Jumanne, 4 Juni 2024

MAHAKAMA, WADAU KIGOMA WAPATIWA MAFUNZO YA UHALIFU UTOKANAO NA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Rai imetolewa kwa Watendaji kutoka Mahakama, Idara ya Uhamiaji, na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wanaohusika na usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu Na. 6 ya mwaka 2008 kutumia Sheria hiyo vema ili kufanya majukumu yao ipasavyo. 

Rai hiyo imetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi  jana tarehe 03 Juni, 2024 wakati akifungua Mafunzo ya kuzuia na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu katika ukumbi wa Kigoma ‘Social Hall’ uliopo mkoani Kigoma.

“Moja ya malengo ya mafunzo haya ni pamoja na kuwajengea uwezo wadau wanaoshughulika katika mnyororo huo wa kuzuia biashara haramu ya usafirirshaji wa binadamu kwa mkoa wa Kigoma,” alisema Mhe. Nkwabi.

Aliongeza, kuwa biashara hiyo ni haramu kwa sababu imekatazwa na Sheria za Nchi na za Kimataifa hususani ya kulinda haki za binadamu, hivyo matendo yote yenye viashiria vya usafirishaji wa binadamu wenye lengo la kumfanya mtu kuuzwa kama bidhaa nyingine yoyote inayouzika sokoni inahusisha unyonyaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Hata hivyo, Mhe. Nkwabi alisema biashara hii ni muendelezo wa biashara ya utumwa na pia hujulikana kama utumwa mambo leo, ambayo ilianza mwishoni mwa karne ya 18 na kushamiri zaidi mwanzoni mwa karne ya 19 katika baadhi ya Nchi za Bara la Ulaya, ambayo ilitokana na sababu tatu muhimu moja ni mahitaji makubwa ya nguvu kazi, kuibuka kwa soko la ngono katika baadhi ya Nchi Duniani ambalo linahitaji Wasichana/Wanawake sambamba na kuibuka kwa soko la viungo vya binadamu Duniani.

Aidha, alizungumzia madhara ya biashara hiyo ambayo huenda sambamba na mateso makubwa kwa wahanga kama vile kupigwa, kubakwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi bila malipo, kunyang’anywa hati zao za kusafiria, kuuzwa kwa waajiri zaidi ya mmoja, kufanyishwa kazi bila mapumziko, kulazimishwa kutoa mimba na wengine kupata mateso makubwa na kupoteza uhai wao au kumuua ama kujiuwa mwenyewe kutokana na madhara hayo.

Jaji Nkwabi, aliwataka washiriki wa mafunzo kufuatilia kwa makini mafunzo hayo kwa kuwa yanakwenda kuboresha utendaji kazi wao katika eneo hilo na kusema kuwa, ndio mafanikio ya Nchi katika kupambana na Biashara hiyo haramu.

Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwaambia Watanzania hususani wanawake/wasichana kuwa, wamekuwa wakisafirishwa kwenda Nchi za Nje kama vile, Oman, Dubai, Qatar, India, Iraq, Malaysia, China, Thailand, Indonesia, Uturuki, Italia, Kenya, na Misri na kubainisha kuwa, wengi wao wamekuwa wakipata mateso makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu na wengine kupoteza maisha yao.

kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Makao Makuu Dodoma, katika Sekretarieti ya kuzuia na kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Kamishna Msaidizi wa Magereza Ahmed Mwendadi alisema kuwa, mafunzo hayo ni muhimu katika kukabiliana na janga hilo na kusema kuwa, Mikoa karibu yote nchini imepatiwa mafunzo hayo isipokuwa Mikoa minne (4) ndio bado ipo kwenye mkakati wa kufanya mafunzo hayo.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo Viongozi na Maafisa wanaoshughulikia jambo hili kwa karibu sana, na hii ni hatua kubwa yenye dalili za kuweza kukabiliana na usafirishaji Haramu wa binadamu katika Mkoa huu,” alisema Kamishna Msaidizi wa Magereza Mwendadi.

Alitumia fursa hiyo, kulishukuru Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (International Organization for Migration) kuwezesha mafunzo hayo kufanyika mkoani humo.

Naye, Afisa Mradi Msaidizi (Programme Assistant) kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Bw. Ken Heriel alisema kuwa Shirika hilo linaendelea na uratibu wake wa kuwezesha mikakati ya mipango kazi  ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ikiwemo Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu wa mwaka (2021-2024). 

Aidha, alisema Wadau wanalo jukumu la kufadhili mafunzo kwa Wasimamizi na Watekelezaji wa Sheria dhidi ya Uhalifu wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu pamoja na kuelimisha umma sambamba na kutoa huduma za ulinzi na mahitaji maalumu kwa wahanga, kuwarejesha kwao na kuwaunganisha wahanga na familia zao. 

Alifafanuzi kwamba, IOM imefanikiwa kutekeleza utoaji wa mafunzo hayo kupitia Mpango wa pamoja Kigoma ‘Joint Programme II’ unaotekelezwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo nchini Tanzania. 

Wadau wanaoshiriki mafunzo hayo ni Maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Maafisa Ustawi wa Jamii, Polisi na Mahakama.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kukabiliana na Uhalifu wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu yanayofanyika katika ukumbi wa (Kigoma Social Hall) uliopo mkoani Kigoma.
Kamishna Msaidizi wa Magereza, Ahamed Mwendadi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Makao Makuu Dodoma akitoa neno kwa Washiriki wa Mafunzo hayo.
Afisa Miradi Msaidizi (Assistant Project Manager) kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (International Organization for Migration-IOM), Bw. Ken Heriel akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Shirika hilo katika ufunguzi wa Mafunzo hayo.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Kibondo, Mhe, Maira Makonya, kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya kakonko, Mhe. Ambilike Kyamba.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Francis Nkwabi (wa tatu kulia)  akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mafunzo ya kukabiliana na Uhalifu wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu. Wa pili ni Kamishna Msaidizi wa Magereza, Ahmed Mwendadi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Makao Makuu Dodoma (kushoto) ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Rose Kangwa (wa nne kulia),  Mkaguzi wa Jeshi la Uhamiaji, Bw.Ally Nalinga (wa kwanza kushoto), na wa pili kushoto ni Afisa Miradi (Project Manager) kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (International Organization for Migration-IOM), Bw. Ken Heriel.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni