Jumanne, 20 Agosti 2024

TEKNOLOJIA KUTUMIKA KUBORESHA HUDUMA KWENYE KITUO CHA USULUHISHI MAHAKAMA KUU YA TANZANIA

Na SALUM TAWANI-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi ipo mbioni kuboresha huduma zake na kuwafikia wateja wake wenye uhitaji maalum  ya kusikia kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwasaidia kutatua migogoro mbalimbali inayowakabili na kupata haki zao walizozikatia tamaa.

Uongozi wa Kituo cha Usuluhishi unaongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Zahra Maruma, hivi karibuni ulikutana na Msuluhishi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi isiyo ya Kiserikali iitwayo ESS Creative Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza kujadili mambo mbalimbali. 

Taasisi hiyo imesajiliwa chini ya Wizara ya Sheria na Katiba inayojishughulisha na utatuzi wa migogoro kwa wenye uhitaji maalum kwa kutumia Teknolojia kupitia programu inayojulikana kama “Empowering Deaf and Hard of Hearing Women in Tanzania”.

Akizungumza katika majadiliano ya kuboresha huduma za Kituo hicho, Mhe.  Maruma alisema kuwa amefurahia ujio wa Mgeni huyo ambaye amepata utaalam kutoka nchini Marekani ambapo shughuli hizo za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa watu wenye mahitaji maalum ya kusikia hufanyika kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia Teknolojia.

‘’Tupo tayari kuanza kutumia teknolojia ili iweze kutusaidia katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi, hasa kwa wadaawa wenye uhitaji maalumu kama hili la wenzetu wenye uziwi au usikivu hafifu. Katika maeneo ya uwezeshaji upatikanaji haki, eneo hili la mawasiliano ni muhimu na kwa upande wa wale wenye changamoto za kusikia  wamekuwa wakikumbana na ugumu wa mawasiliano katika kuwasilisha hoja na madai yao pale wanapohitaji huduma za haki.  

“Mara zote wamekuwa wakitegemea uwepo wa wataalamu wa lugha za alama katika kufanikisha mawasiliano. Teknolojia hii inayotumika ni nyezo ambayo itatusaidia sana katika utoaji wa haki kwa wakati na haraka kwa watu wenye uhitaji maalum, sio tu katika Kituo chetu bali pia Mahakama kwa ujumla,” alisema.

Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa kuna baadhi ya mashauri yanayoendeshwa yanahusisha watu wenye mahitaji maalumu, hivyo kwa kutumia teknolojia itasaidia kuokoa gharama zinazotumika kuwalipa Wakalimani wa lugha ya alama ambazo wakati mwingine zipo juu na upatikanaji wa wataalam hao ambao wapo wachache wakati mwingine huwa ni changangamoto. 

Alisema kuwa matumizi ya Technolojia yatasaidia kuleta uwazi wa mawasiliano na kujenga uaminifu kwa Mahakama kwa kuwa watu wenye uhitaji maalumu katika kusikia, watakuwa na uhakika na usahihi wa wanachokieleza wao na kinachoelezwa na upande wa pili kwa kuwa Technolojia hiyo ambayo ina uwezo wa kubadili sauti kwenda katika maaandishi na maandishi kwenda katika sauti.  

“Matumizi ya Teknolojia yatapunguza gharama zinazotumika katika upatikanaji wa wataalamu na pia muda wa kusubiria wataalamu hao. Badala yake gharama hizo zitaelekezwa kwenye shughuli nyingine za ujenzi wa Taifa,’’ alisema Jaji Maruma.

Jaji Mfawidhi alitanabaisha kuwa kwa kuzingatia Mahakama ya Tanzania ndio kinara katika matumizi ya teknolojia, ujio wa teknoljia hiyo ni kitu kizuri na watakipeleka kwenye Uongozi wa Juu wa Mahakama ya Tanzania ili kuweza kulijadili jambo hilo liweze kuwasaidia Majaji na Mahakimu katika utendaji wa kazi za kila siku pale wanapokutana wadau wenye tatizo la kusikia na hatimaye kufikia dhima na dira ambayo Mahakama ya Tanzania imejiwekea ya utoaji wa haki kwa wakati.

‘’Nikushukuru kwa kujitoa kwenda Wizara ya Katiba na Sheria ambapo ni seheme sahihi ya jambo hili la usuluhishi na hatimaye kuleta huu utaalam hapa Mahakama ya Tanzania kwenye Kituo mahususi kinachoshughulikia utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, ni watu wachache wanaoweza kuwa na utaalam wa namna hii kujaribu kuleta katika chombo husika ili kiweze kuboresha huduma zake kwa kiwango cha juu,’’ alisitiza.

Naye Jaji Angela Bahati, kwa upande wake alimpongeza Bw. Mukiza kwa kuleta wazo hilo na kusema kuwa wapo tayari kushirikiana naye kuhakikisha linafanikiwa kwa kiwango cha juu ili kusaidia katika utendaji mzuri wa kazi, sio tu kwenye Kituo cha Usuluhishi, bali pia kwa Mahakama kwa ujumla na hivyo kurahisisha utoaji wa haki kwa haraka na wakati ambalo ndio lengo kuu la Mahakama ya Tanzania.

Kwa upande wake, Jaji Arufani Kweka alisema wazo hilo ni kitu kizuri chenye manufaa ambacho kitaleta athari chanya kwenye utatuzi wa migogoro kwa wenye uhitaji maalum. 

Alisema kuwa teknolojia hiyo ni ukombozi sio tu kwa Kituo cha Usuluhishi bali pia kwa Mahakama zingine zitasaidia kusukuma mashauri kuisha kwa wakati na haraka, hivyo kurahisisha zoezi zima la utoaji haki na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika Taifa.

Mhe. Kweka alieleza pia kuwa ujio wa teknolojia hiyo inatuonyesha kuwa kuna watu wenye mahitaji maalum walikuwa wanakosa haki zao kwa hofu tu jinsi gani wanaweza kusikilizwa ama kumlipa Mkalimani ili aweze kupata haki yake.

“Hii ilikuwa ni changamoto ambayo iliwafanya kukata tamaa jinsi ya kupata haki kutokana na migogoro iliyokuwa inawakabili. Ujio wa teknolojia hii utarejesha imani, kuwa sasa watakuwa katika wakati mzuri wa kupata haki zao kwa kuwa teknolojia hii haina gharama na itawawezesha wao kujua nini wanahitajika kufanya na wao kueleweka nini wanahitaji,’’ alisema Jaji Arufani. 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mbando alimshukuru Bw. Mukiza kwa kuleta utaalam huo ambao utasaidia katika kupunguza mlundikano wa mashauri ndani ya Mahakama ya Tanzania kwa kuwa sasa hakutohitajika tena wakalimani ambao ni wachache na gharama zao zipo juu  ili kuweza kuwapata.

Akizungumza kwenye majadiliano hayo, Bw. Mukiza alisema utaalam wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa kutumia teknolojia ameupata huko nchini Marekani alikokwenda kusoma na kujionea shughuli zinavyofanyika za usuluhishi kwa watu wenye uhitaji maalum unavyofanyika.

Alisema huo utaalam ni mzuri na kama akiuleta Tanzania utasaidia kurejesha imani iliyotoweka kwa watu wenye uhitaji maalum na kutaisaidia Mahakama ya Tanzania kutoa haki kwa wakati na kupunguza mlundikano wa mashauri ya aina hiyo ambayo, aidha yanasubiria wakalimani ambao ni wachache kupatikana ama kutokana gharama kubwa kuwapata na hivyo kuchangia ucheleweshwaji wa umalizwaji wa mashauri ya aina hiyo.

‘’Hii teknoloji ipo tayari na nitawapatia ili iweze kusaidia katika kutatua migogoro ya watu wenye uhitaji maalum, mkishamaliza kujadiliana na kukubaliana, basi nitaipa hii teknoloji Mahakama ya Tanzania ili kuweza kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili’,’ alisisitiza Bw. Mukiza.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma (katikati) pamoja na Jaji Arufani Kweka (wa kwanza kulia kwa Jaji Maruma) wakiwa na wadau wengine kwenye mjadala namna ya kuboresha huduma za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa watu wenye uhitaji maalum kwa kutumia teknolojia.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya ESS Creative Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza wakijadili jambo katika kikao hicho.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya ESS Creative Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza (wa kwanza kushoto) pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mbando wakiwa katika kikao hicho wakijadiliana namna ya kuboresha huduma za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa watu wenye uhitaji maalum kwa kutumia teknoloji.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni