Jumatano, 14 Agosti 2024

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA ATEMBELEA UJENZI WA KITUO JUMUISHI SONGWE

Na. IMAN MZUMBWE-Mahakama, Songwe

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel juzi tarehe 12 Agosti,2024 alitembelea ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Songwe ili kujionea maendeleo ya mradi huo.

Katika ziara hiyo, Prof. Ole Gabriel alipokelewa na mwenyeji wake, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Bw. Sosteness Mayoka na baadaye kumtambulishwa kwa watumishi.

Mtendaji Mkuu alifurahishwa na mapokezi hayo kisha akawasihi watumishi hao waendelee kuwa na umoja katika kazi ili kufanikisha malengo ya Taasisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mara baada ya utambulisho huo, Prof Ole Gabriel alifanya kikao kifupi na Mtendaji wa Mahakama Songwe, ambapo alipokea taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Kituo Jumuishi Songwe.

Baadaye alielekea kwenye mradi huo na kupokelewa na Mkandarasi kutoka Kampuni ya M/S Home Africa Investment Cooperation Limited ambaye alimweleza taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi.

Prof Ole Gabriel aliapata wasaa wa kuzungumza na wafanyakazi na vibarua wanaosaidia ujenzi, aliwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya licha ya kuwepo kwa changamoto  ambazo zinawakabili.

 Mtendaji Mkuu alimtaka Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili mradi umalizike kwa wakati. Kadhalika, alimhimiza kuongeza vitendea kazi na  idadi ya wafanyakazi ambao watawesha kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi kwa wakati.

Prof. Ole Gabriel alimweleza Mkandarasi huyo kuwa hatasita kumchukulia mtu yeyote hatua za kisheria pale ambapo hatatekeleza kandarasi kulingana na mkataba.

Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu aliambatana na baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Songwe na Katibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na watumishi alipowasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu cha wageni alipofika katika Ofisi ya Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Bw. Sosteness Mayoka akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo Jumuishi Songwe.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Mkandarasi pamoja timu nzima ya ujenzi wa Kituo hicho.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na timu ya ujenzi wa mradi wakielekea kutazama maendeleo ujenzi ulipofikia.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na baadhi ya wafanyakazia na vibarua katika mradi huo.

Mwonekano wa mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi Songwe.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni