Ijumaa, 31 Mei 2024

WAJUMBE KAMATI YA MAADILI YA MAAFISA WA MAHAKAMA WILAYA YA MOROGORO WAAPISHWA

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

 

Wajumbe wa kamati inayoshughulikia Maadili ya Maafisa wa Mahakama Wilaya ya Morogoro wamekula kiapo cha uaminifu katika kutekeleza majukumu yao.

 

Uapisho huo ulifanyika juzi tarehe 29 Mei, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma, kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa Mansoor.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mruma aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuzingatia misingi ya usiri muda wote wanapotekeleza majukumu yao.

 

“Niwapongeze kwa kuaminika na kuwa katika kamati hii. Kama ulivyo msingi wa kiapo, twende tukatekeleze majukumu yetu kwa kuzingatia maadili ya kazi, uadilifu na tutunze siri muda wote,” alisema.

 

Wajumbe wa kamati hiyo walioapishwa ni Mwenyekiti ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, Katibu Tawala, Bi. Lucy Joseph na wajumbe wengine ambao wanateuliwa na Mahakama, akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo.

 

Kamati hiyo inapewa nguvu kutekeleza majukumu yake chini ya kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 ambacho kimeiruhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Miongoni mwa kamati hizo ni Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya Wilaya.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma akimuapisha Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma akimuapisha Mjumbe wa Kamati, Bi. Lucy Joseph ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo akila kiapo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma (hayupo pichani).



Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama Wilaya ya Morogoro (picha mbili juu na mbili chini) wakila kiapo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya   Morogoro, Mhe. Amir Mruma (hayupo pichani).




(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)






 


 


 


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni