Jumatatu, 15 Desemba 2025

MAHAKAMA KUU KANDA YA IRINGA YAWEKA HISTORIA

  • Yaadhimisha Jubilei ya miaka 20 tangu kuanzishwa
  • Ndiyo Kanda ya kwanza kuweka historia hiyo ya Mahakama Tanzania

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, leo tarehe 15 Desemba, 2025 imeweka historia ya kipekee baada ya kuadhimisha jubilei ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005.

Tukio hilo linaifanya Mahakama Kuu Iringa kuwa ya kwanza kati ya Kanda 20 za Mahakama Kuu Tanzania kuadhimisha jubilei tangu zianzishwe. Hatua hiyo imepongezwa na Viongozi wengi waliohudhuria maadhimisho hayo, akiwemo Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud.

Kanda nyingine za Mahakama Kuu zilizopo kwa sasa ni Dar-es-Salaam, Morogoro, Temeke,Tanga, Moshi, Arusha, Manyara, Mwanza, Bukoba, Geita, Shinyanga, Dodoma, Tabora, Sumbawanga, Kigoma, Mbeya, Songea, Mtwara na Musoma.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye viunga vya Mahakama hiyo, maarufu kama 'Uwanja wa Haki' yamehudhuriwa na Mhe. Aboud na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda mbalimbali.

Viongozi wengine wa Mahakama waliohudhuria maadhimisho hayo ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kwa niaba ya Msajili Mkuu na Mtendaji wa Mahakama Kuu, kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Majaji wastaafu, Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama, Mahakimu na watumushi wengine wengi wa Mahakama Kanda ya Iringa.

Kwa upande wa Serikali alikuwepo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa na Mawakili wa Serikali. Wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Dini na wananchi kwa ujumla.

Viongozi mbalimbali walipata nafasi ya kutoa salamu kwenye maadhimisho hayo. Katika salamu zake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewapongeza watumishi wa Mahakama kwa kuadhimisha miaka 20 tangua kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.

Amesema kuwa maadhimisho hayo yanawakumbusha umuhimu na wajibu wa kuzisimamia, kuzipigania na kuhakikisha haki za wananchi zinatolewa wakati wote.

“Sisi wote tunafahamu, umoja, mshikamano, amani na maendeleo yetu ni matunda ya haki. Kwa msingi huo, tunaendelea kuwajibika kama wananchi, viongozi na watumishi ndani ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha Taasisi hii muhimu iliyopewa mamlaka ya kikatiba kutafsi na kutoa haki kwa wananchi tunailinda, tunaitetea na kuiwezesha kufanya wajibu huu wa msingi ili haki iweze kutamalaki katika jamii yetu,” amesema.

Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuipa ushirikiano Mahakama pale kesi zinazopoanza ili wanapohitajika mahakamani kutoa ushahidi wajitokeze ili kurahisisha mchakato wa haki .

Naye Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Mkoa wa Iringa, Wakili Msomi Moses Ambindwile, amesema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imeandika na inaendelea kuandika historia ya kipekee katika utoaji haki na ujenzi wa uongozi wa Mahakama ya Tanzania.

Wakili Msomi Ambindwile amebainisha pia kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imekuwa mithiri ya Chuo Kikuu cha Uongozi nchini kwa kutoa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye, Mhe. Rehema Kerefu, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.

Kwa mujibu wa Wakili Msomi, wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dunstan Ndunguru, Mhe. David Ngunyale, Mhe. Ruth Massam, Mhe. Isaya Arufani, Mhe. Augustine Rwizile, Mhe. Gladys Barthy, Mhe. Cyprian Mkeha, Mhe. Martha Mpaze na Mhe. Victoria Nongwa.

“Lakini pia imewahi kutoa Jaji Viongozi wawili, Mhe. Fakih Jundu na Mhe. Dkt. Feleshi na Wanasheria Wakuu wa Serikali wawili, Mhe. Fredrick Welema na Mhe. Dkt. Feleshi, ambao wamewahi kufanya kazi hapa Kanda ya Iringa,” amesema.

Ameeleza kuwa wao kama TLS wataendelea kusimama bega kwa bega na Mahakama kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wakati wa maadhimisho hayo kulifanyika uzinduzi wa Jarida la Mahakama Kanda ya Iringa linaloitwa, "Uwanja wa Haki " ambao ulifanywa na Mhe. Aboud. Jarida hilo limesheheni makala mbalimbali zinazoelezea historia ya Mahakama Kanda ya Iringa, shughuli za usikilizaji wa mashauri na utendaji kwa ujumla na andiko la kusisimua la chimbuko la Mahakama ya Mwanzo Kalenga iliyopo kwenye Makumbusho ya Taifa ya Kalenga ya Chifu Mkwawa.

Burudani za ngoma, bendi na kwaya ya Mahakama Kanda ya Iringa zimepamba maadhimisho hayo. Kikundi cha Ngoma Kibate kinachocheza na Nyoka aina ya Chatu kimekonga nyoyo za wananchi waliokuwa wamefurika kwenye viunga hivyo vya Mahakama. Kulifanyika pia igizo la mfano wa namna Mahakama inavyofanya kazi wakati wa kuendesha mashauri.

Kabla ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuanzishwa mwaka 2005, shughuli za kimahakama katika Mkoa wa Iringa na Njombe zilikuwa zinafanyika katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Meza Kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud ikifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa maadhimisho ya jubilei ya miaka 20 tangu Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuanzishwa mwaka 2005. Picha chini ikiimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki.


 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James akiwasilisha salamu kwenye maadhimisho hayo. Picha chini ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Mkoa wa Iringa, Wakili Msomi Moses Ambindwile.


Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jarida la Mahakama Kanda ya Iringa kwenye maadhimisho hayo. Picha chini akionesha kwa wananch Jarida hilo.



Kaimu Jaji Kiongozi na Amidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Imani Aboud, akikata keki kwenye maadhimisho hayo.

Mahakimu wa ngazi mbalimbali wa Mahakama Kanda ya Iringa [juu na chini] wakifuatilia kilichokuwa kinajiri.



Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Iringa na wananchi wakiwa kwenye maadhimisho hayo.


Sehemu nyingine ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Iringa [juu na chini] wakiwa kwenye maadhimisho hayo.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Victoria Nongwa, akisakata ngoma kwenye maadhimisho hayo. Picha chini ni fundi wa kucheza na nyoka hatari, Chatu, kwenye ngoma mbalimbali.


Bendi ya Mahakama Kanda ya Iringa ikitumbuiza kwenye maadhimisho hayo.

Kwaya ya Mahakama Kanda ya Iringa [juu na chini] ikilishambulia jukwaa kwenye maadhimisho hayo.



Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Iringa wakionesha mfano namna Mahakama inavyoendesha shughuli za kusikiliza kesi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni