maridhiano 38, Watoa Huduma za Majadiliano 60,
Wapatanishi 185 na Wasuluhishi 293,” alisema Waziri Chana.
Aliongeza kwamba, Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Kituo cha
Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (Tanzania International Arbitration Centre),
Taasisi hiyo itakuwa na Kituo Dar es Salaam ambapo tayari jengo kwa ajili ya
kuanzisha Kituo hicho limepatikana.
Akizungumza wakati akichangia bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu wa Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama
aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa matumizi ya Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri
(TTS).
“Napenda kuipongeza Mahakama kwa hatua kubwa ya kuanza matumizi ya Mfumo
wa Unukuzi na Tafsiri (TTS), nipende kuishauri Mahakama kufunga Mfumo huu
katika Mahakama zote nchini ili kurahisisha upatikanaji wa Haki,” alisema Mhe.
Dkt. Mhagama.
Wabunge mbalimbali wamepata nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya
Katiba na Sheria iliyowasilishwa; miongoni mwa maoni na pongezi zilizotolewa ni
pamoja na pongezi kwa Mahakama juu ya uanzishwaji wa Vituo Jumuishi vya utoaji
Haki (IJCs), uwepo wa Mahakama zinazotembelea (Mobile Courts).
Kati ya Shilingi 441,260,152,000 zilizopitishwa na Bunge, jumla ya fedha
za Kitanzania Bilioni 241.6 ni bajeti ya Mfuko wa Mahakama fungu 40. Baadhi ya
Taasisi ambazo bajeti yake imesomwa na Wizara ni pamoja na Tume ya Utumishi wa
Mahakama, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mahakama, Tume ya
Kurekebisha Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu
wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara iliidhinishiwa na Bunge jumla ya
Shilingi 383,619,511,000 (bilioni 383.62) kwa ajili ya matumizi ya kawaida na
Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo Shilingi 97,815,618,000 (bilioni 97.82)
ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi, Shilingi 176,148,324,000 (bilioni
176.15) ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi 109,655,569,000 (bilioni
109.66) ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha za
maendeleo Shilingi 44,112,800,000 (bilioni 44.11) ni fedha za ndani na Shilingi
65,542,769,000 (bilioni 65.54) ni fedha za nje.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akisoma Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 Bungeni jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe., Eva Nkya wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 jijini Dodoma
Sehemu ya Viongozi wa Wizara ya KJatiba na Sheria pamoja na Taasisi zake wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 jijini Dodoma
Sehemu ya Viongozi wa Wizara ya KJatiba na Sheria pamoja na Taasisi zake wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake tarehe 29 Aprili, 2024 jijini Dodoma