Ijumaa, 14 Juni 2024

MAHAKAMA KUU GEITA YAACHANA NA KARATASI

  • Shughuli zote za kimahakama zinaendeshwa kwa kutumia teknolojia
  • Ujenzi wa Kituo Jumuishi wapamba moto

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Geita

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, inaendesha shughuli zake zote za kimahakama katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa kutumia teknolojia na imeachana na matumizi ya karatasi kwa asilimia 100.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Kevin David Mhina alipokuwa anaongea na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami alipofanya ziara fupi katika Kanda hiyo.

“Mahakama yetu imefikisha miezi saba sasa na kasi ya usikilizaji wa mashauri siyo mbaya. Sisi hatutumii kabisa karatasi, it is paperless by 100 percentKinachotukwaza ni hukumu kwenye mfumo. Hatuwezi kuzipeleka kwenye TanzLii moja kwa moja,” alisema.

Mhe. Mhina alibainisha kuwa shughuli zote za kimahakama, ikiwemo ufunguaji wa mashauri na upokeaji wa rufaa kutoka katika Mahakama za chini, yaani Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya unafanyika kwa njia ya mtandao.

Shughuli zingine zinazofanyika kwa njia ya mtandao ni usikilizaji wa mashauri, upokeaji na ushughulikiwaji wa malalamiko, utoaji na usambazaji wa nakala za hukumu. 

Akiwasilisha taarifa ya utendaji kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, Bi. Masalu Cosmas Kisasila, Afisa Utumishi Hapiness Michael Mushi alieleza kuwa Mahakama Kuu, Kanda ya Geita ilianza tarehe 01 Desemba 2023 baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali No. 853A lililotolewa tarehe 22 Novemba, 2023. 

Alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo kumekuwa na mafanikio makubwa ya kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wananchi wengi kuleta mashauri yao kwa wepesi na umalizikaji wa haraka tofauti na awali ambapo iliwabidi kwenda Mwanza kupata huduma za Mahakama Kuu. 

“Tangu kuanzishwa kwa huduma hii katika Mkoa wa Geita, jumla ya wananchi 1,200 wameshahudumiwa. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na wastani wa wananchi 400 waliokuwa wakihudumiwa hapo awali katika kipindi cha Januari 2022 hadi Novemba 2023, wakati huduma hii ilikuwa ikipatikana Mwanza,” Bi. Hapiness alisema. 

Kuhusu hali ya mashauri, Afisa Utumishi alieleza kuwa idadi ya mashauri yaliyofunguliwa kuanzia Desemba, 2023 hadi Juni 6, 2024 yalikuwa 105, ambayo yamesikilizwa na kuamuliwa yapo 60 na mashauri 45 yanaendelea katika hatua mbalimbali za usikilizaji.

“Idadi hii ya mashauri yaliyopokelewa na yaliyoamuliwa ni kubwa ukilinganisha na mashauri yaliyokuwa yanaamuliwa hapo awali wakati huduma za Mahakama Kuu zilipokuwa zinapatikana Mwanza. Wastani wa mashauri 60 yalifunguliwa kwa kipindi cha Mei 2023 hadi Novemba 2023,” alisema.

Akielezea kuhusu ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Geita, Mbunifu Majengo Helmas Laurian alisema kuwa Mkandarasi Shandong Dejian High Speed Co. Ltd alikabidhiwa eneo la mradi tarehe 28 Novemba, 2023 na alianza ujenzi tarehe 15 Desemba, 2023 na anatarajiwa kukabidhi jengo tarehe 14 Septemba, 2024. 

Jumla ya gharama mpaka kukamilika kwa jengo hilo inategemewa kuwa kiasi cha Tshs 8,062,791,364.52. Kwa sasa mradi huo upo kwenye hatua ya ujenzi wa boma la jengo, sawa na asilimia 30 ya kazi ambayo imeshafanyika.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe.Kevin David Mhina (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami (hayupo kwenye picha).



Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami (kulia) akimweleza jambo Mhe. Mhina. Wengine katika picha ya chini ni Afisa Utumishi katika Mahakama Kuu Geita, Bi. Hapiness Michael Mushi (katikati) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Mhe. Cleofas Frank Waane.
 



Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami (kulia) akiagana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina baada ya kumaliza zira yake.

Afisa Utumishi katika Mahakama Kuu Geita, Bi. Hapiness Michael Mushi akiwasilisha taarifa ya utendaji kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, Bi. Masalu Cosmas Kisasila.


Mwonekano kwa nje wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Geita. 

Mbunifu Majengo Helmas Laurian (wa pili kulia) akitoa maelezo kuhusu ujenzi huo. Picha chini mafundi wakiendelea na kazi.


Mwonekano wa gorofa ya kwanza kwa sasa. 

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerald Chami (wa pili kushoto) akieleza njambo kwa  wasimamizi wa ujenzi alipokuwa kwenye gorofa ya kwanza wa jengo hilo.

Upande wa kusini wa jengo hilo.

Upande wa nyuma (mashariki) wa jengo hilo.

Upande wa mbele (Magharibi) wa jengo hilo.


Wakandarasi na wasimamizi wa jengo hilo wakiwa katika picha ya pamoja.


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni