Ijumaa, 26 Julai 2024

JAJI MKUU WA ZANZIBAR ATEMBELEA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA DODOMA

Aipongeza Mahakama kwa hatua ya maboresho ya miundombinu ya majengo

Na Jeremia Lubango, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla leo tarehe 26 Julai 2024 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kuipongeza Mahakama kwa hatua kubwa iliyopiga kwa upande wa miundombinu.

Jaji Mkuu wa Zanzibar na ujumbe kutoka Mahkama ya Zanzibar walifika Makao Makuu ya Mahakama majira ya saa 3 asubuhi na kupokelewa na Mwenyeji wake Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani pamoja Mkurugenzi Msaidizi wa Utumishi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha.

Baada ya kuwasili katika jengo hilo, Mhe. Abdalla alipata fursa ya kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali za kiutendaji zinazoendelea mahali hapo.

Akiwa ofisini kwa Jaji Kiongozi, Mhe. Abdalla alipata wasaa wa kupokea maelezo mafupi kutoka kwa mwenyeji wake, Mhe. Siyani juu ya namna taratibu za uendeshaji wa shughuli za Mahakama zinavyoendeshwa Makao Makuu.

Baada ya hapo Jaji Mkuu huyo akiwa ameambatana pamoja na baadhi ya Majaji, Watendaji, Wasajili na Maafisa mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Afisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Majengo Mahakama ya Tanzania, Bi. Kailat Bakari walimpitisha maeneo ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama.

Mhe. Abdalla alitembelea ofisi mbalimbali zilizomo katika jengo hilo ikiwemo Ofisi ya Jaji Mkuu, Ofisi ya Msajili Mkuu, Chumba cha Mifumo ya Kutolea Taarifa Muhimu za Mahakama (Judiciary Situation Room), Kumbi za Mahakama (Court Rooms), Ofisi ya Huduma kwa Mteja (Call Centre) pamoja na kujionea miundombinu iliyomo ndani ya jengo hilo.

Alipokuwa Chumba cha Mifumo ya Kutolea Taarifa Muhimu za Mahakama alijionea namna Chumba hicho kinavyofanya kazi  a kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa waliyopiga.

“Nilikuwa naambiwa leo nimejiona kwa macho yangu hakika kwa Afrika ndio Nchi pekee yenye Chumba cha kutolea taarifa muhimu kwa majengo ya Mahakama,” alisema.

Baada ya hapo, Jaji Mkuu huyo alihitimisha ujio wake kwa kutembelea na kujionea nyumba za Majaji zilizojengwa Iyumbu jijini hapa.


Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (katikati) akimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) pindi alipowasili ofisini kwa Jaji Kiongozi tayari kwa kutembelea na kujionea jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania leo tarehe 26 Julai, 2024 jijini Dodoma. 
 
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa pili kushoto) akimsikiliza Afisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Majengo Mahakama ya Tanzania, Bi. Kailat Bakari (mwenye ushungi) wakati alipotembelea kwenye moja ya kumbi za Mahakama zilizopo katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma leo tarehe 26 Julai, 2024. Wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa tatu kushoto ni Jaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, Mhe. Edwin Elias Kakolaki pamoja na Maafisa wengine wa Mahakama. 
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa pili kushoto) akizungumza jambo wakati alipokuwa akipitishwa katika maeneo mbalimbali ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa pamoja na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (kulia) walipokuwa katika moja ya kumbi za Mahakama ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama. Kushoto ni Afisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Majengo Mahakama ya Tanzania, Bi. Kailat Bakari.
Afisa na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA- Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza (kulia) akimuelezea Jaji Mkuu wa Zanzibar namna Chumba maalum cha Kutolea Taarifa za Mahakama kinavyofanya kazi wakati Jaji Mkuu huyo alipotembelea Chumba hicho leo tarehe 26 Julai, 2024.
Jaji Mkuu wa Zanzibar akiwa katika Ofisi ya Huduma kwa Mteja (Call Centre) alipotembelea Ofisi hiyo iliyopo ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania leo tarehe 26 Julai, 2024 jijini Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (aliyenyanyua mkono) akizungumza jambo katika Ofisi ya Huduma kwa Mteja wakati Jaji Mkuu wa Zanzibar alipotembelea Ofisi hiyo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kushoto). Wa pili kulia ni Jaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, Mhe. Edwin Elias Kakolaki, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utumishi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha pamoja na Watumishi wengine wa Mahakama.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) na Jaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, Mhe. Edwin Elias Kakolaki (kulia).

Mkurugenzi Msaidizi wa Utumishi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha (kulia) akimuongoza Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa pili kulia) kutembelea nyumba za Majaji zilizopo Iyumbu jijini Dodoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni