Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
leo tarehe 31 Januari, 2023 amefungua Kongamano la siku moja la wadau lenye
lengo la kujadili wajibu na nafasi ya Mahakama katika kuboresha mazingira ya
biashara nchini.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji wa
Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, Jaji Mkuu alibainisha kuwa Mahakama
ya Tanzania imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na changamoto na vikwazo vya
upatikanaji wa haki, ikiwemo ucheleweshwaji wa mfumo wa Mahakama na mlundikano
wa mashauri katika ngazi na hatua mbalimbali.
Alisema kuwa hatua hizo zilikuja chini ya awamu ya miaka
mitano ya Mpango Mkakati katika uboreshaji wa huduma za Mahakama na Mradi wa
Utoaji wa Huduma za haki ambapo Mpango Mkakati wa kwanza wa Mahakama wa Miaka
Mitano ulianza 2016 hadi 2021.
“Mpango huu ni mwitikio wa Mahakama kwenye changamoto
zinazokabili upatikanaji na utoaji wa haki nchini Tanzania na uliendana na Dira
ya Maendeleo ya Tanzania 2025. Kupitia Mpango Mkakati huu, Mahakama ilipanga,
kubuni na kutekeleza mfululizo wa mikakati ya maboresho ya muda mfupi, muda wa
kati na mrefu ambayo ilitoa huduma za kimahakama zinazozingatia wananchi,"
alisema.
Jaji Mkuu alibainisha zaidi kuwa Mahakama ya Tanzania
imeendelea na awamu yake ya pili ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama
(2021-2025), ambao inaendelea kuutekeleza kupitia Mradi wa Uboreshaji wa
Mahakama na Utoaji Huduma za Haki kwa Wananchi wa Tanzania.
“Katika Kongamano hili, mtapata baadhi ya vionjo vya yale
ambayo Mahakama ya Tanzania imekuwa ikifanya katika kipindi cha miaka minane
iliyopita ya kufanya maboresho ya kimahakama,” aliwaambia washiriki wa
Kongamano hilo.
Jaji Mkuu alieleza zaidi kuwa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inabainisha uhakika wa upatikanaji wa haki
na kuweka jukumu hilo kwa Mahakama kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mtu
anayetafuta haki hiyo.
Aliwaambia washiriki wa Kongamano hilo kuwa licha ya
taasisi tofauti za sekta ya umma na binafsi walizotoka, wote wanashiriki mambo
mengi yanayowahusu, ikiwemo uwepo wa Mahakama huru ambayo inachangia amani na
usalama.
"Sote tunataka Mahakama kulinda haki za kimsingi za
watu binafsi, kutatua migogoro ya kibiashara kwa haraka na kusimama imara dhidi
ya ufisadi kwa umma na binafsi. Kila mdau ana matarajio kutoka kwa Mahakama,
hivyo kutambua maboresho ambayo kila mmoja wetu anafanya ni muhimu kwa
matarajio yetu ya pande zote mbili, "alisema.
Jaji Mkuu alieleza zaidi kuwa Mahakama ya Tanzania
imeandaa mwongozo kuelekea kwenye mabadiliko ya kielektroniki ya haki ili
kuziba pengo la utoaji haki. Alisema kuwa Serikali ya Tanzania imeanzisha Mradi
wa Kidijitali Tanzania.
“Mradi wa Kidijitali Tanzania unatambua kwamba uchumi wa
kidijitali ni mustakabali wa Tanzania na mapinduzi ya kidijitali yatakuwa
kichocheo muhimu cha ukuaji na ustawi wa Tanzania katika siku zijazo. Ni wakati
wa kuboresha programu zetu za kidijitali zinazotumia teknolojia ya kidijitali
kubadilisha michakato ya haki na miundo yetu ya utoaji huduma,” alisema.
Awali katika
salamu zake za ukaribisho kwa niaba ya kamati ya maandalizi, Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt.
Paul Kihwelo alieleza kuwa wanaona ni bahati kuwa wenyeji wa Kongamano hilo la
siku moja ambao lengo lake ni kushirikisha na kutafuta mawazo ili kuibua
mijadala zaidi, kwani Mahakama iliyopewa dhamana pekee ya kutoa haki inaweza
kufanya zaidi na zaidi ili kulainisha magurudumu ya biashara na uwekezaji,
hivyo kuboresha mazingira ya biashara nchini.
“Kongamano hili ni ushuhuda wa wazi wa azimio na dhamira
ya Mahakama ya kuwashirikisha wadau wakuu katika sekta ya utoaji haki kwa
kuzingatia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama (2021-2025) ili kufikia
malengo ya Uboreshaji wa Huduma za Mahakama kwa Wananchi na Mradi wa Utoaji
Huduma za Haki katika kuboresha hali ya biashara, "alisema.
Mhe. Dkt. Kihwelo alisisitiza kuwa uchaguzi wa mada,
wasimamizi, wazungumzaji na washiriki umefanywa kimkakati ili kupata mafanikio
makubwa ndani ya siku moja na walikuwa na matumaini makubwa kutaibua mijadala
na washiriki watakuwa huru kuzungumza na kuchangia mawazo yao kwa uwazi.
Ufunguzi wa Kongamano hilo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David
Concar, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustepher Siyani,
Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Majaji wa
Mahakama ya Afrika Mashariki, maafisa wa Mahakama waliostaafu na walioko kazini
pamoja na Mahakama ya Uingereza. Washiriki wengine wa Kongamano hilo ni kutoka
taasisi binafsi, taasisi za umma pamoja na wizara mbalimbali.
Jaji Mkuu aliungana na washiriki wa Kongamano hilo
lililokuwa linafanyika katika Hoteli ya Morena jijini hapa wakati wa
mchana akiwa ameongozana na Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman
na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Gerson Mdeme.
Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya
Tanzania katika kushirikiana na wadau kwa mujibu wa matakwa ya Mpango Mkakati
wa Mahakama ya Tanzania (2020/21- 2024/25) hususani Nguzo ya Tatu ya Mpango
Mkakati huo ambayo inasisitiza ushirikishaji wa wadau.
Linafanyika kwa mara ya tatu baada ya Kongamano la
kwanza la namna hii kufanyika katika Wiki ya Sheria Februari, 2020 jijini Dar
es Salaam na la pili ambalo lilifanyika katika Wiki ya Sheria mwaka 2022 jijini
Dodoma, lengo likiwa ni kubadirishana uzoefu na kujadili namna ambavyo Mahakama
ya Tanzania inaweza kuchangia ukuaji uchumi nchini pamoja na ustawi wa biashara
kupitia utoaji haki kwa wakati.
Katika Kongamano hilo, mada mbalimbali ziliadiliwa na
kutolewa na wawezeshaji mahili wakiwamo wafanyabiashara, wawakilishi wa sekta
binafsi pamoja na sekta ya umma lakini pia Majaji kutoka Uingereza na Afrika ya
Kusini.
Jaji
wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija akizungumza katika Kongamano hilo
wakati anawasilisha hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 31 Januari, 2023 jijini
Dodoma.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na picha mbili chini) ikifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa wakati wa Kongamano hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni