Jumanne, 23 Julai 2024

MAHAKAMA NJOMBE YAVUKA MWAKA BILA MASHAURI MLUNDIKANAO

Na Innocent Kansha-Mahakama, Njombe

Mahakama mkoani Njombe ilivuka mwaka 2023 ikiwa na mashauri sifuri ya mlundikano na kufikia Disemba 2023, mashauri yaliyobaki yalikuwa 522 na hivyo kufikia lengo la kuondosha mashauri ya muda mrefu mahakamani.

Akiongea na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania leo tarehe 23 Julai, 2024 Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe Bw. Richard Mbambe amesema, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilibakiwa na mashauri 19 Disemba, 2023, huku Mahakama za Wilaya zilibakiwa na mashauri 207 na Mahakama za Mwanzo mashauri 296.

“Mahauri yaliyofunguliwa kuanzia Januari 2024 hadi Juni 2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi ilipokea mashauri 27, Mahakama za Wilaya mashauri 201 na Mahakama za Mwanzo mashauri 1132 takimu hizo zinafanya jumla ya mashauri yamefikia takribani 1360,” amesema Mtendaji Bw. Mbambe.

Bw. Mbambe amesema, mashauri yaliyosikilizwa kunzia Januari, 2024 hadi Juni, 2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi imesikiliza mashauri 30, wakati Mahakama za Wilaya zimesikiliza mashauri 348 na Mahakama za Mwanzo zimesikiliza mashauri 900 na kufanya jumla ya mashauri 1278.

Mashauri yaliyobakia kufikia Juni, 2024 kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ni mashauri 16, Mahakama za Wilaya ni mashauri 60 na Mahakama za Mwanzo ni mashauri 528 na kufanya jumla ya mashauri yaliyobaki kufikia 604, amesema Mtendaji huyo.

Kwa upande wa mashauri yaliyoendeshwa kwa njia ya Mahakama Mtandao (video Conference) ni mashauri 12 kunzia Januari hadi Juni, 2024 mashauri yaliyosikilizwa Mahakama ya Hakimu Njombe ambayo hayakusajili wa Njombe ni mashauri manne (4) kutoka Mtwara shauri moja (1), Kigoma moja (1) na Iringa mashauri mawili (2) hii inatokana na uimarishaji wa matumizi ya mifumo ya kuendeshea mashauri kwa njia ya mtandao.

Bw. Mbambe amesema, Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe hupokea wastani wa wateja 668 kwa mwezi, ikiwa ni sawa na wastani wa wateja 167 kwa wiki wanaofika mahakamani hapo kupata huduma mbalimbali za utoaji haki. Vilevile malalamiko yaliyowasilishwa na wateja kwa mwaka 2023 yalikuwa saba (7) na Mwaka 2024 kuanzia Januari hadi Juni 2024 Mahakama imepokea malalamiko mawili (2) na tayari uongozi umeshayashughulikiwa.

Akielezea maendeleo ya miradi ya ujenzi inayotekelezwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania, Bw. Mbambe amesema Mahakama kwa sasa inatekeleza miradi miradi mitatu (3) ya ujenzi, ikiwemo ujenzi wa  Mahakama Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Njombe ambao ujenzi wake umefikia asilimia 21, ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Lupembe na Mahakama ya Mwanzo Manda.

Ujenzi wa Kituo Jumuishi Njombe ulianza tarehe 12 Disemba, 2023 na unatarajiwa kukamilika tarehe 11 September, 2024. Mradi huu unatarajiwa kugharimu Tshs. 7,647,179,528.62/= (VAT). Mkandarasi anayejenga mradi huu ni Shandon Hi – Speed Dejian Group chini ya usimamiziwa mkandarasi Mshauri (Consultant) Crystal Consultant.

Aidha, mradi upo katika hatua ya ukamilishaji wa sakafu ya ghorofa ya kwanza (first floor slab concrete) hivyo kufanya asilimia ya utekelezaji wa mradi kuwa asilimia 21.

Mtendaji huyo ameongeza kuwa, mradi huo ukikamilika utasaidia kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi badala ya kusafiri kufuata huduma za Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa kama ilivyo sasa, pia itapunguza gharama za kuleta Waheshimiwa Majaji toka Mahakama Kuu vilevile itapunguza mlundikano wa mshauri, itawasaidia wananchi kutumia muda wao katika uzalishaji mali na kujiongezea kipato na kurahisiha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Mkoa wa Njombe una idadi ya wakazi wapatao 889,946 ambao watanufaika na ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kitakapo kamilika na kuanza kutumika kutoa huduma za haki mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa takwimu Mkoa wa Njombe una Mahakama ya Hakimu Mkazi 1, Mahakama za Wilaya nne (4) na Mahakama za Mwanzo 26 kama inavyobainishwa hapo chini.

Wilaya ya Njombe ina Mahakama moja ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo saba (7), ambazo ni Njombe mjini, Makambako, Lupembe, Matola, Igominyi, Mtwango na Uwemba/Mahenye.

Wilaya ya Ludewa inayo Mahakama ya Wilaya moja na Mahakama za Mwanzo saba (7), ambazo ni Ludewa mjini, Mlangali, Mawengi, Lugarawa, Mavanga na Manda/Masasi na Luilo.

Wilaya ya Makete ina Mahakama ya Wilaya moja ambayo mashauri yake hufanyika katika jengo la Mahakama ya Mwanzo Makete mjini. Aidha, kuna Mahakama za Mwanzo nane (8) ambazo ni Makete mjini, Bulongwa, Matamba, Lupalilo, Lupila, Ukwama, Mfumbi na Ipelele.

Wilaya ya Wanging’ombe ina Mahakama ya Wilaya moja, aidha Wilaya ya Wanging’ombe inazo Mahakama nne (4) za Mwanzo ambazo ni Wanging’ombe, Mdandu, Kipengere na Imalinyi.











 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni