Alhamisi, 15 Agosti 2024

MTENDAJI MKUU ATEMBELEA UJENZI WA KITUO JUMUISHI NJOMBE

Na ABDALLAH SALUM-Mahakama, Njombe

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel juzi tarehe 13 Agosti, 2024 alitembelea ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Njombe ili kujionea maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2024.

Kabla ya kwenda kwenye eneo la mradi, Prof. Ole Gabriel alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka na kumweleza azma ya ziara yake.

Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mtendaji Mkuu alimfahamisha kuhusu Vituo Jumuishi nane vinavyojengwa katika Mikoa mbalimbali nchini kwa ufadhili wa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.

“Serikali imekopa fedha nyingi sana kwa ajiri ya ujenzi huu, ukiwemo Mkoa wa Njombe ambao nao umebahatika kupata ufadhili huo,” alisema.

Mkuu wa Mkoa alielezea shukurani zake kwa uamuzi wa Mahakama kujenga Kituo hicho kwani Mkoa wa Njombe haujawahi kuwa na Mahakama Kuu, hivyo pindi mradi huo utakapokamilika utaufanya kuwa na jengo la kisasa la Kituo Jumuhishi. 

Baada ya hapo, Mtendaji Mkuu alielekea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na kusalimiana na watumishi na baadaye kuongea na Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Liadi Chamshama na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Richard Mbambe.

Prof. Ole Gabriel alieleza matumaini yake kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Kituo hicho utaleta manufaa makubwa kwa kusogeza huduma za Mahakama Kuu na utoaji haki kwa ujumla kwa wananchi wa Mkoa huo.


Mwonekano wa ujenzi wa Kituo Jumuishi Njombe.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa miwani nyeusi) akionyesha jinsi jengo lilipofikia.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati aliyevaa miwani) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka. AnayefUata ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama na wa nne kutoka kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe (wengine hawapo katika picha) pamoja na baadhi ya Wakandarasi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi Njombe.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe akielezea ujenzi wa Kituo hicho, pembeni yake ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama na aliyekaa Meza Kuu ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwaagaViongozi baada ya ziara yake.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Maoni 1 :