Jumatatu, 3 Juni 2024

TUYAISHI MAFUNDISHO YA DINI KUJENGA UMOJA NA AMANI; WAZIRI MKUU

·       Asisitiza kuheshimu imani ya kila mtu ikiwa ndiyo siri ya amani ya Nchi

Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza.

Mazishi ya Mama Mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Bi Amina Nyanda Juma yalifanyika tarehe 01 Juni, 2024 mjini Tarime na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mahakama, watumishi wa Mahakama na mamia ya wananchi wa Tarime


Akitoa salama za pole za Serikali wakati wa mazishi hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alisema kuwa wingi wa watu amabo wameshiriki mazishi hayo unaonesha ni kwa jinsi gani marehemu alikuwa akishirikiana na jamii yake na hata kuweza kuwa kiongozi wa kidini wa wanawake waislamu wa eneo hilo la Tarime.


“Kama mnavyoona leo kupitia dini, Mama yetu aliweza kuwaunganisha wengi katika eneo hili na hata hapa wengi wapo wa dini tofauti tofauti ikionesha ni namna gani ambavyo marehemu aliishi vizuri na wananchi wote wa eneo hili pasipo kujali dini zao. Hii ndio sababu leo Tanzania imekuwa kimbilio la watu wengi ambao wanakimbia nchi zao kwa machafuko lakini Tanzania imekuwa ni kitovu cha amani…

kwa sababu Serikali inaheshimu imani ya dini ya kila raia aliyepo nchini na hivo hiyo ndiyo siri ya amani ya nchi yetu tofauti na mataifa mengine na hivo nawasihi sana mzingatie yale mazuri ambayo viongozi wetu wa dini wamekuwa wakituasa katika nyumba zetu za ibada,” alisema Waziri Mkuu.


Mhe. Majaliwa aliongeza kuwa, katika kipindi cha uhai wake, marehemu Bi. Amina alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha waumini wenzake wa kiislamu katika ujenzi wa msikiti mpya wa eneo hilo la Tarime akiwa kama muasisi wa msikiti huo lakini kufuatia ongezeko la watu msikiti huo umeoneka kuwa mdogo na hivyo kuanzisha mchakato wa ujenzi wa msikiti ambao ataendana na mahitaji ya watu wa eneo hilo.


“Kama ambavyo Shekh wa Mkoa wa Mara alivyosema kuwa marehemu ndiyo mwanzilishi wa Msikiti wa eneo hili na hii inazihirishwa wazi na umati wa watu hawa na kwa kipindi hicho waislamu walikuwa wachache, lakini kwa sasa msikiti huo hautoshi kutokana na ongezeko la waumini, na kama alivyoniomba Shekh wa Mkoa kuwa nikisimama niseme jambo kuunga juhudi alizoanzisha marehemu na mimi kwa kuunga mkono ninatoa kiasi cha shilingi milioni kumi kuunga mkono ujenzi wa msikiti mpya.” alisema Mhe. Kassim Majaliwa


Kwa mujibu wa Shekh wa Mkoa wa Mara, Msabaha Kassim Mgabo, alisema kuwa marehemu alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha waislamu wa eneo lake katika ujenzi wa msikiti mpya kutokana na msikiti uliopo kwa sasa kuwa mdogo kutoka na uongezeko la watu na hivyo alianzisha harakati wa ujenzi wa msikiti mpya  ili kuweza kukizi mahitaji ya waumini hao


Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahimu Juma, kwa niaba ya familia alitoa shukrani kwa wote walioweza kuhudhuria katika mazishi ya marehemu Bi. Amina na hata wale walio mfariji kwa njia moja ama nyingine hivyo kuonesha wazi kuwa katika kipindi hiki hayupo peke yake bali kuna wengi pia wanaomboleza naye. 


“Kwa niaba ya famila ya marehemu Mzee Juma Bwire tunatoa shukrani zetu za dhati kwenu wote ambao mmeshiriki nasi katika msiba huu wa Mama yetu mpendwa. Napenda kuwaasa pia katika kipindi ambacho wazazi wetu wangali hai tujitahidi sana kuwafanya wenye furaha, hakikisha kuwa kila siku mzazi wako analala akiwa mwenye furaha kutokana na neno ambalo amesikia kutoka kwako na hii itawafanya wazazi wetu kudumisha furaha katika familia zetu,” alisema Mhe. Prof. Juma 


Aidha, Mhe. Prof. Juma aliwaasa watu wote kuendeleza mshikamano baina yao kwani hata yeye anakiri wazi kuwa mara nyingi marehemu Mama yake alikuwa akihudumiwa na watu wa karibu ambao sio watoto wake kutokana na namna ambavyo alikuwa akiishi na jamii iliyokuwa ikimzunguka.


Aliongeza kuwa hata alipougua kwa mara ya kwanza ni watu wa jirani ambao ndiyo walikuwa wa kwanza kumuhudumia na hivyo wao kama familia walikuja kuungana wakati akiwa hospitali. Hivyo alisisitiza kuwa, ni vema kuishi vizuri na jamii inayokuzunguka.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akitoa neno la pole kwa wafiwa kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipohudhuria mazishi ya Mama Mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mjini Tarime tarehe Mosi June, 2024.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa shukrani kwa niaba ya familia kwa waombolezaji wote walioshiriki katika msiba wa Mama yake mzazi na mazishi yalifanyika tarehe 1 Juni 2024 mjini Tarime.

Waziri Mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa pili kushoto) akishiriki dua ya kumuombea marehemu ambaye ni mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia), dua iliyoongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Mara (hayupo pichani) sheikh Msabaha Kassim Mgabo.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (kushoto) akisalimia na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara alipowasili katika msiba wa mama mzazi wa Jaji Mkuu, ambapo mazishi yake yalifanyika tarehe 1 juni, 2024 mjini Tarime.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwasili msibani nyumbani kwa aliyekuwa Mama Mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alipokuwa akimpokea.

Sehemu ya waombolezaji wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu Tanzania aliohudhuria msiba wa mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania mjini Tarime

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha waombolezaji alipofika msibani kwa ajili ya mazishi ya mama mzazi na Jaji Mkuu wa Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitia ubani na kushiriki kisomo cha dua wakati wa usomaji wa dua ya kumuombea marehemu mama yake iliyofanyika tarehe 1 Juni 2024 mjini Tarime.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma kushiriki kisomo cha dua wakati wa usomaji wa dua ya kumuombea marehemu mama yake dua hiyo iliyofanyika tarehe 1 Juni 2024 mjini Tarime.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Augustine Mwarija akitoa salama za pole kwa wafiwa na waombolezaji wote kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania kwenda kwa familia ya Jaji Mkuu wa Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa salama za pole kwa wafiwa na waombolezaji wote walishiriki mazishi hayo.


Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimwaga mchanga kaburini wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amazishi yaliyofanyika mjini Tarime.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimwaga udongo kaburi wakati wa mazishi ya Mama yake Mzazi aliyefariki tarehe 30 Mei, 2024 na mazishi kufanyika tarehe 01 Juni 2024 mjini Tarime.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni