Jumamosi, 22 Juni 2024

MKUU WA WILAYA YA ULANGA AIMWAGIA SIFA MAHAKAMA KWA KUBORESHA HAKI JINAI

Na EVELINA ODEMBA – Mahakama Ulanga, Morogoro

 

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga iliyopo mkoani Morogoro, Mhe. Dkt Julius Ningu ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa katika kutekeleza majukumu yake na kushirikisha wadau.

 

Mhe. Dkt. Ningu alitoa pongezi hizo wakati akifungua mafunzo ya ndani ya namna bora ya kushughulikia mashauri ya wanyamapori na makosa ya kujamiiana.

 

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mahakama ya Wilaya Ulanga na kutolewa kwa washiriki 38 ambao ni wadau wa Haki Jinai, wakiwemo Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Wapelelezi pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi.

 

“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka kwetu. Nimefurahishwa na ushirikiano mzuri wa Mahakama na Mihimili mingine ya Dora wilayani hapa. Kwa upande wa Serikali wilayani hapa tunaahidi kuzingatia mafunzo haya tutakayopatiwa ili tunapoenda kutekeleza majukumu yetu tuwe na jamii salama,” alisema.

 

Mhe. Dkt. Ningu alieleza kuwa anaungana na Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yake kwa mlengo wa kujumuisha wadau. 

 

“Kama mdau wa haki nimekuwa nikipokea simu nyingi za Wananchi wakitaka niwatatulie mashauri yao yaliyopo mahakamani. Jukumu hilo ni la Mahakama pekee, hivyo nashauri wananchi kutumia Mahakama kutafuta haki zao na wadau wasiingilie kazi ya Mahakama,” alihitimisha.

 

 Awali wakati akitoa neno la utangulizi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ulanga, Mhe. Christopher Bwakila alisema mafunzo hayo yatatolewa na wawezeshaji wa ndani ambao walipata mafunzo mkoani Mara hivi karibuni.

 

Alieleza kuwa mada zitakazofundishwa ni pamoja na namna ya kushughulikia vielelezo vinavyopatikana katika eneo la tukio, mbinu za kupeleleza mashauri ya wanyamapori, kuepuka makosa yanayojitokeza mara kwa mara katika kushughulikia makosa ya kujamiiana na namna ya kutotonesha madonda ya waathirika wa makosa ya ubakaji.

 

Kufanyika kwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo aliyoyatoa tarehe 17 Mei, 2024 mjini Tarime mkoani Mara.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Mhe. Dkt Julius Ningu (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ulanga, Mhe. Christopher Bwakila akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ulanga, Mhe. Christopher Bwakila akiwasilisha mada wakati wa mafunzo.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Mhe. Dkt Julius Ningu (katikati waliokaa) aki
 wa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo (juu na chini).


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama.

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni