Jumatano, 3 Julai 2024

UJENZI WA MAHAKAMA KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIUCHUMI

Na TAWANI SALUM-Mahakama, Mpwapwa Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel juzi tarehe 1 Julai, 2024 alikabidhi kwa Mkandalsi Audax eneo itakapojengwa Mahakama ya Mwanzo  Kinusi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Ole Gabriel aliomba ushirikiano na Ofisi ya Kata ya Ibela ambapo Kijiji cha Kinusi kinapatikana kuhakikisha ujenzi wa Mahakama hiyo unakamilika, hivyo kukamilisha ndoto ya wanakijiji wa  Kinusi.

Vilevile, Mtendaji Mkuu aliielekeza Kampuni ya OGM iliyo chini ya Mshauri Elekezi, Bw. Robert Modu, kusimamia utekelezaji wa mradi huo. 

“Nisingependa kuona mradi huu unafanyika chini ya kiwango, naomba kama kutakuwa na changamoto yoyote tujulishane kwa haraka ili kutimiza malengo na matarajio ya wanakijiji wa Kinusi,” alisema.

Mtendaji Mkuu alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bunge la Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri wa Fedha, Dkt.  Mwigulu Nchemba  kwa kutoa fedha ili ujenzi wa Mahakama hiyo uweze kufanyika na kukamilika kwa wakati.

“Nataka mwezi March, 2025 ujenzi huu uwe umekamilika,ni mategemeo yangu mradi huu utakamilika kama tulivyokubaliana, wanakijiji wa  Kinusi naomba  tumpe Mkandalasi ushirikiano ili kuweza kumaliza mradi huu kwa muda tuliokubaliana,” alisema.

Akizungumza katika  hafla hiyo,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene alisema historia inaonyesha kuwa kabla ya uhuru sehemu hiyo kulikuwa na Mahakama ila baadae ikaondolewa.

“Mmechagua mahala sahihi, naomba sana kumshukuru Rais Samia kwani ndiye aliyetoa fedha hizi nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama yetu, tutahakikisha tunatunza na kushirikiana na Mkandarasi kuepusha wizi, hasa simenti na nondo. Nikuhakikishie Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa waanakijiji wa Kinusi ni waaminifu na waungwana.

‘’Mahakama hii itasaidia sana kuendeleza zoezi zima la utoaji haki na hivyo kuchochea maendeleao katika kijiji hiki,’’ alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Ipela, Bw. Feston Muyugule alisema kuwa wanakijiji wa Kinusi walikuwa wanaenda umbali mrefu kama wilayani Mpwapwa, takribani kilomita 120, kwenda kijiji cha Kibakwe kilomita 60 na kijiji cha Chipogolo kilomita 80 kwa ajili ya kwenda kutafuta haki.

Alisema kuwa hali hiyo inaitesa wanakijiji wa Kisusi, hivyo kujengwa kwa Mahakama hiyo ni kuwaletea neema na kutatua changamoto zilizokuwapo katika zoezi zima la utoaji haki.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata, Bi. Joyce Mwakyusa alisema kuwa walikuwa wanaelemewa na mzigo mzito katika suala zima la utoaji haki kwa kuwa haki ilikuwa inapatikana mbali na walikuwa kwenye wakati mgumu wa kutatua kero za migogoro ya ndoa, ardhi, ugomvi pamoja wizi na walitumia muda mwingi kutatua changamoto hizo badala ya kufanya shughuli za kimaendeleo.

Alisema kuwa ujio wa Mahakama hiyo utawapunguzia mzigo mzito wananchi uliokuwa unawaelemea na kujikita katika zoezi zima la kuwaletea maendeleo wanakijiji wa Kinusi.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa nne kutoka kushoto), akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenit ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe.George Simbachawene (wa tano kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wanakijiji cha Kinusi katika khafla ya kukabidhi eneo la ujenzi iliyofanyika Kinusi Ipera Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma.

 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyeshika nyaraka)akiangalia mchoro ambao utajengwa Mahakama ya Mwanzo Kinusi.

 Mchoro unaonesha jinsi Mahakama ya Mwanzo Kinusi itakavyokuwa.


 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na Waziri wa Nchi Ofisi ya Raii Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (wa kwanza kutoka kulia) wakiteta jambo kuhusu mradi huo.

 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tatu kutoka kulia) akikagua eneo ambalo Mahakama ya Mwanzo Kinusi itajengwa.

 

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Moses Lwiva (wa nne kutoka kushoto) akijadili jambo na Maafisa wa Mahakama.

 

Waliochuchumaa wa kwanza kulia ni Waziri na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (kushoto wa kwanza) ni Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wakiwa wakioneshana kiwanja pamoja wananchi na watumishi wa Mahakama walioudhuria hafla hiyo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni