Jumanne, 4 Juni 2024

MAFUNZO MAALUM KUHUSU WAATHIRIKA WA UKATILI KINGONO YANAFANYIKA MOROGORO, MTWARA

Na Evelina Odemba- Mahakama Morogoro na Na Richard Matasha-Mahakama, Mtwara.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor jana tarehe 3 June, 2024 alifungua mafunzo ya namna ya kuepuka kutonesha majeraha ya kisaikolojia kwa waathirika wa ukatili wa kingono.


Mafunzo kama hayo ya siku tatu yanatolewa katika Mahakama Mtwara yakiwajumuisha Mahakimu 16. Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Martha Mpaze ndiye aliyefungua mafunzo hayo.


Kwa upande wa Morogoro, mafunzo hayo yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland na yanatolewa kwa Mahakimu 15 wanaohudumu katika Kanda ya Morogoro.

 

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mhe. Mansoor alisema kuwa imekuwa bahati kwakuwa yanawashirikisha watumishi wa Mahakama kutoka Kanda ya Morogoro na hata wawezeshaji pia ni sehemu ya watumishi wa Kanda hiyo. 

 

“Lengo letu katika siku hizi tatu sio tu kunyonya maarifa bali pia kumpa kila mshiriki ujuzi wa kuendesha kesi hizi kwa ufanisi, kubadilishana uzoefu wa namna tunavyoweza kuboresha katika kuwalinda wale waliothirika na ukatili wa kingono,” alisema.

 

Alitaja malengo mengine ya mafunzo kama kuchunguza mienendo tata ya unyanyasaji wa kijinsia na kuelewa jukumu muhimu ambalo wao kama Mahakimu na Majaji wanatekeleza katika kusimamia haki, huku wakilinda utu wa waathirika.

 

Mhe. Mansoor alisisitiza kuwa mada zitakazofundishwa zimepangiliwa kwa uangalifu ili kukuza uelewa wa namna ya kuwalinda mashahidi walio katika mazingira magumu, ikiwa ni sehemu ya majukumu ya washiriki hao katika kudumisha haki.

 

Aidha, Jaji Mfawidhi aliupongeza uongozi wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland kuona umuhimu wa kuwanoa Mahakimu hao katika uwanda huo na kuwataka washiri waliopata bahati kutumia nafasi hiyo vizuri kutanua fikra zao na kuboresha utendaji kazi.

 

Miongoni mwa wawezeshaji ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Fadhili Mbelwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo na Afisa Ustawi toka Manispaa ya Morogoro, Bi. Judy Mbelwa.

 

Akizungumza wakati anafungua mafuzo hayo katika Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Mpaze alisema, “Ni fursa ya kipekee tuliyopata kuletewa mafunzo haya, ni rai yangu tushiriki kwa ukamilifu ili tukayafanyie kazi haya katika vituo vyetu vya kazi.”

 

Alisema kuwa mafunzo hayo siyo tu zoezi la kukuza uelewa na maarifa bali pia ni kuhakikisha wanastawisha utendaji kazi wao katika Mahakama na kuepusha kutonesha majeraha ya mashahidi wa ukatili wa kijnsia na kingono.

 

Naye Mkufunzi wa mafunzo, ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Pamela Mazengo alisema mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwawezesha washiriki kuwa wakufunzi kwa Mahakimu wengine ili kuhakikisha mashauri yanayohusisha ukatili wa kijinsia na kingono, haswa kwa watoto yanaendeshwa ili kupunguza au kuondosha kutonesha majeraha yatokanayo na ukatili huo.

 


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.


 

Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe Martha Mpaze (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo. Kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe Seraphine Nsana na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, ambaye pia ni mkufunzi katika mafunzo hayo, Mhe Pamela Mazengo.


Afisa Ustawi, Bi. Judy Mbelwa akifafanua jambo wakati akitoa mada kwenye mafunzo yaliyokuwa yanafanyika Morogoro.



Mkufunzi ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe Pamela Mazengo akitoa mada wakati wa mafunzo Mtwara.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati), kushoto ni Naibu Msajili, Mhe. Fadhili Mbelwa na kulia ni Mtendaji wa Mahakama, Bw. Ahmed Ng’eni wakiwa na baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Kanda ya Morogoro (juu na chini).




Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe Martha Mpaze (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo Mtwara (juu na chini). Aliyeketi kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe Seraphine Nsana na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ,Mhe Pamela Mazengo, ambae ni mkufunzi wa mafunzo hayo.


 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Singida)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni