Na INNOCENT KANSHA-Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ametoa rai
kwa Maafisa Mahakama kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na kujituma
kwa bidii wanapohakikisha wanatimiza majukumu yao kwa nafasi wanazozitumikia.
Akizungumza
katika hafla fupi ya kumwapisha Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Sundi Fimbo. Hafla iliyofanyika Mahakama Kuu Masjala Kuu jijini Dar es Salaam,
leo tarehe Mosi Julai, 2024. Mhe. Siyani amesema kuwa, uteuzi huo umezingatia
historia ya utendaji kazi wake na Mahakama ina imani na uwezo wake wa kutenda
kazi kwa nafasi aliyopewa.
“Uteuzi
huu ulizingatia historia ya utendaji kazi wake, nafasi hii ya kuwa Naibu
Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ina majukumu mengi zaidi kuliko
yale ambayo Mhe. Fimbo amekuwa akiyafanya akiwa Kanda ya Dar es salaam na
Divisheni nyingine alizopita kabla ya hapa,” amesema Jaji Kiongozi.
Mhe.
Siyani amesema kuwa, ni nafasi ambayo inahusisha zaidi kupanga mipango
mbalimbali ambayo itasaidia Mahakama Kuu na Mahakama zingine zote zilizopo
chini yake kupiga hatua, siyo kupiga hatua kurudi nyuma ni kupiga hatua kwa kwenda
mbele.
“Nitumie
fursa hii kuwakumbusha Maafisa Mahakama wote kwamba, uteuzi uliofanyika na
teuzi zingine zote zitakazokuja baada ya huu, hazitazingatia mtu ana umri gani
wa kufanya kazi mahakamani.Teuzi zitatazama sana mchango ambao mtu huyo anaweza
kuutoa kwa Mahakama, zitazingatia ni kwa namna gani mtu huyo anaweza kutuunganisha
na kutufanya tusonge mbele,” amesema Jaji Kiongozi.
Aidha,
Mhe. Siyani ameongeza kuwa, zama za kutazama umri wa mtu aliokaa mahakamani ili
kumfikiria kwa nafasi nyingine ni zama zilizopitwa na wakati na amewataka
Maafisa Mahakama na wasio Maafisa Mahakama walielewe jambo hilo ikiwa ni ujumbe
mahususi kwa kila mtumishi.
Jaji
Kiongozi amewataka watumishi wa Mahakama wanaofanya kazi katika maeneo
mbalimbali nchini kutofanya kazi kwa mazoea. Macho ya viongozi yanaweza kuwa
yanawaona watumishi huo lakini hayawasomi, watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa
weledi na ufanisi mkubwa na kwa kupitia njia hiyo ndiyo pekee itakayosaidia
mtumishi kuonekana, amesisitiza Jaji Kiongozi
Jaji
Kiongozi ametoa ushauri kwa Naibu Msajili Mwandamiazi huyo, kwa kumweleza kuwa,
wakati wa kutimiza majukumu yake miongoni mwa mambo mengi ni lazima kuzingatia
vipaumbele na kipaumbele kimoja kikubwa ni kuhakikisha Mahakama hairudi nyuma kwenye
mambo yote ya msingi ya matumizi ya Teknolojia ya Hababri na Mawasiliano
(TEHAMA).
“Ukilala
ukiamuka, ukiota ndoto, ukiweweseka muda wote fikiri na utambue ni namna gani
tutafika kwenye safari tuliyokwisha kuianza ya kuhakikisha huduma za haki
tunazozitoa zinatolewa kwa utaratibu tofauti na ule ambao tumekuwa nao hususani
kupitia matumizi ya TEHAMA,” amesisitiza Jaji Kiongozi.
Jaji
Kiongozi ameongeza kuwa, Mhe. Fimbo atapaswa kushirikiana na Viongozi wengine na
hususani Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri kuhakikisha Mpango Kazi wa Uendeshaji
Mashauri na shughuli nyingine za Mahakama zinaimarika (The Court Busness
Process)
Akimwagia
sifa za kiutendaji Naibu Msajili Mwandamizi mpya huyo, Jaji Kiongozi amesema
kuwa, “nafahamu umekuwa kinara na kiongozi mahiri katika utendaji kazi ukiwa Mahakama
Kuu, Kanda ya Dar es salaam, umefanya kazi vizuri sana na kujitoa kwako ndiyo
kumefanya wengine wakuone...
Usibweteke,
sasa ndiyo wakati wa kuonesha kwamba nilikuwa natumikia eneo dogo la kitaasisi
sasa naweza kufanya zaidi. kajikite katika kutekeleza majukumu yako kwa kushirikiana
na wenzako utakao wakuta katika kutekeleza majukumu hayo na wote watakusaidia.
Usimbague mtu yoyote ushirikiano ndiyo chachu ya mafanikio,”ameongeza Mhe.
Siyani
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam Mhe. Salma Maghimbi
amempongeza Mhe. Sundi Fimbo kwa kuteuliwa katikati ya watu wengi wenye sifa za
kushika nafasi ya Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu.
“Mimi
niliyekuwa nafanya naye kazi naona uteuzi huu ni sahihi kabisa kutokana na
uwezo wake wa kusimamia na kuratibu shughuli zote za uendeshaji wa Mashauri Mahakama
Kuu Kanda na Mahakama zote zilizopo chini ya Kanda yetu ya Dar es salaam, hata
kama angepatikana kwa kupiga kura ningepiga kura mara nyingi iwezekanavyo ili
apatikane yeye,” amesema Mhe. Maghimbi.
Mhe.
Maghimbi akawakumbusha Maafisa Mahakama wote kufanya kazi kwa bidii kwa sababu mtu
anapofanya kazi juhudi zake zile anazozifanya zinakuwa zinaonekana na
hazijifichi. Kwa sasa Mpango Kazi wa Mahakama upo katika kipindi cha mpito
kutoka kwenye karatasi ngumu kwenye kidijiti.
Kitu cha muhimu kuliko vyote ni kupokea hayo mageuzi na kuyakumbatia kwa kuyafanyia kazi ili yawe sehemu ya maisha kazini, Maafisa Mahakama wote tukiweza kufanya hilo basi tutaweza kufanya kazi kwa urahisi zaidi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) akimwapisha Mhe. Sundi Fimbo (aliyeshika Biblia) kuwa Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Hafla hiyo iliyofanyika Mahakama Kuu Masjala Kuu jijini Dar es Salaam, leo tarehe Mosi Julai, 2024.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (aliyekaa mbele) akitoa neno mara baada ya uapisho huo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akizungumza na viongozi waandamizi mbalimbali wa Mahakama (hawapo pichani) waliohudhuria hafla hiyo ya uapisho ofisini kwake jijini Dar es salaam mara baada ya uapisho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam Mhe. Salma Maghimbi akitoa neno wakati wa hafla ya uapisho.
Sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria katika hafla fupi ya kumwapisha Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Mhe. Sundi Fimbo (wa kwanza kulia).
Sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria katika hafla fupi ya kumwapisha Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Mhe. Sundi Fimbo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni