Ijumaa, 9 Agosti 2024

ZOEZI LA KUDIJITI NYARAKA ZA ZAMANI MAHAKAMANI LAANZA

Na. SALUM TAWANI-Mahakama, Dar es Salaam

Zoezi la kudijiti nyaraka za Mahakama ya Tanzania limeanza kwa kutambaza (scanning) maamuzi ya miaka ya nyuma kuanzia mwaka 2018 kurudi mpaka mwaka 1980.

Uamuzi wa kutambaza maamuzi hayo utasaidia kuyaifadhi kidijitali na pia kupandishwa katika mfumo unaochapisha maamuzi mtandaoni (TanzLII).

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert, hivi karibuni alitembelea Maktaba ya Mahakama ya Rufani Jijini Dar es Salaam na kujionea zoezi hilo linaloendelea.

Zoezi hilo linatokana na mradi wa kupandisha maamuzi ya miaka ya nyuma ambao ni matokeo ya Mkutano wa Wadau uliofanyika tarehe 13 na 14 Julai, 2023 Jijini Dodoma. 

Wadao hao walitoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mchapaji Mkuu wa Serikali, Tume ya Kurekebisha Sheria, Mwakilishi  Maktaba ya Mahakama ya Tanzania, AfricanLII pamoja na GIZ, kampuni ya Kijerumani

Mkutano huo ulihusisha ushirikiano kwenye upatikanaji wa maamuzi na sheria bure mtandaoni na kuwezesha zoezi hilo kuanza mnamo tarehe 29 Julai, 2024.

Akizungumza akiwa kwenye Maktaba hiyo, Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania alisema kuwa zoezi hilo linaloendelea litasaidia kuongeza chachu na kasi ya ufanyaji tafiti za kisheria na upatikanaji wa rejea za maamuzi ya Mahakama.

Mhe. Herbert alieleza kuwa zoezi hilo pia litasaidia uharakishaji wa utoaji haki kwa wakati na haraka kutokana na upatikanaji wa nyenzo za ufanyaji tafiti kupitia kwenye Mfumo wa TanzLII kirahisi.

“Hili zoezi ni zuri na la msingi sana kwa kuwa maamuzi ya zamani huwa ni ngumu kuyapata. Hatua ya kuyatambaza maamuzi haya ni jambo jema na linaloleta tija ndani ya Mahakama na kwa jamii kwa ujumla... 

“Maamuzi haya yatadumu kwa muda mrefu kwa kuwa sasa yapo kidijitali, hivyo upatikanaji wake utakuwa rahisi na pia Mahakama ya Tanzania inahamasisha kuwa na nyaraka laini kuliko nyaraka ngumu,” alisema.

Naye Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi, akizungumza wakati wa kushuhudia zoezi hilo, alisema kuwa uamuzi wa kuyatambaza maamuzi hayo ni jambo la busara, kwani litasaidia kurahisisha ufanyaji tafiti kwa urahisi na haraka na kuwasiaidia Majaji na Mahakimu kutoa haki kwa haraka na kwa wakati. 

Alisema pia kuwa maamuzi hayo ni ya thamani, hivyo yakibaki katika hali ya nakala ngumu ni rahisi kuharibika na kuleta ugumu kwenye tafiti. Mhe. Mlingi alibainisha kuwa zoezi la utambazaji wa maamuzi hayo litayafanya yaishi kwa muda mrefu zaidi na kupatikana kirahisi.

Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho, alisema kuwa utambazaji wa maamuzi hayo utasaidia tafiti za kishera na rejea kirahisi na kusaidia zoezi zima la utoaji haki kuwa la haraka.

Aidha, Mhe. Kariho alieleza kuwa kwa Maafisa wa Mahakama na wadaawa kupata maamuzi ya zamani kidijitali itasaidia uboreshaji wa misingi ya kisheria na ujenzi mzuri wa hoja katika kutafuta haki.

Katika zoezi hilo, maamuzi ya zamani 5,424 ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ya miaka kuanzia 1980 hadi 2018 tayari yametambazwa na maamuzi 1,430 ya Mahakama ya Rufani kwa miaka hiyo, yametambazwa. 

Kazi hii ilianza tarehe 29 Julai, 2024 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2024, kwa Kanda za Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi na Mwanza.

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert (wa kwanza kulia) akiwa na akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Maktaba na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho huku wadau wengine wakiangalia namna maamuzi ya zamani yanavyotambazwa ili yaweze kupandishwa kwenye mfumo unaochapisha maamuzi mtandaoni (TanzLII).

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert (wa tatu kulia) akiwa na Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mlingi na wadau wengine wakishuhudia zoezi hilo la utambazwaji wa maamuzi ya zamani.

Mkurugenzi wa Maktaba na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho (wa kwanza kushoto) akiwa na wadau waliotembelea zoezi linaloendelea la kutambaza maamuzi ya zamani.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni