Jumatano, 3 Julai 2024

JAJI MTULYA AWAAPISHA WAJUMBE WA KAMATI ZA MAADILI YA MAAFISA MAHAKAMA


·       Waelezwa majukumu yao

Na FRANCISCA SWAI, Mahakama – Musoma

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewaapisha Wajumbe wa Kamati za  Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya katika Mkoa wa Mara na kuwataka kuzingatia viapo vyao.

Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya walioapishwa jana tarehe 2 Julai, 2024 ni Wakuu wa wilaya za Musoma, Bunda, Tarime na Rorya  ambao ni Wenyeviti wa kamati hizo pamoja na Makatibu Tawala wa wilaya hizo ambao ni Makatibu wa Kamati hizo. Aidha, wajumbe wengine wa Kamati hizo pia waliapishwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mtulya alisema kamati hizo zipo kwa mujibu wa sheria hivyo aliwataka wajumbe hao kuzingatia maadili ya viapo vyao na kutekeleza jukumu hilo la Kisheria kwa usiri na weledi mkubwa.

‘‘Sheria ya mienendo ya maadili ya Mahakimu inaeleza kwa undani hakimu aweje, aishije na namna ya kufanya kazi zake. Pale anapovunja sheria hizi au kukosea katika mwenendo wake ndipo kamati zenu zinafanya kazi,’’ alisema Mtulya.

Mhe.  Mtulya aliwaasa wajumbe kuwa kazi zao si ndogo bali ni kubwa kwani wanatekeleza jukumu la kikatiba na kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji kamati hizi zinahusisha wajumbe wa namna mbalimbali ikiwemo wananchi wa kawaida, viongozi wa dini na viongozi wa kiserikali.

Aidha, Mhe. Mtulya amesisitiza wajumbe katika kutekeleza majukumu yao wakumbuke kuwa hawatekelezi majukumu hayo kwa vyeo vyao bali kama wawakilishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Katika zoezi hilo, wajumbe na viongozi wa kamati hizo walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kupewa ufafanuzi wa maswali yao. Pia walipewa elimu juu ya sheria mbalimbali zinazoelezea uwepo wa kamati hizo, namna wanavyoteuliwa, kazi za kamati husika, majukumu ya kila mjumbe katika kamati hizo pamoja na kuapa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na weledi.

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

     

Mtendaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi (aliyesimama), akiwakaribisha wajumbe katika hafla fupi ya uapisho wa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya, Kanda ya Musoma.

Mkuu wa Wilaya Musoma, Dkt. Khalfan Haule (aliyesimama), akiwatambulisha wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama wilaya ya Musoma katika Hafla fupi ya uapisho wa wajumbe hao uliofanyika Mahakama Kuu Musoma.

 Mkuu wa Wilaya Rorya, Bw. Juma Chikoka (aliyesimama), akiwatambulisha wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Rorya katika hafla fupi ya uapisho wa Wajumbe hao uliofanyika Mahakama Kuu Musoma.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama) akisema neno la utangulizi kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika hafla fupi ya uapisho wao uliofanyika Mahakama Kuu Musoma.

 Katibu Tawala Wilaya ya Tarime Bw. Saul Mwaisenye (aliyesimama), akiuliza swali wakati wa hafla fupi ya uapisho wa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Wilaya, Kanda ya Musoma uliofanyika Mahakama Kuu Musoma.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya Kanda ya Musoma.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya  Musoma Mhe. Salome Mshasha (aliyesimama), akifafanua jambo lililoulizwa na wajumbe katika hafla fupi ya uapisho wa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya, Kanda ya Musoma uliofanyika Mahakama Kuu Musoma.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (mbele) akitoa elimu juu ya Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwa  wajumbe wa kamati hizo ngazi ya Wilaya, Kanda ya Musoma.

Picha ya juu na chini ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (mbele) akiwaapisha wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya, Kanda ya Musoma.



 

(Imehaririwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama) 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni