Na. DANIEL SICHULA – Mahakama, Mbeya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mbeya
Mhe. Joachim Tiganga amefungua mafunzo ya utoaji elimu ya kupinga ukatili wa
kijinsia mitandaoni ikiwa ni maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia kwa wanawake na watoto ikiwemo rushwa ya ngono.
Mhe. Tiganga amewakumbusha washiriki na wadau kwamba unyanyasaji
wa kijinsia mitandaoni si suala la utani bali ni uzalilishaji mkubwa ambao
umekuwa ukiathiri afya ya akili za wanajamii hasa vijana na watoto pia kutoa
wito kwa wadau kusimama kidete kupinga ukatili wa kijinsia mitandaoni ili
kutengeneza mazingira salama kwa kila mmoja wetu.
“Ni
muhimu kukumbuka kuwa kuna madhara makubwa ya tabia na maneno yetu mitandaoni,
kilichoandikwa mtandaoni kimeandikwa. Unaweza usione madhara yake leo lakini
baadaye itakuathiri tu. Inatupasa
kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii vizuri ili kuileta jamii pamoja
kwenye mawasiliano chanya kuliko kutumia kama njia ya kuwaathiri wengine hasa
vijana na watoto,’’ alisema Mhe. Tiganga.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Majaji
na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa, alifafanua kauli mbiu ya mwaka 2025 katika maadhimisho
ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Katika kuadhimisha siku ya kupinga ukatili wa
kijinsia mitandaoni, tumejielekeza zaidi katika utoaji elimu ya uelewa kwa
jamii juu ya ukatili wa kijinsia hasa ya rushwa ya ngono katika katika nyanja mbalimbali,’’
alisema Mhe. Nongwa
Aidha, alisema kuwa, utoaji elimu ya kupinga ukatili
wa kijinsia kwa washiriki na wanafunzi wa kitivo cha sheria wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki
Mbeya (CUoM) elimu itakayotolewa ni kwa vitendo kwa kutumia Mahakama ya mfano (Mootcourt)
ili kila mshiriki aweze kuelewa juu ya uendeshaji wa kesi za aina hiyo ya
ukatili wa kijinsia.
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitivo cha Sheria wa Chuo Kikuu
cha Kikatoliki Mbeya Dkt. Abduraman Kaniki ameshukuru uongozi wa TAWJA Kupitia
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kwa kuchagua Chuo hicho katika utoaji wa elimu ya
kupinga ukatili wa kijinsia.
“Napenda kuwapongeza uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Mbeya kutoa elimu hii kwa wanafunzi hawa, kwani watajifunza vitu vingi na
kwakua elimu inatolewa kwa vitendo na kila mmoja wetu atashuhudia namna kesi
zinavyoendeshwa mahakamani hakika hili ni darasa muhimu sana kwa wanafunzi wa
sheria walioko hapa katika kupinga ukatili wa kijinsia mitandaoni na kuweza
kutambua matumizi salama ya mitandao,” alisema Dkt. Kaniki.
Katika utoaji wa elimu hiyo TAWJA Kanda ya Mbeya
imeshirikiana na wadau wa haki jinai wakiwemo Mahakimu, Mawakili wa Serikali,
TAKUKURU, Dawati la jinsia, Mawakili wa Kujitegemea, Wahadhili pamoja na
Maafisa Ustawi wa Jamii.
Washiriki wa Mahakama ya Mfano (Mootcourt) pamoja na
wadau katika utoaji wa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia walitunukiwa vyeti
pamoja na vikombe vyenye ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia mitandanoni.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa haki jinai waliotoe elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia mitandaoni watatu kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akifungua mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia mitandaoni .
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa akifafanua jambo wakati wa utoaji elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia mitandaoni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa
Mhe. Joyce P. Massawe akitambulisha uongozi wa Mahakama Mbeya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni