Jumapili, 9 Juni 2024

MAHAKIMU SINGIDA KAZI IPO

  • Wasafisha mashauri yote ya mlundikano

 

Na FAUSTINE KAPAMA - Mahakama, Singida. 

 

Mahakama katika Mkoa wa Singida imekamilisha usikilizaji wa mashauri kwa mwaka 2023 kwa zaidi ya asilimia 100, hivyo kutekeleza kikamilifu jukumu la utoaji haki kwa wakati kwa wananchi.

 

Akizungumza hivi karibuni na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard ChamiMtendaji wa Mahakama Singida, Bw. Yusuph Kasuka alisema kuwa katika ngazi zote za Mahakama walivuka mwaka 2022 na jumla ya mashauri 685.

 

“Mwaka 2023 tulipokea mashauri 6,369 kuanzia ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi hadi Mahakama za Mwanzo. Jumla ya mashauri 6,465 yameamuliwa na yanayoendelea kusikilizwa ni 589,” alisema.

 

Akielezea mchanganuo wa mashauri kwa kila ngazi ya Mahakama, Bw. Kasuka alieleza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ilivuka mwaka 2022 na mashauri 135, yaliyosajiliwa mwaka 2023 yalikuwa 131, mashauri yaliyosikilizwa na kuamuliwa yalikuwa 148        na yanayoendelea ni 118.

 

Kwa upande wa Mahakama za Wilaya Singida, Manyoni na Iramba, alieleza kuwa kwa pamoja zilivuka mwaka 2022 na jumla ya mashauri 348, mwaka 2023 yakafunguliwa mashauri 883, mashauri 999 yaliamuliwa na yanayoendelea yapo 232.

 

Akizungumzia upande wa Mahakama za Mwanzo, Mtendaji Kasuka alisema kuwa kwa pamoja zilivuka na mashauri 202 mwaka 2022, mwaka 2023 zikapokea jumla ya mashauri 5,355, yaliyoamuliwa yalikuwa 5,318 na mashauri yanayoendelea yapo 239.

 

"Naomba nieleweke kuwa tulikuwa na jumla ya mashauri 17 pekee ya mlundikano kwa ngazi za Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya hapa Singida. Mahakimu jinsi wanavyochapa kazi wamesafisha mashauri yote. Kwa sasa hatuna mashauri ya mlundikano,” alisema.

 

Mtendaji Kasuka alieleza kuwa mkakati uliosaidia kufikia mafanikio hayo ni uwepo wa vikao vya kuondosha mashauri (clean up sessions) ambapo Mahakimu walikuwa wanafanya kazi nje ya saa za kazi za kawaida.


Alisema kwamba mkakati uliopo kwa sasa ni kushughuka kwa haraka na mashauri yaliyobaki na yatakayofunguliwa kwa mwaka huu wa 2024 ili mwananchi aweze kupata haki yake inayopstahili kwa wakati. 


Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami (kushoto) akisalimiana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Ally Omary Nzowa alipowasili ofisini kwake kwa ziara fupi hivi karibuni. Aliyekaa kulia kwenye picha chini ni Mtendaji wa Mahakama Singida, Bw. Yusuph Kasuka.


Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami (wa pili kushoto) akizungumza na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Ally Omary Nzowa (katikati). Aliyekaa wa kwanza kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama Singida, Bi. Eva Leshange.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami (kushoto) akita katika picha ya pamoja na Viongozi Wakuu wa Mahakama Mkoa wa Singida.

Mtendaji wa Mahakama Singida, Bw. Yusuph Kasuka akifafanua jambo alipokuwa anazungumza ofisini kwake na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami (kushoto picha chini). Kulia katika picha ya chini ni Afisa Utumishi wa Mahakama Singida, ambaye pia ni Mwakilishi wa Kitengo cha Habari, Bi. Eva Leshange.



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni