Ijumaa, 23 Agosti 2024

UONGOZI BORA WA MAHAKAMA UNAVYOING’ARISHA TANZANIA KIKANDA, KIMATAIFA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete ameipongeza Mahakama ya Tanzania chini ya Uongozi wa Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa jitihada zinazofanywa kuimarisha mfumo wa haki nchini kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo utatuzi wa migogoro ya kazi. 

Mhe. Kikwete ametoa pongezi hizo jana tarehe 22 Agosti, 2024 katika Ukumbi wa PSSF Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa anafunga mkutano wa nane wa kamati ya utatu wa wadau wa haki kazi ambao uliandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.

“Naupongeza sana Uongozi wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma, kwa kuhakikisha haki inatendeka kwa uwazi na uadilifu. Mafanikio haya ni ya kujivunia na yanaonesha dhahiri kuwa Tanzania inaheshimu na kutekeleza maazimio ya kimataifa kwa manufaa ya raia wake,” alisema.

Waziri Kikwete alibainisha kuwa mafanikio yanayoonekana ndani ya Mahakama ya Tanzania yasingefikiwa bila ushauri na usaidizi mzuri unaotolewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani kwa Jaji Mkuu, kwani mchango wake umeleta mabadiliko chanya na ishara ya uongozi bora wa kuigwa. 

“Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuimarisha mfumo wa sheria na haki nchini. Ushirikiano wenu umewezesha Mahakama ya Tanzania kufanikisha hatua muhimu, ambazo zimeifanya nchi yetu kuendelea kuwa mfano bora katika kanda yetu na hata kimataifa,” alisema.

Mhe. Kikwete alieleza kuwa mafanikio ya Mahakama yanapotambuliwa nje ya mipaka, si tu ni sifa kwa Mahakama ya Tanzania, bali pia sifa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alibainisha kuwa Rais Samia amekuwa kiongozi wa mfano katika kusimamia haki, demokrasia na utawala wa sheria na mafanikio yanayoonekana mahakamani ni sehemu ya maono yake kuwa Tanzania inasonga mbele katika utoaji haki, uwazi na usawa. 

Akizungumzia kauli mbiu ya mkutano huo inayosema, “Wajibu wa Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo wa Haki kazi kwa Ustawi wa Taifa,” Waziri Kikwete alieleza kuwa mchakato wa utatu una nafasi ya kipekee katika kusimamia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. 

“Napenda kusisitiza kuwa, mjadala na maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano huu ni muhimu sana, lakini utekelezaji wake ndio utakaoleta tofauti. Ni wakati sasa wa kuchukua hatua na mapendekezo tuliyoyatoa yanatekelezwa kwa vitendo. Wizara itasimama kidete kuhakikisha yote tuliyokubaliana yanapata utekelezaji unaostahili,” alisema.

Mhe. Kikwete alieleza zaidi kuwa Wizara yake inayohusika na masuala ya kazi, itaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yatakayoletwa mbele yake na kuweka misingi bora ya sheria za kazi zinazoendana na kasi ya maendeleo ya kidunia. 

“Niwaahidi kwamba kamwe Wizara haitawaangusha. Aidha, uimarishwaji wa sheria bora ni msingi wa ukuaji wa sekta ya ajira na kazi hapa nchini, ambapo huchochea mazingira bora ya uwekezaji na ustawi wa jamii yetu. Naomba tuendelee kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunaijenga nchi yetu kwa pamoja,” alisema.

Awali, akizungumza wakati akimkaribisha Waziri kufungua mkutano huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina, alisema kuwa mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wadau wote wa utatu, yaani Serikali, Waajiri na Chama cha Wafanyakazi umekuwa wa ufanisi mkubwa.

Alieleza kuwa wakati wa mkutano kuna mengi yalijadiliwa, hususani ushirikiano wa Taasisi za kikazi katika kutatua migogoro ya kazi, umuhimu wa elimu kwa watatuzi wa migogoro ya kazi pamoja na ushiriki wa Taasisi za kazi katika mikutano ya kimataifa.

Katika mkutano huo, mada mbalimbali ziliwasilishwa, ikiwemo nafasi ya wadau katika kuboresha mfumo wa haki kazi kwa ustawi wa Taifa, wajibu wa Mahakama katika kuboresha mfumo wa haki kazi na saikolojia katika utatuzi wa migogoro ya kazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anazungumza kwenye hafla fupi ya kufunga mkutano wa nane wa kamati ya utatu wa wadau wa haki kazi ambao uliandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi jana tarehe 22 Agosti, 2024 jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya wajumbe wa mkutano (juu na chini) wakifiuatilia mambo mbalkimbali yaliyokuwa yanajiri.


Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi (juu na chini) wakiwa kwenye mkutano huo.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria mkutano huo. Aliyesimama kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Edson Mkasimongwa.

Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa haki kazi (juu na chini) waliohudhuria mkutano huo.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni