Jumatatu, 19 Agosti 2024

JAJI MAGHIMBI AWAAPISHA WAJUMBE WA KAMATI YA MAADILI WILAYA YA KIBAHA

 ·       Asema Kamati Hizo ni Jicho la Tume

 Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amesema Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ni jicho la Tume ya Utumishi wa Mahakama katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha maadili ya utumishi wa Mahakama ili kuufanya utumishi katika Mhimili huo uwe wenye kuheshimika, uadilifu, weledi na uwajibikaji.

Jaji Maghimbi ameyasema hayo tarehe 17 Agosti, 2024 wakati akiwaapisha wajumbe wanne wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha ambapo pia alizipongeza Kamati za Mkoa wa Pwani pamoja na Wilaya zake kwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake.

 “Kipekee nawashukuru na ninawapongeza wajumbe wote kwa kuaminiwa na kupewa jukumu la kushiriki katika kuhakikisha Maafisa Mahakama wanafanya kazi kwa uadilifu, sio jukumu dogo kwa sababu unahusika na kutoa uamuzi, ni kazi kidogo nzito ndio maana nawapongeza,” alisema Jaji Maghimbi.

 Alisema kuwa Kamati zimepewa wajibu wa kisheria wa kuishauri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhusu uzingatiaji wa Maadili ya utumishi kwa Maafisa Mahakama ili watoe huduma bora kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi aliwakumbusha wajumbe hao kutokasimisha majukumu yake kwa chombo, mamlaka au mtu mwingine yeyote kwa kuwa Kamati inao wajibu wa kuendesha vikao vyake, kutoa na kupokea taarifa na kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi ya Mahakimu.

Aidha, Mhe. Maghimbi alisema Mahakama imedhamiria kwa dhati kusimamia kwa uzito suala la maadili pamoja na kuhakikisha kwamba wanachukua hatua stahiki za uwajibikaji dhidi ya Maafisa wake wanaotuhumiwa kukiuka maadili na kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa.

Jaji Maghimbi alisema Mahakama haiwezi kuonekana kuwa huru na inayotenda haki endapo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa maadili, hivyo Kamati za Maadili ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama unaolenga kuhakikisha kuwa Mahakama inaendelea kuaminiwa na wananchi kama sehemu ya kupata haki kwa wakati, kwa weledi isiyoambatana na vitendo vya uvunjifu wa maadili.

Wajumbe walioapishwa ni pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Charles Lukumai, Hakimu Mkazi wa Mahakama Wilaya Ubungo, Mhe.  Subilaga Wilson Mwakalobo, Mwl. Joyce Francis Shauri na Shekh Amini Kondo Matambo.

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inahusisha wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzani Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya Kibaha mara baada ya kuwaapisha.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati), kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Nickson Simon, kushoto ni Katibu wa Kamati hiyo ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Ndg. Moses Magogwa pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo. Wengine ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka.

Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya Wilaya Kibaha. Kutoka kushoto ni Mhe. Emmael Lukumai, Mhe. Subilaga Mwakalobo, Mwl. Joyce Shauri na Shekh Amin Matambo.

(Imehaririwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni