Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Wanafunzi 54 wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Matsapa iliyopo Wilaya ya Ubungo inayofundisha kwa lugha ya Kiingeleza leo tarehe 12 Julai, 2024 wametembelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kujifunza mambo mbalimbali ya kisheria na utoaji haki.
Wakiwa wemeongozana na Walimu sita, Wanafunzi hao waliwasili katika jengo la Mahakama hiyo majira ya saa 3.00 asubuhi na kupokelewa na Afisa Utumishi, Bi. Winnie Shirima na kupelekwa kwenye Ukumbi wa Chumba cha Habari NMB.
Baada ya mapumziko mafupi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi alikutana na Wanafunzi hao na kuwapa maelezo kadhaa kuhusu Mahakama ya Tanzania, kama moja ya Mihimili inayounda Dola hapa nchini, kabla ya kuanza ziara yao.
Maeneo waliyotaka kujua ili kuwawezesha Wanafunzi hao kujifunza na kupata umahiri katika uhalisia baada ya nadharia ya darasani ni muundo wa Mahakama ya Tanzania, aina mbalimbali za mashauri na Mahakama zenye mamlaka ya kuyasikiliza na Viongozi wanaohusika na usikilizaji wa mashauri mbalimbali kulingana na uzito.
Akizungumza na Wanafunzi hao, Mhe. Maghimbi aliwaeleza jinsi Mahakama ilivyoanzishwa kwa mujibu wa Katiba, ngazi za Mahakama zilizopo kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani na namna mwananchi anavyopata haki kwa njia ya kusikiliza, rufaa, marejeo na mapitio.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa Mahakama hutekeleza majukumu yake kwa uhuru bila kuingiliwa na Mihimili mingine ya Dola kama Serikali na Bunge na kwamba uhuru huo unapenya hata ndani ya Mahakama yenyewe kwa Majaji na Mahakimu kuamua mashauri bila kupokea maelekezo kwa mtu yoyote.
Kadhalika, Mhe. Maghimbi aliwaeleza Wanafunzi hao kuwa kwa sasa Mahakama inaendesha shughuli zake kwa njia ya mtandao na kwamba usajili wa mashauri yote unafanyika kwa njia ya mtandao, hivyo akawahimiza kujikita kwenye teknolojia wakati wa masomo yao ili wasije wakaachwa na utandawazi.
Amewaeleza pia kuwa Viongozi wa Mahakama, kama Jaji Mkuu, Majaji, Mtendaji Mkuu, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu huteuliwa na Rais na kwamba Mahakimu huajiriwa kama watumishi wengine baada ya kupita kwenye mchakato wa ajira.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni