Na. Francisca Swai-Mahakama, Musoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, amewasisitiza wajumbe wa menejimenti kuwa wabunifu katika kuhakikisha shughuli za Mahakama hazikwami pamoja na kuweka mazingira rafiki ya watumishi kufanya kazi kwa moyo na kujituma.
Mhe. Mtulya alitoa rai hiyo alipokuwa akichambua taarifa mbalimbali za wajumbe wa menejimenti ya Kanda ya Musoma zilizoainisha utendaji kazi kwa robo ya IV ya mwaka 2023/2024 kwenye kikao kiliyofanyika hivi karibuni katika Wilaya ya Bunda.
“Changamoto katika mazingira yetu ni nyingi, ila kama Viongozi tunatakiwa kuwa wabunifu katika kuwapa motisha watumishi na kujenga mazingira rafiki ya kazi ili shughuli mama ya Mahakama isikwame, kwani kazi ndio kitu pekee kilichotukutanisha na kutuunganisha,’’ alisema.
Mhe. Mtulya aliwapongeza wajumbe kwa jitihada walizofanya mwaka 2023 za kuhakikisha Kanda ya Musoma inavuka mwaka bila kuwa na mashauri mlundikano na kusisitiza hatua zianze kuchukuliwa sasa ili kuhakikisha inakuwa desturi yao.
Kupitia kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwasisitiza wajumbe hao kuchukua hatua madhubuti katika kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama, hasa Mahakama za Mwanzo.
Alisisitiza wajumbe kupanda miti kuzunguka maeneo ya Mahakama na kuitunza kwani itakuwa na manufaa hapo baadaye, ikiwemo kutengeza samani mbalimbali za ofisi pamoja na mahitaji mengine kadri itakavyojitokeza.
“Kama Mahakama tumepoteza sehemu kubwa ya ardhi yetu hasa katika maeneo ya Mahakama za Mwanzo. Tujue historia ya maeneo yetu ili tuweze kuyalinda hasa kwa kupanda miti katika mipaka kuzunguka maeneo ya Mahakama,” alisema.
Pamoja na taarifa mbalimbali zilizowasilishwa, mwakilishi wa watumishi Kanda ya Musoma aliyehudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Taifa, lilifonyaka Jijini Dodoma tarehe 16 – 17 Mei, 2024, Bw. Maulid Magoma, alipata wasaa wa kuwasilisha mrejesho wa kilichojiri katika Baraza hilo, ikiwemo majibu ya hoja mbalimbali kutoka katika Kanda ya Musoma.
Kikao hicho kilichoundwa na wajumbe kutoka Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Mahakama za Wilaya za Musoma, Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime na Rorya kiliazimia kutekeleza na kusimamia kwa ukaribu masuala mbalimbali.
Baadhi ya masuala hayo ni kutumia vyema mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama inavyosisitizwa na Viongozi wa juu, kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama, kusikiliza mashauri kwa wakati ili kutovuka mwaka na mlundikano na kutozalisha Mahabusu pasipo sababu za msingi, hasa Mahakama za Mwanzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akitoa maelekezo na kusisitiza jambo wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma kilichofanyika Bunda.
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi akiongea jambo katika kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma kilichofanyika Bunda.
Wajumbe wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma wakifuatilia kwa makini taarifa ya mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma, Bw. Maulid Magoma (aliyesimama) alipokuwa akiiwasilisha kwao taarifa ya yaliyojiri katika Baraza kuu la Wafanyakazi Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni